.

9/11/2021

Hatima ya Gwajima, Silaa CCM yaiva
Hatima ya Gwajima, Silaa CCM yaiva
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimepokea taarifa kutoka Kamati ya Maadili ya Wabunge wa chama hicho, kuhusu tuhuma zinazowakabili wabunge watatu waliohojiwa na kamati hiyo hivi karibuni kwa ajili ya kufanya uamuzi.

Wabunge hao ni Josephat Gwajima (Kawe), Jerry Silaa wa Ukonga na Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC0, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema CCM ni chama ambacho kina misingi na uendeshaji wake ni Katiba, Kanuni na taratibu.

“Niwahakikishe kwamba CCM bado ipo imara hasa katika kulinda na kuhakikisha kwamba inaendeleza msingi wake wa kuwapo kwake. Ni kweli kamati ya wabunge imeshakabidhi taarifa kwa chama lazima nikiri na hatua zinazofuata ni taratibu ndani ya chama chetu.

“Hiyo ilikuwa hatua ya awali, hatua ya pili mpaka tunafikia kwenye kufanya maamuzi (uamuzi). Chama kinaheshimu sana misingi ya kuanzishwa kwake kwa kufuata katiba, kanuni na taratibu,” alisema.


 
Alifafanua kuwa katika kanuni za uongozi za CCM, suala hilo likipokewa na chama linaenda Kamati ya Usalama na Maadili.

“Likitoka hapo ndani ya chama chetu linategemea na hoja ambayo ipo na inatakiwa kwenda ngazi gani. Ikitoka  kamati ya maadili kuna Kamati Kuu (CC) kuna yale mashauri ambayo yanakwenda NEC kwa ajili ya uamuzi,” alisema.

Alisema kama lipo jambo la aina hiyo ambalo linahusu kufikishwa kwenye vikao vya uamuzi muda ukifika watasema.

“Tunakiri kupokea taarifa ya wabunge na hatua inayofuata ni mapema kusema lakini tumepokea tunaendelea na utaratibu kwa mujibu wa katiba na kanuni zetu,” alisema.

Awali, akitoa taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyokutana jana chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kimewapitisha wagombea wa CCM katika uchaguzi mdogo utakaofanyika hivi karibuni kwenye jimbo la Ushetu na Konde.

Aliwataja waliopitishwa kuwa ni Emmanuel Cherehani (Ushetu) na Mbarouk Amru Habibu (Konde) na kampeni za CCM zitaanza Septemba 25, mwaka huu, ambapo Katibu Mkuu Daniel Chongolo atazindua kampeni hizo kwa Jimbo la Ushetu.

Aidha, alisema kamati hiyo imempongeza Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kwa kufanya kazi ya kuwaletea Watanzania maendeleo.


 
“Rais Samia ameweza kusimamia bila kutetereka suala ambalo lilikuwa linasumbua kwa takribani miezi miwili suala la tozo, na wamefanya vizuri sana hadi kufikia Septemba mosi zimekusanywa Sh. bilioni 63, ameonyesha kutotetereka pamoja na changamoto zilizoonekana,” alisema
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger