BAADA ya uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na mdhamini wao Kampuni ya GSM, kusikia nia ya mfadhili wao wa zamani Yussuf Manji kurejea ndani ya Klabu hiyo, tayari wamejiongeza kwa kuwaahidi wachezaji wao kitita cha shilingi milioni 300, endapo watafanikiwa kushinda Kombe la FA msimu huu.
Yanga ipo kwenye hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), ambapo mchezo ujao inatarajiwa kukipiga dhidi ya Tanzania Prisons.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ipo kileleni ikiwa na pointi zake 54, baada ya kucheza mechi 25, huku Watani wao Simba wakiwa nyuma yao na ponti 52, baada ya kushuka dimbani mara 22.Chanzo chetu makini kimeliambia Championi Jumatano kwamba, uongozi wa Yanga kwa sasa umeamua kuwekeza matumaini yao makubwa kwenye michuano ya Kombe la FA, baada ya kuanza kuona dalili za wazi za kukosa ubingwa.
“Hatimaye sasa kwetu furaha inazidi kutawala, maana tangu kumekuwepo na taarifa za Manji kuonyesha nia ya kurejea kikosini sasa wadhamini wetu GSM wamekuwa wakimwaga neema ya fedha kila kukicha na lengo lao hasa ni kuhakikisha wanaweka historia ya kuchukua kombe hata moja.
“Taarifa za Manji zimewafanya mabosi zetu kujikuta wakitangaza kuweka mezani kiasi cha shilingi bilioni moja, huku mchanganuo wake ukijigawa kwa milioni 700, kama timu itafanikiwa kupata ubingwa na hizi milioni 300 kama tutabeba FA,” kilisema chanzo hicho.
GPL