Mwinyi "Hii ndiyo Sababu ya Kuwapa Mazao Wazungu Wakatupatia Baiskeli"RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amekumbusha uhaba wa fedha za kigeni ulivyoikumba Tanzania mwanzoni mwa uongozi wake kiasi cha kufikia hatua ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa na nchi za Ulaya na Asia ili kukwepa kutumia fedha za kigeni.

Katika kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu', Mwinyi anasema hali hiyo mbaya kiuchumi ikisababishwa na masharti magumu yaliyotolewa na Benki ya Dunia, IMF na wakopeshaji wengine dhidi ya Tanzania na hasa uamuzi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuifukuza timu ya IMF.

Anayataja baadhi ya masharti yaliyowekwa kuwa ni IMF kutaka thamani ya Shilingi ya Tanzania ipunguzwe kwa asilimia 25, kupandisha riba za benki, kupunguza matumizi ya serikali, kusitisha nyongeza ya mishahara, kuondosha udhibiti wa bei na kulegeza udhibiti wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Anasema kutokana na mvutano huo, uzalishaji uliohitaji kuagiza malighafi, vipuri na mafuta kutoka nje ukaathirika, huku TAZARA ikisimamisha huduma Aprili 1982.

"Wauzaji kutoka nje wakadai walipwe kabla ya bidhaa hazijasafirishwa kuja Tanzania. Meli za mafuta zikakataa kupakua mafuta bandarini mpaka walipwe kwanza, na wakati mwingine zilikaa bandarini Dar es Salaam kwa wiki kadhaa wakisubiri malipo. Ninavyokumbuka, kuna waliokubali walipwe kahawa wakaiuze wenyewe mbele ya safari.


"Tatizo la mafuta lilitusumbua sana. Ikabidi Machi 1980 serikali iongeze bei ya mafuta kwenye bajeti ya mwaka 1980/81. Wenye magari wakaruhusiwa kununua petroli kwa siku tatu tu za juma.

"Ofisi za kibalozi na maofisa wa balozi wakatakiwa kununua petroli kwa fedha za kigeni. Serikali ikajitahidi kuzungumza na nchi zinazotuuzia mafuta na zinazozalisha mafuta wanachama wa OPEC kutafuta msaada au unafuu.

"OPEC ikatusaidia kidogo, na baadhi ya nchi wazalishaji mafuta zikajitolea kutusaidia kidogo. Algeria, ambayo ilituunga mkono kwenye vita dhidi ya Idd Amin, wakatukopesha Dola milioni 30 kwa riba ya asilimia tatu tu.


"Iraq ikatupa mkopo wa masharti nafuu wa Dola milioni nane ikiwa ni nyongeza kwa mkopo mwingine wa Dola milioni 30 waliokuwa wametupatia mwaka 1979," anasimulia.

"Mwinyi anabainisha kuwa mbinu nyingine iliyotumika kipindi hicho cha uhaba mkubwa wa fedha za kigeni ni kufanya biashara ya kubadilishana bidhaa ili kukwepa kutumia fedha za kigeni.

Anasema kuwa mwaka 1981 Angola ilikubali kuiuzia Tanzania mafuta kwa mkopo wa masharti nafuu na unaolipwa kwa bidhaa badala ya fedha za kigeni.

"Mwaka 1982 tukaingia mkataba na Msumbiji wa kufanya biashara ya kubadilishana bidhaa badala kulipana fedha. Sisi tuliwapa mabati, kakao na majembe na wao wakatupa matairi na tyubu zake, pamoja na vyerehani.


"Mwaka 1993 tukaafikiana na China na Ujerumani Mashariki juu ya biashara ya kubadilishana bidhaa. Makubaliano yakawa Tanzania iwape Wachina saruji, korosho na mbao na wao watupatie malighafi na vipuri.

"Kwa Ujerumani Mashariki makubaliano yakawa kwamba sisi tuwape kahawa, pamba, chai na tumbaku na wao watupatie baiskeli 10,000. Kwa hakika, tulijaribu kila mbinu ya kuishi kwenye mazingira ya uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.

"Ili kukabiliana na kushuka kwa uzalishaji na tija kwenye sekta ya umma, kwenye sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi mwaka 1980, CCM ilitangaza sera mpya ya tija na kusema kuwa sasa wafanyakazi watalipwa kulingana na matokeo.

"Kwa maana hiyo iwapo kiwanda cha umma kitapata hasara, menejimenti na wafanyakazi hawatakuwa na haki ya kulipwa nyongeza ya mshahara au kupandishwa vyeo, lakini bonasi zitalipwa pale ambapo kiwanda kimeongeza uzalishaji, tija na faida," anakumbusha.


Ili kutekeleza maagizo hayo ya CCM, Mwinyi anasema serikali ilitoa Waraka wa Serikali Na. 1 wa Mwaka 1981 na kisha ikatunga Sheria ya Baraza la Tija la Taifa.

Anabainisha kuwa pia iliazimiwa wanasayansi au wafanyakazi watakaobuni mbinu za kukuza uchumi watazawadiwa, wakati wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao watachukuliwa hatua.

"Wakati huo huo kufuatia kilio cha wafanyakazi, Mwalimu akatangaza kuwa itatolewa nyongeza ya mshahara ya asilimia 20 kwenye kima cha chini cha mshahara na kufikia Sh. 480 kwa mwezi mijini na Sh. 340 kwa mwezi vijijini," anasimulia.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE