Maiti Yazikwa, Yafukuliwa na Kurudishwa Mochwari Kimyakimya

Linaweza kuwa tukio la ajabu, lakini ndio limetokea huku usiri mkubwa ukitawala. Ndugu wa familia ya marehemu Danielson Lema (72), aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Nkwansira wilayani Hai, Kilimanjaro, wamepewa maiti ya mtu mwingine, Shanshandumi Kimaro (82) na kwenda kuzika bila kubaini kuwa sio ndugu yao.

 

Mwili wa Kimaro, aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Isuki ulizikwa na familia ya Lema Mei Mosi, mwaka huu baada ya kukabidhiwa kimakosa na wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Hai.


Hata hivyo, Mei 2 mwili huo ulifukuliwa kisha kurudishwa kwenye chumba cha maiti kimya kimya bila uongozi wa hospitali hiyo kubaini.

 

Tukio hilo ambalo lilifanyika kwa usiri mkubwa, limeibua maswali mengi tata kuhusu usalama na umakini wa wahudumu wa chumba cha maiti pamoja na ndugu husika kushindwa kutofautisha miili ya wapendwa wao licha ya kuwepo kwa taratibu za ndugu kutambua mwili kabla ya kukabidhiwa.

 

Hata hivyo, mpaka juzi uongozi wa hospitali hiyo pamoja na ofisi ya mganga mkuu wa wilaya walikuwa hawafahamu lolote kuhusu taarifa hiyo mpaka.

 

Kutokana na tukio hilo, Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk Irene Haule aliomba apewe muda kufuatilia tukio hilo kwa kuwa ndio amelisikia kwa mara ya kwanza na kuahidi kulitolea ufafanuzi.

 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kamwa kilichopo kijiji cha Isuki, Judika Tarimo alisema Mei mosi mwaka huu, ndugu wa Kimaro walikwenda hospitalini hapo kuchukua mwili wa ndugu yao kwa ajili ya maziko, lakini walipofika hawakuukuta mwili wa ndugu yao na badala yake walikuta mwili wa mtu mwingine.

 

Alisema Kimaro alifariki Aprili 28 mwaka huu, siku moja na Lema na miili yao kuhifadhiwa chumba cha maiti katika hospitali hiyo. “Huyu Kimaro alifariki siku moja na Lema, sasa cha kushangaza wakati familia ya Lema wanakwenda kuchukua mwili wa ndugu yao, wakasahau na wakamchukua huyu bwana na kwenda kumzika.

 

“Ndugu wa Kimaro walipokwenda hospitali kwa ajili ya kuandaa mwili wa ndugu yao kwa ajili ya mazishi, hawakuukuta bali walikuta mwili wa mtu mwingine.

 

Walichokifanya kwa sababu maiti hizo mbili zilipelekwa siku moja wakafuatilia yule aliyechukuliwa wa kwanza kwenda kuzikwa kijiji cha Nkwansira ndipo walipobaini walichanganyiwa miili,” alisema Tarimo.

 

Tarimo alisema baada ya taratibu zote kufanyika kwa sababu mwili ule ulifukuliwa Jumapili ya Mei 2, ulirudishwa chumba cha maiti.

 

Alisema ndugu walijipanga tena kufanya taratibu za mazishi ambayo yalifanyika Mei 4. Piason Lema, kaka wa marehemu na mwenyekiti wa ukoo wa familia hiyo, alisema wakati ndugu walipokwenda kuchukua mwili wa ndugu yao walipewa mwili na kuhakikishiwa ni wa ndugu yao, hivyo walikuwa na imani na mhudumu wa chumba cha maiti.

 

“Mei mosi, ndugu walikwenda hospitali wakapewa mwili, lakini huenda tulishindwa kutofautisha maana miili iliyokuwepo chumba cha kuhifadhia maiti tulivyowaangalia wale bwana walikuwa ni wafupi, wazee na walikuwa wanafanana,” alisema.

 

Alieleza ndugu hawakuwa na shaka kwani waliamini ndugu yao alibadilika kutokana na kukaa kwenye jokofu muda mrefu.

 

Alieleza baadaye walipata taarifa kwamba waliyemzika si ndugu yao na taarifa hizi walizipata kutoka kwa ndugu yao mwingine aishiye Nkoma.

 

“Tulizika Jumamosi, tulipopata taarifa kuwa tumemzika mtu ambaye si yeye ikabidi mwili ule ufukuliwe siku iliyofuata na ukari[1]dishwa chumba cha maiti. Tulichukua mwili wa ndugu yetu tukamzika siku ile ile baada ya kufukua yule mwingine,” alisema Lema.

 

CREDIT: Mwananchi


 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE