1/15/2021

Nini Kinasababisha Ajali Nyingi Za Ndege Indonesia?Usafiri wa ndege duniani kote unaaminika kwamba ndiyo salama kuliko aina nyingine zote za usafiri! Hata hivyo, si mara zote usafiri huo huwa salama!

Nchini Indonesia, ukiachana na ajali ya hivi karibuni iliyotokea Januari 9, 2021 ikiihusisha ndege ya abiria, Boeing 737-500, mali ya Shirika la Ndege la Sriwijaya iliyosababisha vifo vya watu wote… waliokuwa ndani ya ndege hiyo, kumekuwa na rekodi mbaya ya usalama wa usafiri wa anga huku nchi hiyo ikitajwa kuongoza kwa kuwa na ajali nyingi za ndege barani Asia kuliko nchi nyingine yoyote.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mtandao wa Statista.com, tangu mwaka 1971, jumla ya ajali kubwa 16 za ndege zimetokea nchini Indonesia, na kusababisha jumla ya vifo 1,798, idadi ambayo ni kubwa kuliko nchi nyingine yoyote katika bara la Asia.

Download App ya Udaku Spesho HAPA

Takwimu nyingine kutoka katika Mtandao wa Aviation Safety Network, zinaonesha kwamba tangu mwaka 1945, jumla ya ajali za ndege 103 zimetokea nchini Indonesia na kuifanya nchi huyo kuwa miongoni mwa nchi hatari zaidi kwa usafiri wa anga.

Swali ambalo unaweza kujiuliza, usafiri wa ndege unatumika duniani kote, watu wanasafiri salama kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine, kwa nini hali ni tofauti nchini Indonesia? Kwa nini nchi hiyo inaongoza kwa ajali za ndege?


Sehemu ambayo ni hatari zaidi nchini humo, ni katika Bahari ya Java ambako asilimia kubwa ya ajali zinazotokea, zimekuwa zikitokea kwenye bahari hiyo.


Kabla hatujaendelea na uchambuzi huu wa kina, pengine itakuwa bora nikikukumbusha ajali kubwa na za kutisha zilizotokea nchini Indonesia na idadi ya vifo vilivyotokana na kila ajali.

BAADHI YA AJALI KUBWA ZA NDEGE INDONESIA

Septemba 26, 1997, Ndege ya Shirika la Garuda Indonesia, Airbus A300B4 iliyokuwa inatoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Soekarno-Hatta jijini Jakarta kuelekea Uwanja wa Ndege wa Polonia ilipata ajali mbaya ikiwa na abiria 222 na wahudumu wa ndege 12.

Watu wote 234 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walipoteza maisha na ndiyo ajali iliyoweka rekodi ya kusababisha vifo vingi zaidi katika historia ya usafiri wa anga nchini humo.

Sababu kubwa ya ajali hiyo, inatajwa kuwa ni ukungu uliosababisha rubani ashindwe kuona mbele na kugonga kingo za mlima.


Oktoba 29, 2018, ndege nyingine kubwa, Boeing 737 MAX iliyokuwa inamilikiwa na Shirika la Lion Air, ikitokea Soekarno–Hatta kuelekea Pangkal Pinang nchini humo, ikiwa na jumla ya abiria 189, ilipata ajali katika Bahari ya Java, dakika kumi na tatu tangu ipae.


Ajali hiyo inatajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya Shirika la Lion Air na ajali mbaya zaidi ikihusisha ndege mpya za Boeing 737 MAX zilizozinduliwa mwaka mmoja tu kabla, 2017.

Desemba 28, 2014, Ndege ya Shirika la Indonesia AirAsia, Airbus A320 ikitokea Surabaya nchini Indonesia kuelekea Singapore, ikiwa na abiria 162 ilipata ajali katika Bahari ya Java na kusababisha vifo vya watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo.


Sababu za ajali hiyo, zilikuja kuelezwa kwamba ni hitilafu katika mfumo wa rada, ambazo zilitoa taarifa zisizo sahihi kwa rubani na kusababisha ajali hiyo. Ni miili ya watu 116 tu ndiyo iliyopatikana, kati ya watu 162 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Download App ya Udaku Spesho HAPA


Hizo ni baadhi tu lakini zipo ajali nyingine kibao, ikiwemo ya Mandala Airlines Flight 091 iliyopata ajali na kusababisha abiria 149 kupoteza maisha huku 17 wakinusurika, ajali ya ndege ya Pan Am, Boeing 707-321B iliyosababisha vifo vya watu 107  na nyingine nyingi.

NINI KINASABABISHA AJALI NYINGI ZA NDEGE INDONESIA?

Zipo sababu nyingi ambazo zimekuwa zikianishwa kwenye kila ajali inayotokea lakini sababu za msingi zimekuwa ni pamoja na uzembe wa marubani, mafunzo duni wanayoyaopata marubani nchini humo, matatizo katika mifumo ya kuongozea ndege angani, uchakavu wa ndege na hali mbaya ya hewa hasa katika Bahari ya Java.

Unapojaribu kuchimba kwa undani kutaka kujua kwa nini Indonesia ina ajali nyingi zaidi za ndege kuliko nchi nyingine yoyote, utagundua kwamba sababu za msingi ni zilezile ambazo zimekuwa zikijirudia, ambazo unaweza kuzigawanya katika makundi matatu; sababu za kiuchumi, sababu za kijamii na sababu za Kijografia. Kivipi?

Kwa kipindi kirefu, tangu muasisi wa taifa hilo na rais wa kwanza, Kusno Sosrodihardjo almaarufu Sukarno alipopinduliwa madarakani Machi 12, 1967, nchi ya Indonesia ilikuwa ikitawaliwa kidikteta na Rais Suharto Kertosudiro ambaye utawala wake uligubikwa na vitendo vya rushwa na ufisadi mkubwa, hali iliyosababisha uchumi wake kulegalega kwa muda mrefu.

Baada ya Rais Suharto kujiuzulu wadhifa wake huo mwaka 1998, uchumi wa nchi hiyo ulianza kukua kwa kasi kubwa, biashara nyingi zikafunguliwa na kuanza kushamiri. Miongoni mwa biashara iliyoanza kukua kwa kasi nchini humo, ilikuwa ni usafiri wa ndege.

Zipo sababu nyingi zilizosababisha kukua kwa usafiri wa anga nchini humo tofauti na usafiri wa aina nyingine, sababu kubwa ikiwa ni Jografia ya nchi hiyo sambamba na miundombinu mibovu ya barabara.

Kwa taarifa yako, Indonesia ni mkusanyiko wa visiwa zaidi ya elfu 17 na inatajwa kuwa nchi ya nne duniani kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu, ikiwa na wakazi milioni 267. Utawala wa Kidikteta wa Rais Suharto, ulisababisha nchi hiyo iwe na miundombinu mibovu ya barabara ambazo hazipitiki kwa urahisi na bandari zisizo na ubora.

Ukiachana na sababu hizo, sababu nyingine ni hali ya hewa. Indonesia ina hali ya hewa ya Kitropiki, ambapo baadhi ya maeneo huwa na kiwango kikubwa cha mvua kwa mwaka, kiwango kikubwa cha ukungu sambamba na pepo zenye nguvu zinazovuma kutoka baharini, ambazo zimekuwa zikisababisha vimbunga na dhoruba kubwa hasa katika Bahari ya Java. Pia Indonesia inapitiwa na mikono bahari miwili, Lombok na Sapi, inayotajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa hali ya hewa nchini humo.

Tangu kuondoka madarakani kwa Rais Suharto, usafiri wa anga ulionesha kuwa rahisi zaidi kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine nchini Indonesia. Kuongezeka kwa biashara, kukawa kunawalazimu wafanyabiashara wengi kuwa wanasafiri mara kwa mara na kwa haraka kupitia ndege.

Serikali iliyoingia madarakani baada ya Suharto kujiuzulu, ilishindwa kukabiliana na ukuaji wa kasi wa sekta ya usafiri wa anga, makampuni na mashirika mengi ya ndege yakawa yanazidi kuanzishwa, bei za usafiri wa ndege zikapungua kutokana na ushindani mkubwa.

Kukosekana kwa usimamizi wa kutosha wa serikali na mamlaka za usafiri wa anga, kulisababisha ndege nyingi chakavu zianze kuingizwa nchini humo, marubani wasio na vigezo vya kutosha wakawa wanaajiriwa kwa wingi, ukaguzi wa ndege ukawa haufanyiki kikamilifu na hapo ndipo matatizo makubwa yalipoanza kujitokeza. Ajali za ndege zilianza kuongezeka kwa kasi mwishoni mwa miaka ya 1990 na kusababisha maafa makubwa


MASHIRIKA YA NDEGE YA INDONESIA YAFUNGIWA MAREKANI NA ULAYA

Kutokana na wimbi hilo la ajali, mwaka 2007 Marekani ilizifungia kampuni na mashirika yote ya ndege ya Indonesia kuendesha shughuli zake ndani ya mipaka ya Marekani, ikiituhumu serikali ya Indonesia kutokuwa makini katika usimamizi wa makampuni hayo.

Zuio hilo lilikuja kuondolewa mwaka 2016 baada ya serikali kupitia mamlaka ya usafiri wa anga, kuonesha juhudi kubwa katika kuboresha usafiri huo na kuzuia ajali zinazoweza kuzuilika kwa kuongeza umakini.

Si Marekani pekee, hata nchi za jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU), pia ilizipiga marufuku kampuni na mashirika ya ndege kutoka Indonesia kuendesha shughuli zake katika anga na ardhi ya umoja huo, kwa kushindwa kudhibiti ajali hizo za ndege. Zuio la Umoja wa Ulaya liliondolewa rasmi mwaka 2018.

Uchunguzi uliofanywa na Mtandao wa AirlineRating.com chini ya kiongozi wake, Geoffrey Thomas ndiyo uliowezesha Indonesia kutolewa katika zuio hilo ambapo ripoti iliyotolewa na mtandao huo, ilionesha kwamba kumekuwa na ukaguzi wa mara kwa mara wa ndege nchini Indonesia tofauti na awali, kumejengwa karakana nyingi kwa ajili ya ukaguzi na matengenezo ya ndege na mafunzo ya urubani nchini humo yameboreshwa.

Ajali iliyotokea Januari 9, 2021 inaweza kuirudisha Indonesia kwenye kifungo kingine cha kufanya shughuli zake Marekani na kwenye jumuiya ya umoja wa Ulaya na hiyo itatokana na ripoti inayosubiriwa, juu ya nini hasa kilichosababisha ajali hiyo ya ndege.

Kwa kifupi hizo ndiyo sababu za Indonesia kuwa na idadi kubwa ya ajali za ndege, zinazosababisha vifo vingi vya nguvukazi ya taifa hilo.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger