.

5/30/2021

Tanzania na Kenya zakubaliana kuondoa vikwazo 30 vya biashara
Mawaziri wanaohusika na masuala ya biashara wa nchi za Tanzania na Kenya wameanza utekelezaji wa maelekezo ya Maraisi wa nchi hizo kuondoa vikwazo vya biashara kataika mpaka wa Namanga.


Katika utekelezaji wa maelekezo hayo watendaji hao akiwemo Waziri wa Viwanda wa Tanzania Prof.Kitila Mkumbo na Waziri wa Vianda wa Kenya, Betty Maina wamekutana jijini Arusha na kusaini makubaliano ya kuondoa vikwazo 30 vya kibiashara huku wakiahidi kukamilisha utatuzi wa vikwazo vingine 34 vilivyobaki ndani ya miezi mitatu.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amewahamasisha wafanyabiashara wa Kitanzania kuendelea kufanya biashara na kwenda kuwekeza nchini Kenya kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na amewataka kuwasiliana na Wizara iwapo kutakuwa na changamoto zozote.

Hayo ameyasema katika Mkutano wa tano (5) baina ya Tanzania na Kenya kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo vikwazo vya biashara visivyokuwa vya kiushuru (NTBs) baina ya nchi hizo uliofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 29 Mei 2021 katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.Prof. Mkumbo amesema Mkutano huo wa kibiashara baina ya nchi hizo ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya biashara katika sekta za kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji. Jumla ya masuala 64 yamejadiliwa ambapo kati ya hayo masuala 30 yametatuliwa na mengine 34 yaliyobaki yamewekewa mkakati maalum na muda wa utekelezaji.

Miongoni mwa masuala yaliyotatuliwa kwa upande wa Tanzania ni pamoja na kuwezesha upitishaji wa bidhaa mpakani, hususan vinywaji baridi kama vile juisi kutoka Tanzania kwenda Kenya, kuondolewa kwa tozo za ukaguzi (inspection fees) zilizokuwa zinatozwa na Mamlaka za Kenya kwenye bidhaa za Tanzania, ikiwemo unga wa ngano, zenye alama ya ubora kutoka Mamlaka husika Tanzania, kuwezesha upitishaji wa mahindi kutoka Tanzania kwenda Kenya na Kuondoa ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za kioo kutoka Tanzania kwenda Kenya. Amefafanua Prof. Mkumbo.

Kwa upande wa Kenya, masuala yaliyotatuliwa ni pamoja na kutoa upendeleo kwa bidhaa za sementi zinazozalishwa nchini Kenya ambazo zinakidhi matakwa ya vigezo vya uasili wa bidhaa vya na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutoa upendeleo maalum kwa vinywaji kutoka Kenya ikiwemo juisi za nanasi (Pineapple Juices) baada ya kukidhi vigezo vya uasili wa bidhaa vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger