Rais Yoweri Museveni 'Sitaki Kupatanishwa na Wapinzani'

advertise here


Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameonya watu wenye lengo la 'kumpatanisha' yeye na upande wa upinzani baada ya kumalizika uchaguzi mkuu uliompa ushindi kuongoza muhula wa sita. Huku upande wa upinzani unaoongozwa na msanii Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliyeshika nafasi ya pili miongoni mwa wagombea 11 akipinga vikali kutambua matokeo hayo.Kauli hiyo imekuja baada ya kuibuka wasiwasi kwa taifa na baadhi ya viongozi wa dini kuomba maridhiano kwa serikali na upinzani. Katika maadhimisho ya miaka 35 ya chama cha NRM kuingia madarakani yaliyofanyika Ikulu ya nchi hiyo siku ya Jumanne, viongozi wa Kanisa Katoliki katika sala ya kuliombea taifa, waliomba Rais Museveni kufanya maridhiano na kumuachia kiongozi wa chama cha upinzani cha NUP, Robert Kyagulanyi aliyekuwa amezuiliwa nyumbani kwake.


Rais Museveni aliwajibu akisema, serikali ya NRM tayari ilianza maridhiano miaka mingi iliyopita ndio sababu katika serikali yake kuna mwana wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin , mwanae Rais wa zamani Tito Lutwa Okello na wengine wengi.


''Fikiria kuna baadhi ya watu wanaokuja kwangu wanataka kuwa wapatanishi wangu na upande wa upinzani, 'kunipatanisha' nini? sitaki 'upatanishi' wowote.''Alisema Rais Museveni. ''Kila mtu anafahamu mahala pangu na mimi ninafahamu mahali upinzani wanapopatikana ninaweza kwenda kwao tukazungumza, sitaki upatanisho wowote, ni matusi kuniambia unataka kunipatanisha.'' Aliongeza Museveni .


Kiongozi wa chama cha NUP Robert Kyagulanyi alipokutana na wabunge wake wateule siku ya Jumanne kwa mara ya kwanza, aliwataka wapinge matokeo ya uchaguzi mkuu . ''Tuna ushahidi wa kutosha na nyinyi mnafahamu kuwa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi alitangaza matokeo ambayo si ya kweli na kwanza tunapinga udanganyifu huo, na sasa tuko kwenye mazungumzo tuone kama tunaweza kupeleka kesi Mahakamani''. Alisema Kyagulanyi. Awali vyombo vya habari nchini humo vilimnukuu Rais Museveni akisema kuwa yuko tayari kufanya maridhiano na yeyote ambaye anamsimamo tofauti na ule wa chama tawala cha NRM.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE