Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Maswali magumi 5 moto wa Kariakoo 
MASWALI magumu yameibuka juu ya namna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilivyokabili tukio la moto kwenye soko la kihistoria la Kariakoo, jijini Dar es Salaam na chanzo halisi.

Soko la Kariakoo lililoungua moto juzi usiku na kuteketeza maduka yaliyokuwa ndani yake, likiwa limegubikwa na moshi hadi jana. PICHA: MIRAJI MSALA
Maswali hayo ni pamoja na umbali wa yalipo Makao Makuu ya Zimamoto (Fire) Upanga, Dar es Salaam na Soko la Kariakoo, ambao ni kilomita moja.

Jingine ni muda uliotumiwa katika kudhibiti moto huo ambao ulizuka kuanzia saa 2:40 juzi usiku na udhibiti ulikwenda hadi saa 9 usiku.

Jingine ni uwapo wa miundombinu ya maji ya kuzima moto kwa eneo la Kariakoo, kwa kuwa magari yalipoishiwa maji yalikosa pa kuongezea maji na kulazimika kuyafuata mbali.

Jingine ni muda tukio lilipotokea ni ambao hakuna foleni wala watu wengi hivyo ni rahisi kwa magari ya Zimamoto kufika kwa wakati na kuudhibiti, lakini hayakufanikiwa kufanya hivyo.


 
Jingine ni uwezo wa Zimamoto kukabili matukio kwa haraka kabla ya kusababisha madhara makubwa, na kama wana vifaa vya kuhimili matukio hasa kwa maeneo kama Kariakoo yenye maghorofa mengi yaliyobanana.

“Ikiwa Zimamoto wako umbali usiozidi kilomita moja hadi soko lilipo wameshindwa kufika mapema na kudhibiti moto huu, ikiwa hakuna miundombinu ya maji katika eneo muhimu kama hili ambalo ni kitovu cha uchumi wa nchi, hii ni hatari sana inazua maswali magumu,” alisema Joseph Kavishe.

Aidha, alionyesha kushangazwa na kukosekana kwa miundombinu na vifaa vya kuzimia moto katika eneo lililotumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 224, huku kukiwa na ofisi yenye wafanyakazi wa umma.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jana alitembelea soko hilo na kutoa siku saba za uchunguzi wa tukio hilo na kukabidhi ripoti kwa hatua zaidi.

SAMIA AWAPA POLE

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na soko hilo kuungua moto, na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza kwa kina kujua chanzo.

“Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi, lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, hivyo tukio hilo si hasara kwa wafanyabiashara tu bali hata kwa serikali,” alisema Rais Samia katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

TUKIO HALISI

Nipashe ilifika jana kwenye soko hilo na kukuta maduka pembezoni mwa soko yakiwa yamefungwa na kuwapo idadi ndogo ya wauzaji na wanunuzi tofauti na siku zote huku vikosi vya ulinzi na usalama vikiimarisha ulinzi.


 
Mbali na vikosi vya uokoaji na zimamoto vya umma na binafsi kuiambia Nipashe kwamba udhibiti wa moto ili kupunguza madhara ulikuwa ni wa asilimia 90, gazeti hili lilishuhudia moshi mweusi ukiendelea kusambaa eneo la soko, ulio na harufu kali.

Makamu Mwenyekiti wa Machinga Taifa na Wajasiriamali Wadogo, Stephen Lusinde, alisema takribani wafanyabiashara 1,662 wameathiriwa na tukio hilo na kwamba soko hilo ni kati ya masoko yenye historia tangu mwaka 1968.

Alisema takwimu za Shirika la Masoko Kariakoo zinaonyesha wafanyabiashara waliopo ndani ya soko hilo na wanaolipia kodi ya pango ni 224, kati yao waliopo eneo la chini kabla ya kupanda ghorofa ni 120, ghorofa ya kwanza ni 100 na wengine wanne ambao wapo katika matangazo.

“Tukio hili ni kubwa kwa sababu limepiga eneo la kitovu cha soko hili Tanzania, nawapa pole wafanyabiashara wenzetu ambao ni wa aina tatu, wadogo, kati na wakubwa. Yaani wote katika makundi haya wanauziana bidhaa kutoka muuzaji mkubwa hadi mdogo,” alisema Lusinde.


“Natoa wito kwa wafanyabiashara wenzangu tuvumilie na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alifika hapa na kutuambia tuvumilie ndani ya siku saba ili kujua sababu na chanzo,” aliongeza Lusinde.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Amina Greyson, alisema amefanya biashara soko hilo tangu mwaka 1997, na kwamba hukopa benki ili kukuza biashara yake hivyo hasara aliyoipata anawaza ni namna gani ataifidia.

ZIMAMOTO

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, aliiambia Nipashe kwamba baada ya tukio hilo kutokea majira ya saa 2: 40 na kupata taarifa kwenye kituo cha jeshi hilo Ilala, kwa kushirikiana na vikosi vingine walianza kuzima moto.

Alisema hadi saa 8:30 usiku wa manane walifanikiwa kuuzima moto akisema tatizo kubwa walilokumbana nalo ni uhaba wa maji eneo la Kariakoo na kukwamisha kwa kiasi ya utendaji kazi.

“Hakuna mtu aliyejeruhiwa kwa sababu tukio lilitokea usiku pengine lingetokea mchana ingekuwa taharuki na watu kujeruhiwa. Kanuni zetu baada ya kuzima moto ni uchunguzi, uchunguzi utakapokamilika taarifa itatolewa. Shughuli za biashara zitaendelea kusitishwa itategemeana na ukaguzi na kujiridhisha kwamba lini shughuli zitaendelea,” alisema Kamanda Masunga.


 
Sadiki Mwambambale, mmoja wa waokoaji kutoka kampuni binafsi ya Zimamoto na Ukoaji ya PMM, alisema walifika saa 5 usiku (juzi) eneo la tukio kutoa ushirikiano kuzima moto huo ambao hadi jana ulidhibitiwa kwa asilimia 80 na kwamba umeathiri zaidi eneo la chini la jengo.

“Huko ndani kilichopona hakuna labda majengo na biashara kuzunguka jengo, ATM ya Exim Benki na Benki ya Stanbic.

Inasemekana chanzo kikawa ni hitilafu ya umeme. Ila wafanyabiashara na uongozi uangalie wasiache biashara zikakaa bila mpangilio, mfano mtu anayeuza dawa za mimea, mifugo utakuta huyo huyo na cherehani.

“Utakuta pembeni tu kuna biashara ya chakula, majembe, matoroli, maplasiki, imeleta tabu kwetu kuudhibiti mapema moto kutokana na kwamba lazima tuchukue tahadhari za kiafya, ndio maana moshi unaotoka harufu umejaa dawa na plastiki.

 HABARI KAMA HIZI DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL KWA KUBONYEZA > HAPA

Post a Comment

0 Comments