Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Watuhumiwa 5,429 Wakamatwa

JESHI la Polisi nchini Tanzania, linawashikilia watu 275 kwa tuhuma za mauaji, yaliyotokea nchi nzima kuanzia Mei hadi Julai 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam.

 

Taarifa hiyo imetolewa Julai 20, 2021 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP, David Misime, akieleza tathmini ya operesheni endelevu ya jeshi hilo katika kusaka wahalifu nchi nzima.

 

“Waliokamatwa kujihusisha na mauaji ni 275, kati yao waliokamatwa kutokana na mauji ya wivu wa kimapenzi ni 21, imani za kishirikina ni 22 na 231 kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa pamoja na kujitafutia kipato kwa njia za kiuhalifu,” amesema Kamanda Misime.

 

Akielezea tathmini ya operesheni hiyo, Kamanda Misime amesema watuhumiwa 5,429, walikamatwa kufuatia zoezi hilo. Amesema, 63 walikamatwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha, 141 wakikamatwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu. Huku 1,265 walikamatwa kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba.

 

Kamanda Misime amesema, waliokamatwa kwa makosa ya kubaka ni 508, wakati 125 wakikamatwa kwa tuhuma za kulawiti. Kufuatia operesheni hiyo, watu 2,300 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

 

“Dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha kilo 540 kilikamatwa, Cocain gramu 104, bhangi kilo 3304.321 zilikamatwa. Mashamba ya bhangi hekari 11.75 ziliharibiwa. Mirungi kilo 2233.394 zilikamatwa,” amesema Kamanda Misime.

 

Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi amesema, watu 398 walikamatwa kwa tuhuma za kutengeneza pombe haramu ya gongo na kuuza, kiasi kilichokamatwa ni lita 13612.175 na mitambo ya kutengeneza pombe hiyo iliyokamatwa ni 94.

 

“Waganga wa ramri chonganishi waliokamatwa ni 15. Aidha katika watuhumiwa wote 5,429 waliokamatwa kulingana na ushahidi ulivyowagusa, wameshafikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Misime.

 

Kamanda Misime amewataka wananchi wajiepushe na vitendo vya uhalifu.

“Jeshi katika kila mkoa na kikosi limejipanga vizuri kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inakuwa shwari. Tunatoa wito na karipio kali kwa wahalifu kuachana na vitendo vya kiuhalifu na pia wale wote wanaoendelea kushawishi wananchi kwenye vitendo vya ukiukwaji wa sheria za nchi,” amesema Kamanda Misime.

 

“Silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni 37, ikiwemo bastola nne, shortgun tatu, magobore 29 na uzigun moja,” amesema Kamanda Misime.


 HABARI KAMA HIZI DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL KWA KUBONYEZA > HAPA

Post a Comment

0 Comments