.

5/27/2021

Mbowe: Chadema Hatutashiriki Uchaguzi 2025

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema chama hicho hakitashiriki Uchaguzi Mkuu ujao kama mchakato wa Katiba Mpya utaendelea kuwekwa kapuni.

 

Mbowe alitoa msimamo huo jana jijini, akisisitiza kwamba wanakusudia kupita nchi nzima kuidai katiba hiyo kwa kuwa ni haki ya wananchi. Alikuwa akizindua mfumo wa kielekroniki wa chama hicho wa kuwatambua wanachama wake.

 

“Tunaposema tunahitaji Katiba Mpya, tutawafundisha wanachama na viongozi wetu, watambue umuhimu na uzito wake, kwa sababu udhaifu wa katiba yetu ya sasa umesababisha kuwa na kiongozi aliyekuwa madarakani kuharibu nchi, kuumiza na kuwatesa wananchi kwa kuwa katiba hii inampa mamlaka makubwa ya kifalme.

 

“Rais akisema mfunge mtu huyu, sitaki kuona mikutano ya hadhara au kuona kiongozi wa upinzani, anashinda uchaguzi na haki za wananchi wote milioni 60 zinapotea shauri ya kiongozi mmoja mwenye madaraka na mamlaka makubwa kutokana na udhaifu wa katiba hii ya sasa,” alifafanua.

 

Mbowe alisema tayari ameshazungumza na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la Katiba Mpya, kwamba siyo mapenzi ya mtu mmoja, bali ni mapenzi ya taifa.

 

“Nimemwambia Mama Samia (Rais), mambo ya katiba siyo mambo ya mapenzi yake, ni mapenzi ya taifa la Tanzania na Katiba Mpya tutaitafuta na kuipigania kwa jasho na damu ili kupata katiba ya nchi yetu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025,” alisema.

 

Katika hatua nyingine, Mbowe, alimpongeza Rais Samia kwa kile ambacho alikiita kurudisha tabasamu na matumaini kwa wananchi akidai walipoteza imani na viongozi kutokana na baadhi ya mambo maovu.

 

“Mama (Rais) amerejesha matumaini na tabasamu kwenye sura za Watanzania na CHADEMA, kwa hilo tunamuunga mkono na nilimwandikia ujumbe wa kutaka kuonana naye kwa ajili ya mazungumzo.

 

“Alinijibu kwamba tutakutana na kuzungumza, hivyo basi tunasubiri nafasi hiyo ya mazungumzo kwa kuwa kuna mambo mengi mabaya yamefanyika kwenye nchi hii,” alisema.

 

Mbowe alidai kuwa moja ya mambo watakayoyawasilisha kwa Mkuu wa Nchi ni kitendo cha wafuasi wa chama hicho zaidi ya 250 kufungwa gerezani huku akidai baadhi yao wameshtakiwa kwa makosa ya kubambikwa ukiwamo unyang’anyi, uhujumu uchumi, mauaji na ubakaji.

 

Pia alitangaza mkakati wa CHADEMA kuanza kujenga ofisi za chama hicho kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na kanda ili kuongeza imani kwa wanachama wake, kuwaziba midomo baadhi ya makada kutoka vyama vingine vya siasa kuwa chama hicho hakina ofisi.

 

“Ofisi hizi zitajengwa kwa nguvu za wanachama ili kuonyesha nguvu ya umma inaweza kufanya chochote bila kutengemea ruzuku ya Sh. milioni 380 kwa wabunge na madiwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020, walizokuwa wanapokea kwa mwezi.

 

Alisema kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, walipaswa kupokea ruzuku ya Sh. milioni 140 kwa mwezi, lakini waliikataa kutokana na kutoutambua uchaguzi huo.

 

“Atakayeomba kurudi na kuomba msamaha tumpokee na kumsamehe kwa kuwa chama chetu hakihukumu bali tunataka kujenga taifa lenye haki na mshikamano pasipo kuwabagua watu kutokana na itikadi za vyama, sura, rangi, kabila au dini,” alisema.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger