Paula pokea simu ya dada yako Lulu

 

By Dk Levy
 

Paula wewe ni msichana mwenye sura nzuri. Shepu mujarabu na rangi amazing. Yes lazima upewe sifa Paula. Labda tuamue tu kupingana na Mungu Mwenyezi, aliyekuumba uwe hivyo ulivyo. Kazi yako kubwa ni kumrudishia shukurani zake tu.

Paula! Picha linaanza kwanza wewe ni mtoto wa mastaa. Mama anajulikana sana, baba anatambulika kinoma. Upewe nini Paula? Kuwa mtoto wa hao wazazi wawili ni ustaa tosha. Uhitaji kuwa karibu na staa yeyote ili uwe staa mama.

Mastaa unaowashobokea leo. Miaka miwili nyuma wengi walikuwa wanaota tu. Kukaa karibu na mama au baba yako hakuna staa yeyote wa kukutia huzuni na unyonge Paula. Hata wanaokupenda na kukuthamini ni kwa sababu wewe ni mtoto wa Kajala na P Funk.

Paula unataka nini? Shule uliyosoma ya kishua kinoma. Unaowashobokea leo, koo zao zote hazijawahi kusoma au kusomesha mtoto pale. Hata robo ya ada yako kwa mwaka kwao ingekuwa kama jinamizi. Kwa nini leo wawe kikwazo cha ‘fyucha’ yako?

Paula! Pindi ulipozaliwa mwanzoni mwa miaka ya 2000. Elizabeth Michael, ‘Lulu’, hakuwa ametimiza hata miaka saba. Alikuwa mdogo. Lakini akawa maarufu kuliko mama yako Kajala. Kifupi Kajala alikuwa miongoni mwa viumbe wa kike waliotamani kufahamiana na Lulu.

Mzee wako P Funk Majani. Tunaweza kusema aliishi katika kivuli cha ustaa kama Lulu. Naongelea kipindi ambacho Diamond Platinumz yuko Tandale huko, akiwa darasa la saba au kidato cha kwanza. Rayvanny ndio kabisa, alikuwa Nzovwe Mbeya akihesabu a,e,i,o,u.
 
Paula, unaweza kuwa mtu makini sana. Lakini upumbavu huja baada ya pesa na umaarufu. Hakuna jambo gumu kama kupata umaarufu na pesa utotoni. Kuvuka na umaarufu huo katika daraja lile lile kwenye umri wa utu uzima ni ngumu mno. Waliweza kina Michael Jackson.

Angalau kina Chris Brown na Justin Bieber. Na kwa upande wa wanawake wapo kina Beyonce. Ambao wameanza kupata umaarufu na pesa utotoni. Na wakafanikiwa kuvuka daraja la utu uzima katika usawa uleule. Pesa nyingi na umaarufu mkubwa.

Paula, watu wanampenda mtoto kwa utoto wake. Kwa sababu ya sura ya kitoto, sauti ya kitoto. Kuingia katika utu uzima ni kazi nyingine kubwa ya kuwashawishi watu wakupende ukiwa na mwonekano mpya wa sura, umbile na sauti. Ni ngumu sana.

Watu wanakuzoea kwa utoto wako. Kuhama nao kwenye utu uzima lazima uwe na kitu cha ziada. Ni kazi mno. Wazungu wengi walishindwa hiki. Ukianza kuwa na boy/girl friend. Au sauti kuanza kutoa ‘bezi’, mashabiki wengi hujitenga nawe.

Elizabeth Michael maarufu kama Lulu. Aliingia kwenye daraja la kina Beyonce, Lil Wayne, Justin Bieber na King Michael Jackson. Alipendwa akiwa bado mtoto. Akapendwa akiwa mtu mzima. Aliigiza utotoni akapendwa, leo anaigiza katika utu uzima, anapendwa vilevile.

Mtihani aliovuka ni mzito kuliko ule aliofanya pale Magogoni. Paula, kuwa Lulu huyu huyu wa Majizo, usichukulie poa. Hata upuuzi wake wa miaka ya nyuma ilikuwa akili ya utoto. Lakini ‘kujibrandi’ kutoka katika taswira mbaya mpaka njema, ni kitu kikubwa sana.

Paula, alichofanya Lulu ni kubadilika jumla baada ya mitihani mizito. Wewe usisubiri yakutokee na Kanumba wako ndipo ubadilike. Huu ni wakati wako wa kuachana na drama. Kuachana na ujinga na kufuata msingi wa maisha ya binti wa Kiafrika.

Huwezi kuwa pisi kali kama huna akili kichwani. Kwanza Paula kwa urembo wako unatokaje na mtu mwenye familia? Mtoto wa mastaa unatakiwa uwe na elimu kubwa. Adabu, heshima na ndoto kubwa kubwa. Usiwe poyoyo Paula.

Leo hii mtazame Lulu, ana maisha poa tofauti na mastaa wengi wa kike. Hata kukomaa na elimu siyo wote walioweza. Paula, hata nia tu ya Lulu kujiendeleza kielimu ni sehemu ya tofauti yake na wengi. Wale ambao walianza kupata pesa na ustaa utotoni.

Paula, mastaa wa kike wako wangapi? Kabla hujajiuliza kuwa mbona Lulu yeye anapata wenye pesa tu? Mwenye pesa nyingi ina maana mjanja. Ana akili na uelewa katika utafutaji. Sasa mwenye akili, uelewa na pesa nyingi anakuaje na demu boya?

Paula, huyu Lulu ana kitu cha ziada sana. Taswira yake ya utotoni ni ngumu leo hii kuwa pale alipo. Kuwa pale ina maana ana kitu cha ziada. Hata Wayne na Justin Bieber, Marekani wanawaheshimu kutokana na kuvuka daraja ambalo Bow Wow, Lil Romeo na wenzao walishindwa.

Paula, huyo Lulu kaweza kushaini utotoni na ukubwani kwenye tasinia ya sanaa. Ni zaidi ya kupata Masters na PhD. Amini hilo Paula. Kuwa Lulu kashinda mtihani mkubwa sana katika maisha ya ustaa kutoka utotoni. Wengi huishia vibaya.

Mwisho wao au kinachoendelea kwao kila mtu anajua. Lakini Lulu kaweza. Maisha yake akiwa bado chini ya miaka 18, siyo haya aliyonayo hivi sasa. Paula wakati mwingine dada zako kama Lulu, watazame kwa jicho la tatu. Itakupa urahisi wa mafanikio.

Lulu angekuwa katika maisha fulani, angekuwa mbali kielimu na kimaisha. Lakini kwa maisha haya ya Bongo Movie, huenda ndiye msanii pekee mwenye umri mdogo. Lakini ana elimu, maisha ‘klasiki’ kuliko wasanii wengi wa kike. Kutokana tu na akili yake.

Paula usikariri kuwa ukiwa mzuri na staa wa kike utapata maisha bora. Kuna kitu cha ziada kwenye maisha tuliyoumbiwa na Mungu. Kwa wewe una nafasi kubwa sana ya kuendelea na elimu. Maana ndio ndoa (elimu) pekee isiyo na talaka. Amini hili Paula.

Cha kufanya ulizia Lulu anamaliza lini ‘honeymoon’ na Majizo. Mtumie meseji kisha usizime simu yako. Akipiga pokea fasta ili akupe madini. Kwa sababu haya mambo unayoyaishi leo, yeye kayaishi mara 100 zaidi yako. Lakini akaona siyo issue akaamua kubadilika jumla. Paula pokea simu ya Lulu.

Mwananchi

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE