.

8/21/2021

Alphonce Simbu: Alia na maandalizi duni Olimpiki 2020 
Alphonce Simbu: Alia na maandalizi duni Olimpiki 2020
TANZANIA imerudi mikono mitupu kwenye Michezo ua Olimpiki ya 2020, iliyomalizika hivi karibuni Tokyo, Japan na kuwakilishwa na wanariadha watatu, Alphonce Simbu, Gabriel Geay na mwanadada Failuna Abdi.

Pamoja na idadi ndogo ya wanariadha walioiwakilisha Tanzania, lakini macho na matumaini makubwa yalibaki kwa Simbu na hiyo inatokana na kuwa na rekodi nzuri alizowahi kuziweka kwenye mashindano kadhaa huko nyuma.

Katika makala hii, Simbu anavunja ukimwa na kueleza kinachosababisha Tanzania kushindwa kubeba medali, kuwa ni maandalizi hafifu wanayopata wanariadha wake ukilinganisha na nchi jirani kama Kenya na Uganda.

Simbu anasema Tanzania ni moja ya taifa lenye vipaji vingi vya riadha, lakini vimekosa makocha na kambi zenye ubora wa kuleta medali, ndio sababu wamekuwa wasindikizaji kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Olimpiki.


 
Mshindi huyo wa medali ya shaba aliyoipata mwaka 2017 kwenye mashindano ya Dunia yaliyofanyika Uingereza, anasema siri ya wanariadha wa Kenya kufanya vizuri ni kutokana na maandalizi mazuri wanayoyapata kutoka kwa makocha wa nje, ambao wanauelewa vyema mchezo huo.

“Bado tuna safari ndefu kuwafikia Wakenya, wenzetu kambi zao wanadhaminiwa na makampuni ya nje na makocha wao wa ndani nan je wana uwezo au uelewa mkubwa wa namna ya kumuandaa mchezaji ili alete medali, lakini hapa kwetu hakuna,” Kocha tuliyekwenda naye kwenye Olimpiki ya 2020, ni kocha mzuri anajitaidi kwa kweli, lakini uwezo wake ulikuwa ni kutusaidia sisi kupata viwango vya kushiriki michuano ya Olimpiki na siyo kubeba medali kama ambavyo Watanzania walitarajia,” anasema Simbu.

Mwanariadha huyo anasema hawezi kulitupia lawama Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) sababu anajua namna linavyo pambana katika mambo mengi hadi kufikia hapo walipo, lakini anahisi wanakosa sapoti ya kutosha kutoka Serikalini ili waweze kuuinua zaidi mchezo huo kama ulivyo mchezo wa soka.


Anasema kwa mtazamo wake yeye kama wanariadha wengi wa Tanzania wanavyofikiri, wangepatiwa kambi ya kudumu na kuwepo kwa makocha wenye viwango vya kimataifa, basi suala la medali lingekuwa ni la kawaida kama ilivyo Kenya na nchi zingine zilizopiga hatua katika mchezo huo.

KUPOTEA VIPAJI

Simbu anasema vipaji vingi vya wakimbiaji vinapotelea mitaani kwa kukosa muendelezo mzuri kutoka mashuleni na kwenye taasisi za watu binafsi, kama ilivyo kwa Filbert Bayi, ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa kuinua vipaji vya wanariadha wadogo nchini.

Bayi amekuwa akiwasaka wachezaji kutoka katika Mashindano ya Umishumta na Umisseta na wale wanaofanya vizuri, amekuwa akiwachukua na kuwasomesha bure katika shule zake za Kibaha na Kimara.

“Unajua watu wanalalamika kwamba tumeenda Olimpiki hatujarudi na medali, ni kweli lakini, watu wajue kwamba Tanzania ina vipaji vingi vya riadha, lakini vinakosa kuendelezwa ili baadae vilete medali.” “Ili mwanariadha akuletee medali anahitaji kambi ya muda mrefu, yenye mazoezi ya kutosha kutoka kwa makocha wataalamu na hapa nchini kwetu kuna vipaji vingi, lakini haviendelezwi, “anasema Simbu.


 
USHAURI KWA RT

Kutokana na ndoto alizokuwa nazo mbeleni kwenye mchezo huo, Simbu anaishauri RT kuhakikisha inapambana kuwekeza kwa makocha wenye viwango vya kimataifa, kama ilivyo kwa wenzao Wakenya ili kuwapa furaha wa Tanzania kwa kubeba medali kwenye mashindano makubwa kama Olimpiki, Afrika na ile ya Jumuiya ya Madola.

Simbu anasema kama uwezekano mkubwa utafaywa katika riadha, basi mchezo huo utaizidi michezo mingine yote, kwani huko nyuma riadha ndio ulikuwa mchezo wenye kufanya vizuri kuliko mingine. Hilo halina ubishi.

“Najua viongozi wa RT walio wengi wanapambana sana kuhakikisha mchezo wa riadha unafanya vizuri, lakini Serikali inatakiwa kuungana nao ili kusaidia pale ambako wameshindwa, viongozi wenyewe hawawezi sababu kuna mambo mengi ambayo yanahitaji gharama kubwa, hivyo lazima waunganishe nguvu, “anasema Simbu.

MIPANGO YAKE

Simbu anasema baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki na kurudi mikono mitupu, yeye na wenzake wanarudi Arusha kwenda kujichimbia na kufanya mazoezi kwa bidii kujian daa na mashindano yanayokuja huko mbeleni.


Anasema kiu yake kubwa ni kuona anawafurahisha zaidi Watanzania na kuweka rekodi kama ilivyo kwa wakongwe, Filbert Bayi na Seleman Nyambui, ambao wamewahi kuliletea taifa la Tanzania medali za Olimpiki.

“Baada ya kurudi kutoka Japani nimerudi nyumbani Arusha malengo yangu ni kufanya mazoezi kwa bidii ili kuhakikisha nafanya vizuri kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola na yale ya Dunia, ambayo yatafanyika mwakani,” anasema Simbu.

AHADI KWA WATANZANIA

Simbu mwenye umri wa miaka 29, anasema ahadi yake kubwa kwa Watanzania ni kuhakikisha analeta medali ya dhahabu kabla hajastaafu mchezo huo, na ameahidi kuitoa medali hiyo kwa wananchi wa Tanzania.

Anasema kwa maandalizi anayoendelea kuyafanya anaamini ndoto hiyo siku moja itatimia hata kama itachelewa sababu kushiriki Olimpiki mara mbili na mashindano mengine ya dunia, kumemsaidia kupata uzoefu, lakini pia ameona namna wenzao wanavyojiandaa.

“Ndoto yangu siku zijazo ni kupata medali tena ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki kabla sijaacha kukimbia, hili sina shaka nalo, sababu nataka kuweka alama kama walivyofanya watangulizi wangu, Mzee Nyambui na Bayi, ambao huwa nawatumia kama mfano,” anasema Simbu.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger