Diva Amchimba Zari, Apewa za Chembe Mtandaoni

WABONGO wenyewe wanasema wagombanao ndiyo wapatanao! Hicho ndicho kinachojiri kwa sasa kufuatia mtangazaji maarufu Bongo, Loveness Malinzi ‘Diva’ kukesha akimsifia staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.Ikumbukwe kwamba, Diva na Diamond au Mondi hawakuwa wakiivana chungu kimoja kwa miaka mingi kiasi cha chuki kutamalaki kati yao.

Kwa kipindi chote, Diva alikuwa shabiki kindakindaki wa mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kabla ya kuhamia kwa Rajab Abdul ‘Harmonize’.


 

DIVA ADAIWA KUMCHIMBA ZARI

Hata hivyo, kwa sasa Diva anasemekana kufika mbali zaidi kiasi cha kumchimba mzazi mwenza au baby mama wa Mondi, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.Kitendo cha Diva kuendelea kumsifia Mondi huku ikidaiwa kwamba, yupo tayari kuwa naye kimapenzi kimewaibua Team Zari na kumpa za chembe katika kipindi hiki ambacho wawili hao na watoto wao wawili, Tiffah Dangote na Prince Nillan wanajitanua huko nchini Afrika Kusini (Sauzi).

 

DIVA AANZA KUFUNGUKA

Baada ya kipindi kirefu, hivi karibuni Diva alianza kufunguka kwamba yeye ni shabiki namba moja wa Mondi hadi hapo atakapoingia kaburini na yupo tayari kupambana na yeyote atakayekuwa kinyume na staa huyo wa Wimbo wa Waah.Mbali na ishu za kimapenzi, Diva anasema kuwa anamkubali sana Mondi kwani anafanya kazi kwa bidii na anaona ameleta mabadiliko kwenye muziki.Diva anasema pamoja na kwamba Harmonize anafanya vizuri, lakini siyo sababu ya yeye kumshindanisha na bosi wake wa zamani; yaani Diamond.

 

Diva anasema kuwa, Diamond atabaki kuwa mtu aliyevumbua kipaji cha Harmonize na kumfikisha hapo alipo sasa hivi hivyo kumshindanisha naye inakuwa siyo jambo sahihi.“Mfano mimi, siku zote najivunia mabosi wangu Joseph Kusaga, marehemu Ruge Mutahaba na Gadner Habash (viongozi wa Clouds Media Group; mwajiri wa zamani wa Diva).

 

Wamenitengeneza, sasa ukianza kunifananisha nao sasa hivi kwa sababu tu nina wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, si sahihi, kwanza unakuwa huna adabu,” anasema Diva.

 

Diva anaongeza kuwa, wanaomshindanisha Diamond na Harmonize wanakosea na kusema kuwa licha ya yote hayo, kizazi tulichonacho ni kizazi cha Harmonize na ni mwanamuziki anayemkubali wengine watabaki kuwa malejendi tu

Kuhusu uvumi wa kwamba watu wanaomsapoti Harmonize ni wale wanaomchukia Diamond, Diva anasema kuwa si kweli kuhusu hilo kwani Harmonize ana mashabiki wake mwenyewe.

 

DIVA ADAI KUMPENDA MONDI

Lakini kubwa zaidi lililowaacha wengi midomo wazi ni baada ya Diva kumwambia Mondi kwamba hajui aanzie wapi, lakini ukweli ni kwamba anampenda!Sasa, baada ya Diva kudai hivyo ameibua maswali mengi na kujikuta akishambuliwa kama mpira wa kona na baadhi ya wafuasi wa Zari wakimtaka kukaa mbali na jamaa huyo kwa sababu kwa sasa ni mali ya mwanamama Zari.

 

Pamoja na kwamba Diva hakusema kama anampenda Mondi kivipi; yaani kikawaida au kimapenzi, lakini wafuasi wa Zari wanadai kwamba hana lolote zaidi ya kujitongozesha kwa staa huyo.

 

HAIWEZEKANI?

Baadhi yao wanadai kwamba, haiwezekani Diva akadai kumpenda Mondi kirahisirahisi ili hali alishamkashfu mno katika siku za nyuma.“Huyu jamaa (Mondi) sijui kwa nini baadhi ya watu huwa mnamchukia kwa sababu ni mtu mkarimu sana na ana moyo wa utu mno.

 

“Hakika nchi hii bila unafiki unaweza kujikuta hunenepi.“Safi sana Diva kwa sasa ni shabiki mwenzetu wa Wasafi.“Siamini kama kweli Diva anamsifia Simba (Mondi) kwa sababu alikuwa anamponda sana.“Mlioko karibu na Diva mwambieni asimtafute Zari ubaya, kwa sasa atuache sisi Team Zari tuna jambo letu,” ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya ishu hiyo.

 

TUJIKUMBUSHE

Takriban miaka mitano iliyopita, Diva alianza kumrushia Mondi hasa akiwa hewani kwenye Radio Clouds FM kwa madai kwamba walikuwa na bifu la chinichini.

 

Vita hiyo ya maneno ya wawili hao ambao waliwahi kuimba wimobo wa pamoja wa Piga Simu, ilianza baada wawili hao kukutana kwenye Kipindi cha XXL cha Clouds FM ambapo aliyekuwa mtangazaji wa kipindi hicho, Hamis Mandi ‘B Dozen’ (kwa sasa yupo EFM) aliwauliza kama wamemaliza tofauti zao.

 

Katika majibu yake, Mondi alisema kwamba, Diva alikuwa akimsema vibaya bila sababu yoyote na hapo ndipo Diva alipodakia na kuanza kurusha maneno makali hadi walipozimiwa vipaza sauti.

 

Katika kipindi hicho, Mondi alisikika akijiuliza ni kwa nini ‘hakumkaza’ kwani ndiyo heshima ingekuwepo.Kwa upande wake, Diva alisikika akijibu kuwa, Mondi siyo ‘taipu’ yake.Hata hivyo, ilishindikana kuwatuliza wakiwa studio ndipo wakatolewa nje na baada ya hapo Diva alihamia mitandaoni na kudai kumshtaki Mondi kwa kile alichodai kwamba, jamaa huyo alimtishia kumuua.

 

Miaka kadhaa baadaye, Mondi aliibuka na kusema kwamba, chanzo cha chuki ya Diva dhidi yake ilitokana na kumnyima nafasi ya utangazaji kwenye vituo vyake vya redio na televisheni vya Wasafi Media.“Diva kila siku anasumbua, ananipigia simu, anaomba kazi Wasafi TV.

 

“Anawapigia watu wengi tu wa karibu yangu akiwemo Lilian Mwasha (mtangazaji wa Wasafi Media) na wengine.“Anasema anataka kuleta kipindi chake cha usiku Wasafi TV. Mimi nimekataa, siwezi kumpokea, labda kama menejimenti watakubali, lakini mimi sitaki.

 

“Mimi nimesema sitaki aje Wasafi TV, kwa hiyo ndiyo maana hapa katikati ameongeza chuki nyingi, lakini mimi sina imani naye na sitaki kuiua Wasafi. Kwa hiyo siwezi kumpokea, kama nilivyosema sitaki, akaona afanye bifu kuwa bifu, ila mimi ninamsamehe tu bure,” anasema Mondi.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE