Mwanadada Fatema Dewji ametangazwa kuwa mlezi wa timu ya wanawake (Simba Queens) hii leo na CEO wa klabu ya Simba Barbara Gonzalez.
“Namtangaza Fatema Dewji kuwa mlezi wa timu yetu ya wanawake (Simba Queens). Ni mwanasimba kindakindaki na ana uzoefu mkubwa kwenye masuala ya masoko.”- CEO Barbara Gonzalez.
Mara baada ya kutangazwa Fatema Dewji ameahidi kufanya makubwa hasa kutokana na utaalamu wake wa kuwa na ubobezi wa maswala ya masoko.
”Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani kwenu wote kwa kunipa nafasi ya kusimama na kuzungumza nanyi, kisha niwashukuru sana sana Bodi ya Simba Sports Club kwa imani na mapenzi yao juu yangu kwa kunichagua kuwa Mlezi au Patron wa timu ya Simba Queens,”- amesema Fatema.
Fatema Dewji ameongeza ”Naahidi kufanya kazi nzuri na kubwa pamoja na Wasichana hawa mahodari na Utawala wake, Bodi, wanachama na mashabiki wa Simba kuhakikisha kwa pamoja kuwa tunabakiza kombe la Ligi Kuu ya Wanawake kwa Simba Queens na pia tunafuzu kuingia kwenye Champions League.”
”Kutokana na utaalamu wangu wa kuwa na ubobezi katika masuala ya masoko, nitahakikisha kuwa vipaji na uwezo walio nao Simba Queens unatambulika hapa Tanzania na nje na uwe na uzito kufana na timu ya simba.”
”Pia naahidi kuweka nguvu katika kutafuta na kukuza njia za upatikanaji wa rasi limali ili kuiboresha Timu pamoja na wasichana hawa. Asanteni sana!”