.

8/06/2021

Ukiwa kundi hili usichanje mpaka ushauri wa daktari 
JOPO la wataalamu wa afya wa mashirika ya Kimarekani nchini, limetaja makundi matatu ya watu ambao hawastahili kuchanjwa chanjo ya Uviko-19.

Makundi hayo yametajwa kuwa ni wenye umri wa chini ya miaka 18, anayejisikia kuumwa kama homa siku anayotakiwa kuchanjwa na wenye mzio (allergic), huku wajawazito, wenye ugonjwa wa kifua kikuu na upungufu wa damu wakitakiwa kupata ushauri wa madaktari kwanza.

Wakizungunza na waandishi wa habari jana ofisi za Ubalozi wa Marekani, jijini Dar es Salaam, wataalamu hao akiwamo Daktari wa Huduma za matibabu kwa raia wa Marekani wanaokuja nchini kwa ajili ya kujitolea, Dk. Arkan Ibwe, alisema kwa wenye umri wa chini ya miaka 18 mpaka sasa hakuna utafiti kuthibitisha chanjo kwao.

Alisema kwa wanaoumwa homa siku ya kuamkia kuchanjwa wanapaswa kusubiri wapone ndipo wachanje, huku wenye mzio wanatakiwa kujulikana aina ya mzio walionao ili kuangalia chanjo itakayoendana nao ili wasipate madhara.

Aidha, Daktari wa Elimu na Afya ya Jamii na Huduma za Uzazi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), Dk. Emmanuel Tluway, alisema hakuna kinachozuia wajawazito kupewa chanjo, lakini kutokana na hali zao wanashauriwa kupata ushauri kwa madaktari wao au wataalamu wa afya kabla ya kufanya uamuzi.


 
"Kutokana na mabadiliko ya mwili kwasababu za ujauzito wako katika uwezekano mkubwa wa kuambukizwa Uviko, ni muhimu kuangalia faida na hasara, kama faida ni kubwa basi wachanje kwa ushauri wa wataalamu wa afya, hadi sasa hakuna utafiti unaozuia wasichanje na haijaelezwa kama utafiti wa chanjo uliwahusisha wajawazito, hivyo hatuna majibu ya kisayansi kwa asilimia 100, ila wanashauriwa wachanje," alisema.

Alisema wenye ugonjwa wa kifua kikuu wanapaswa kuwasiliana na madaktari wao kabla ya kufanya uamuzi, kwa kuwa wagonjwa hao huwa katika hatua tofauti.

"Wenye magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, saratani, Ukimwi na Shinikizo la damu wanatakiwa kuchanja, lakini kubwa ni kutoa taarifa sahihi kwa mhudumu wa afya kabla ya kuchanja ili aweze kukushauri vyema," alisema Dk. Ibwe.

Kuhusu kazi ya chanjo mwilini, Dk. Tluway alisema inasisimua mwili kuuwezesha kupambana kwa haraka na Uviko, inaimarisha kinga kwenye chembe hai nyeupe zinazohusika kupambana na kuangamiza, pamoja na kuangamiza vizuri vinapoingia mwilini.

Alisema chanjo nane zilizopitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), zimepitia hatua nne za utafiti na kujiridhisha kuwa ni salama kwa binadamu yeyote huku kukiwa na madhara au maudhi madogo madogo yanayoweza kutibika kwa haraka.

Dk. Tluway aliyataja kuwa ni hatua ya kwanza ni maabara ambayo hujaribiwa kwa wanyama ili kuangalia usalama wa chanjo, hatua ya pili ni kwa binadamu wanaojitolea kushiriki ambao huwa kati ya 20 hadi 100 na kama itaonyesha madhara haitaendelea hatua nyingine.

Alisema katika hatua ya pili kinachoangaliwa ni kama chanjo ni salama, maudhi au mabadiliko yanayojitokeza, uhusiano wa chanjo na iwapo inasisimua kinga ya mwili.


 
Hatua ya tatu idadi ya wanaofanyiwa majaribio inaongezeka hadi kufikia 1,000 ambao huangalia ni maudhi ya muda mfupi, kinga inakaa kwa kiasi gani baada ya kuchanja na kama chanjo inakinga mwili.

Alisema kama italeta matokeo mazuri wanakwenda hatua ya tatu ambayo ni wanaofanyiwa majaribio kuwa ni kuanzia 1,000 hadi 40,000 ambao wakionyesha matokeo mazuri inapitishwa na kupewa cheti cha ithibati kama chanjo salama.

Alisema hatua ya nne ni kukusanya data za maudhi na madhara ya muda mrefu kwa waliochanjwa na linakuwa endelevu huku watu wakiendelea kupatiwa chanjo na huchukua miaka 10 au zaidi.

Naye, Daktari wa Tiba na Huduma za Sera za Afya wa Shirika la CDC, Dk. Eva Matiko, akizungumzia uwapo wa chanjo tofauti, alisema Uviko ni janga linalohitaji mapambano ya silaha tofauti na wakati mwingine zote zitumike kukabili.

Alisema Tanzania imefanyia utafiti kupitia mamlaka zake, chanjo nane zilizoorodheshwa na WHO na kujiridhisha tano ikiwamo ya Johnson and Johnson zinafaa kutumika nchini na kwamba ni salama kabisa, huku akisisitiza maudhi madogo madogo ni jambo la kawaida.

Awali, akifungua mkutano huo, Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuongoza kampeni ya kupata chanjo Julai 28, mwaka huu na kusema ni uongozi na uamuzi thabiti kwa manufaa ya wananchi wake.

"Chanjo zimekuwa sehemu muhimu za nyenzo za kulinda afya ya jamii kwa zaidi ya miaka 200 sasa. Karibu kila nchi duniani hutoa chanjo za mara kwa mara kwa watu wake ili kuwakinga dhidi ya maradhi mbalimbali," alisema.

Vile vile, alisema nchini Marekani zaidi ya asilimia 99 ya vifo vipya vya Uviko-19 ni vya watu ambao hawajachanja na kwamba ukweli ni kuwa chanjo zinaweza kuokoa maisha.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger