Maelfu wahudhuria sherehe za uapisho wa Rais Museveni

Zaidi ya watu 4,000 wakiwemo viongozi kutoka kila pembe ya bara Afrika wamehudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda iliyofanyika mjini kampala.

Bwana Museveni alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika Januari ambapo mpinzani wake mkubwa ambaye pia ni mwanamuziki maarufu, Bobi Wine, ameendelea kudai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura.

Kiongozi huyo, 76, amekula kiapo hii leo kama rais kwa muhula wake wa 7 kutawala nchi hiyo.

Miaka mingine mitano ya uongozi itamuwezesha kuongoza Uganda kwa miaka 40 na kuwa mmoja kati ya vongozi waliotawala kwa muda mrefu zaidi Afrika.

Wafuasi wa chama tawala (NRM) walijitokeza katikati ya eneo la Ikulu iliyopo Nakasero na uwanja wa Kololo ambako sherehe hiyo ilikuwa inafanyika kushangilia msafara wa rais.

Katika kipindi cha miongo mitatu chini ya utawala wake, Uganda imepiga hatua kijamii na kiuchumi.

Lakini kiongozi huyo amekuwa akikosolewa kwa kushikilia madaraka kwa kipindi kirefu na kukandamiza wapinzani wake.

Nchi hiyo imeshuhudia matukio ya upinzani kukandamizwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku mamia ya wafuasi wa vyama vinavyompinga wakizuiliwa huku wengine wakiwa hawajulikani walipo.

Mamlaka ilipeleka wanajeshi wengi waliokuwa wamejihami katika mji wa Kampala kabla ya sherehe hiyo.

Baadhi pia walipelekwa kuzunguka nyumba za wapinzani wakuu.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE