.

8/28/2021

Ni zamu ya Tanzania Kombe la Dunia 2022TAIFA Stars imeingia tena kwenye mtihani mzito wa kutafuta tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia la 2022 kule nchini Qatar.

Baada ya kupita katika hatua ya awali ambayo ilikuwa ya mtoano, sasa Stars imetinga hatua ya makundi na imepangwa Kundi J dhidi ya miamba Congo DR, Madagascar na Benin.

Taifa Star itaanza kurusha karata yake ya kwanza Septemba 2, ikiwa Kinshasa dhidi ya wenyeji Congo DR na baada ya hapo Septemba 07 itakuwa nyumbani kucheza na Madagascar kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Kocha wa Stars, Kim Poulsen ameita jeshi la wachezaji 28 ambao wameingia kambini tangu mwanzo mwa wiki hii kujiandaa na mechi hizo, ambazo mwenyewe amekiri kwamba ni ngumu, lakini ameahidi kupambana kuhakikisha Tanzania inafuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza.


 
Poulsen anasema mchezo dhidi ya Congo DR ndio ambao ameupa uzito mkubwa kwa sasa kutokana na ubora waliokuwa nao, ambao unatokana na asilimia kubwa ya wachezaji wao kucheza soka Ulaya.

“Uteuzi wangu wa wachezaji kwa ajili ya mechi hizi mbili nimeangalia na uzito waliokuwa nao wapinzani wetu Congo na Madagascar hizi ni timu mbili ngumu zinaundwa na wachezaji wengi wanaocheza Ulaya, hivyo inahitaji kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa ili kutoa upinzani,” anasema Poulsen.

Kocha huyo anasema pamoja na ubora waliokuwa nao wapinzani wao, lakini anaamini mchezo wao dhidi ya Congo DR hautokuwa mwepesi kwao na wenyeji wao kutokana na utayari waliokuwa nao wachezaji wake licha ya muda mchache wa maandalizi.


Anasema kila mchezaji aliyemuita kwenye timu ameonesha kufanya mazoezi kwa kujituma na kufuata maelekezo, ambayo wanawapa yeye na wasaidizi wake jambo ambalo linampa faraja na kuamini wanaweza kufanya maajabu ambayo hayatarajiwi na wengi.

“Wachezaji wote niliowaita wamenionesha kwamba wamepania kufanya vizuri wamekuwa wakijituma mazoezini na kutimiza ipasavyo kila zoezi ambalo wanapewa hilo nijambo zuri kuelekea kwenye mchezo mgumu naamini kuna kitu tunakwenda kukionesha watu wasubiri,” anasema.

Kocha huyo raia wa Denmark anasema hata Congo nao wanaihofia Tanzania kutokana na uwepo wa Mbwana Samatta, ambaye wanamjua vizuri, hivyo hiyo ni faida kubwa kwao kwani watacheza kwa tahadhari wakimhofia.

ZAMU YA TANZANIA

Tanzania imekuwa ikishiriki kwa mara kadhaa mechi za awali za kufuzu fainali za Kombe la Dunia, lakini imekuwa ikiishia njiani kwa kutolewa mara nyingi na mataifa dhaifu sana. Kwa kuliangalia hilo Poulsen anasema mwaka huu ni zamu ya Tanzania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, kutokana na utayari waliokuwa nao ukilinganisha na miaka ya nyuma.


 
Kocha huyo anasema kwa miaka mitano nyuma mpira wa Tanzania umepiga hatua kubwa kuanzia ushindani uliopo kwenye ligi yake na ubora wa klabu zake katika ushiriki wao kwenye michuano ya kimataifa.

Poulsen anasema mbali na hivyo timu za taifa za Tanzania za umri mbalimbali zimeshiriki mashindano kadhaa ya kimataifa na asilimia kubwa ya wachezaji ndio wale wale ambao amewajumuisha yeye kwenye kikosi chake, hivyo anaamini sasa hivi wapo tayari kucheza Kombe la Dunia.

“Sioni ugeni ambao tunao sababu haya mataifa yote, ambayo tumepangwa nayo siyo mageni kwa wachezaji wa Tanzania, lakini haitokuwa mara yao ya kwanza kucheza nazo kwahiyo kwake hakuna ugumu kama watapata maandalizi bora kama walivyo wapinzani,” “Kitu cha msingi hapa ni kufuzu fainali za Kombe la Dunia na hilo linawezekana kutokana na uzoefu, ambao Tanzania tunao, alafu tukishafuzu huko ndio tutakwenda kutafuta uzoefu mwingine wa kubeba Kombe la Dunia,” anasema Poulsen.

SAPOTI YA TFF

Kocha Poulsen anasema sapoti wanayopata kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nayo ni moja ya sababu, ambayo itawasaidia katika harakati zao za kufuzu fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022.


Anasema amekuwa mzoefu wa muda mrefu katika masuala ya soka uwajibikaji wa vyama vya soka kwa timu za taifa unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu ya taifa hilo ameliona pia kwa uongozi wa sasa chini ya Rais Wallace Karia, ambaye amekuwa karibu katika kuihudumia Taifa Stars.

“Namshukuru Rais wa TFF, Wallace Karia amekuwa akitupa sapoti ya karibu sana siku zote tunapokuwa kwenye maandalizi kama haya amekuwa akifanya kila awezalo kutupatia kambi nzuri na mahitaji yote muhimu, “anasema Poulsen.

Taifa Stars ni miongoni mwa mataifa mengi ya Afrika, ambayo yanatafuta nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, baada ya kushindwa tangu michuano hiyo ilipoanzishwa miongo kadhaa iliyopita.

Tanzania chini ya kocha Marcio Maximo, ilionesha kama ingeweza kufuzu fainali hizo na za Mataifa ya Afrika Afcon, lakini ilijikuta ikigonga mwamba licha ya Mbrazil huyo kujitahidi kwa kiasi kikubwa na kuishia kuipandisha viwango.

Makocha waliofuata nao walijitahidi kwa uwezo wao, lakini tukaishia kufuzu fainali za Afcon chini ya kocha Emmanuel Amunike , baada ya hapo hakuna tumeendelea kupambana huku TFF, ikibadili makocha na kuboresha ligi yetu ili kupandisha ubora wa wachezaji na sasa mwanga umeanza kuonekana.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger