Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Serikali Yasema SGR Haitakuwa na Tatizo la Umeme


SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa Treni ya Kisasa (SGR) haitakuwa na tatizo la umeme, kwa sababu mabehewa yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi umeme wa ziada kwa saa moja hadi mbili.

 

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, alibainisha hayo mwishoni mwa wiki mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari na Shirika la umeme Tanzania (Tanesco).

 

Dk Kalemani alisema kumekuwa na wasiwasi kuhusu umeme utakaotumika katika uendeshaji wa SGR, lakini hilo halipaswi kuwa tatizo, kwani mabehewa yatakayoendesha mradi huo yatakuwa ya kisasa.

 

“Kumekuwa na wasiwasi kwamba umeme unaweza ukakatika na hivyo treni hii isiweze kutembea, lakini ukweli ni kwamba mabehewa yatakayokuja katika mradi huu ni mabehewa yanayotumia teknolojia ya juu inayoweza kutunza umeme kwa saa moja hadi saa mbili. Kwa hiyo hata umeme ukikatika kwa dakika 10 bado SGR itaendelea kutembea,”alisema.

 

Dk Kalemani alisema hadi sasa Tanesco imekamilisha uwekaji wa umeme katika kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilometa 160 na kwamba hata mradi huo ukitaka kuanza leo, wako tayari kuuendesha kwa kuwa nishati hiyo ipo.

 

Alisema wamefunga minara 456 katika njia hiyo inayoanzia Dar es Salaam hadi Kingolwira na kwamba serikali imetumia Sh bilioni 71.1 kukamilisha kipande hicho.

 

Reli hiyo ya kisasa itaunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa lengo la kupunguza gharama za usafiri, muda wa kusafiri, ufikishaji rahisi huduma za jamii kwa jumuiya ya eneo la mradi na uwezeshaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi za jirani.

 Tazama Hapa Chini Msanii Rosa Ree Akimkemea Shetani:


  DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL => HAPA KUPATA HIZI HABARI KWENYE SIMU YAKO HATA BILA BUNDLE


Post a comment

0 Comments