Mbongo Afunga Ndoa Tatu na Mtoto wa TB Joshua
Kumbukumbu zinasema hii ndio ndoa ya kwanza ya aina yake kufungwa katika jiji la Arusha, ambayo ni ndoa ya mseto baina ya kijana wa kitanzania, Brian Moshi na Mtoto wa Nabii, TB Joshua wa Nigeria , Serah Joshua.

 

Maharusi hawa walifunga ndoa hii jana Jumamosi Mei 8, 2021 katika Kanisa Katoliki la Moyo Safi Mama Bikiria Maria lililopo eneo la Unga Ltd jijini Arusha na kufuatiwa na sherehe kubwa iliyofanyika katika moja ya kumbi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

 

Ndoa hii imekuwa ya tatu kufungwa na maharusi hawa, kwani awali walifunga ndoa ya kwanza nchini Nigeria katika Kanisa la Pentekoste na baadaye ndoa nyingine Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) na sasa wamefunga ndoa nyingine jijini Arusha katika Kanisa Katoliki.Padri Festus Mangwangi ndiye ambaye amefungisha ndoa hiyo, anasema sio ndoa ya ajabu ni ndoa mseto ambayo baada ya kufungwa kila mmoja anabaki na dini yake, lakini watoto watakuwa waumini wa Kanisa Katoliki.

 

Anasema kabla ya ndoa hiyo kufungwa, maharusi walisaini makubaliano hayo na baadaye kupata baraka za Kanisa Katoliki.

 

Anasema awali zilifungwa ndoa mbili katika nchi mbili tofauti, ndoa ya kiserikali na ndoa ya taratibu za Kanisa la Pentekoste ambayo bibi harusi amekuwa akiabudu.

Hata hivyo, Padri Mangwangi anasema bwana harusi, Brayan ni mkatoliki, aliona ni muhimu kufuata taratibu za kikatoliki na ndipo alikuja nchini na kuomba kufungwa ndoa tena baada ya pande zote kukubaliana.“Hii ndoa inatambulika na Kanisa Katoliki kuwa ni ndoa mseto kila mmoja anabaki na dini yake lakini watoto ndio watakuwa wakatoliki,” anasema.

 

Mamia ya wakazi wa Arusha jana walijitokeza katika harusi hiyo kuanzia kanisani hadi ukumbi wa mikutano wa AICC katika tafrija kubwa ambayo ilifanyika.

 

Katika harusi hiyo, ambayo bwanaharusi ni mfanyabiashara kwenye sekta ya utalii na bibi harusi ni mwanasheria, mke wa TB Joshua pamoja na ndugu zake kutoka Nigeria walihudhuria sambamba na familia ya bwana harusi.


 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE