ATCL Yasitisha Safari Zake Kwenda India

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imesitisha safari zake za ndege kati ya Dar as Salaam na Mumbai (India ) kuanzia tarehe 4 mwezi Mei hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine ya kurudisha safari hizo.

 

Hatua hiyo ni kutokana na kuwepo kwa ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini India. Kwa sasa India inakabiliwa na janga kubwa la virusi vya corona. Hospitali zimelemewa kwa kuwa na wagonjwa wengi na ripoti za watu kufariki mitaani zikiongezeka.

 

Mataifa ya Afrika yanategemea kupata chanjo kutoka India kwa kutumiwa mpango wa Covax . Ingawa ongezeko la maambukizi limesababishwa kupiga marufuku usafirishaji wa chanjo hizo na kuangazia watu wake kwanza.

 

Malawi ilipiga marufuku pia wasafiri wanaotoka India, pamoja na Bangladesh, Brazil na Pakistan kutokana kusambaa kwa virusi vya corona katika mataifa hayo.

 

Hali ilivyo India

Siku ya Jumanne watu walioambukizwa virusi vya corona ilifikia watu zaidi ya 355,000 idadi ikiwa ya chini ikilinganishwa na zaidi ya 400,000 tarehe 30 mwezi Aprili.

 

Idadi ya maambukizi ” inashuka”, serikali ilisema , lakini idadi ya wanaopimwa imepungua hivyo maambukizi yanaweza kuwa juu. India imelemewa na maambukizi ya virusi vya Corona na taifa hilo limevunja rekodi kwa maambukizi mengi kwa siku za hivi karibuni.

 

Hospitali nyingi katika jiji la Delhi pamoja na miji mingine mingi zimezidiwa na wagonjwa wa mlipuko wa corona, hali inayowalazimu watu kufanya mipango ya wagonjwa wao kutibiwa nyumbani.

 

India imekuwa ikiripoti zaidi ya wagonjwa 300,000 kwa siku, na idadi hiyo kubwa ya wagonjwa imeuzidi uwezo wa mfumo wa matibabu nchini humo.Nyingine zilizositisha safari za kwenda na kutoka India

Si Tanzania pekee kwa upande wa Afrika Mashariki iliyositisha safari za ndege kwenda nchini India. Kenya imesitisha kwa muda safari za ndege za abiria wanaotoka India. Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona nchini India.

 

Kagwe alisema ‘ hali nchini India imekuwa mbaya sana…. Na kulazimu kuzuiwa kwa safari za ndege kwa siku 14 zijazo.’ Uganda nayo ilipiga marufuku safari zote za ndege kutoka India kuanzia tarehe 1 mwezi Mei ili kuzuia wimbi jingine la janga la corona nchini humo.

 

Waziri wa Afya nchini humo Ruth Aceng alisema serikali ilichukua hatua mbali mbali ili kuzuia kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi hivyo. Hata hivyo kuna safari kutoka India ambazo Uganda ilisema hazitaathiriwa na marufuku hiyo na ni pamoja na;

 

Safari za ndege za mizigo ambazo wahudumu wake hawataruhisiwa kutoka kwneye ndege zao. Kusimama kwa muda wa safari za ndege ambapo abiria hawashuki. Ndege ambazo zitapatawa na hali ya dharura.

 

Operesheni zinazohusiana na misaada ya kibinadamu ,misaada ya matibabu na huduma za uokoaji zilizoidhinishwa na mamlaka husika. Raia wa Uganda wanaorejea nyumbani kutoka India kwa matibabu.

 

Nchi nyingine zilizopiga marufuku safari za ndege India ni pamoja na Canada, falme za kiarabu na Uingereza -marufuku zilizoanza kutekelezwa jumamosi iliyopita lakini hazitathiri ndege za kubeba mizigo.Hatua za tahadhari

Siku ya jumatatu Serikali ya Tanzania ilitoa muongozo mpya kuhusu ugonjwa wa corona ambapo wasafiri watakaokuwa wanatoka katika nchi zenye maambukizo ya virusi vipya vya corona watatakiwa kukaa karantini kwa siku 14.

 

Muongozo huo uliosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo Profesa Abel Makubi ulianza kufanya kazi Mei 4 2021, unaeleza kuwa karantini hiyo itawahusu wasafiri ambao ni wakaazi na wageni.

 

Kabla ya kwenda karantini kwanza watafanyiwa vipimo vya lazima vya corona. Kwa wageni watatakiwa kukaa karantini kwa gharama zao “watachagua eneo moja katika orodha itakayotolewa na serikali.”

 

Wasafiri ambao ni wakaazi wa Tanzania wataruhiswa kujitenga kwa siku 14 katika nyumba zao wenyewe. Mwezi mei mwaka jana Tanzania iliondoa karantini ya lazima kwa wasafiri kutaka nje ya nchi hiyo na badala yake wakatangaza kuwa kutafanyika vipimo vya ugonjwa huo.

 

Wizara ya Afya ya Tanzania imeeleza kuwa nchi hizo zenye virusi vipya vya corona zitatambuliwa kupitia taarifa zinazotolewa kila siku na Shirika la Afya Duniani (WHO).

 

Kwa sasa virusi vipya vinavyogonga vichwa vya habari zaidi ni vya India na Brazil. Wataalamu wanatahadharisha kuwa idadi ya maambukizi inaweza ikawa kubwa zaidi ya hiyo.

 

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE