2/09/2021

Aliyetuhumiwa kutumikisha walemavu afariki dunia.MFANYABIASHARA Sadikiel Meta, 71 aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa omba omba amefariki dunia.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 9,2021 na wakili anayemtetea mshtakiwa huyo Robert  Langeni baada ya kesi hiyo kuitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa

"Mteja wangu amefariki tangu Januari  28 mwaka huu katika Hospitali ya Temeke alipokuwa amelazwa", amesema wakili Langeni.

Mapema wakili wa serikali Kija luzungana alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi
, Kassian Matembele wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini hana jalada la uchunguzi la kesi

Hata hivyo mahakama haikusema lolote juu ya taarifa hiyo ya kifo kutoka kwa wakili wa mshtakiwa na ikiahirisha kesi hadi Februari 23, 2021 itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa

Katika kesi hiyo Meta anashtakiwa na wenzake 14  ambapo mbali na shtaka la kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa omba omba mashtaka mengine ni usafirishaji haramu wa binadamu,  kutakatisha fedha,  kukwepa kulipa kodi na ba kuisababishia serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hasara ya zaidi ya sh. Milioni 31.3


Mbali na Meta baadhi ya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Yusuph Mohamed (35), Yusuph Magadu (20), Emmanuel Salu (20) Gogad Mayenga (18), Samson Taruse (26), Hussein John (18), Zacharia Paul (18), Dotto Shigula (19), Petro Simon (21), Emmanuel Sahani (38), Joseph Mathias (20), Masanja Paul (21), Aminiel Sangu (19), na Emmanuel Lusinge.

Wanadaiwa kati ya mwaka 2020 na Januari Mosi 2021 jijini Dar es Salaam,  kwa pamoja walishiriki kufanya uhalifu wa kupanga kwa kuongoza genge la uhalifu na kutekeleza kufanikisha kusafirisha binadamu kwa haramu.

Pia katika shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu inadaiwa, katika kipindi hicho hicho huko Tandale ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mshtakiwa Meta na Mohamed waliwatumikisha walemavu 37 na kuwafanya wawe omba omba wa  mtaani kwa lengo la kujipatia kipato.

Miongoni mwa wa walemavu hao ni mtoto Kashinje Emmanuel,  mwenye umri wa miaka saba, Doto Silas Happines Bezagurwa, Neema Edward na  Peter Sereke wote wa ama umri wa miaka 11.

Imedaiwa wa washtakiwa hao pia walikuwa wakisafirisha walemavu kutoka mikoa ya Shinyanga na Tabora kwenda Dar es Salaam na kwamba wakishapokelewa wanawaingiza kwenye shughuli za omba omba kwa lengo la kujipatia faida.

Aidha mshtakiwa Meta anadaiwa kushindwa kulipa kodi ya thamani ya Sh. 31,328,500.31 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) .
 
Pia mshtakiwa Meta anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 31.3.

Katika shtaka la mwisho la utakatishaji imedaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari Mosi 2021, mshtakiwa Meta alijipatia Sh. Milioni 31,328,500.31 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kushindwa kulipa kodi.


MFANYABIASHARA Sadikiel Meta, 71 (pichani kushoto enzi za uhai wake) aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa omba omba amefariki dunia.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger