Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu, amemzungumzia mhudumu wa afya anayepita nyumba kwa nyumba kuchanja chanjo ya Uviko-19, akionya kampeni hiyo isitumiwe vibaya katika kuwalazimisha watu kuchanja.
Jana katika mitandao ya jamii, kulisambaa habari na picha ikimuonyesha Ofisa wa Afya wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma akipita nyumba kwa nyumba kuwachanja chanjo ya Uviko 19 watu zaidi ya 160 kwa siku moja.
Akizungumzia leo Septemba 27, 2021 katika mkutano mkuu maalum wa uchaguzi viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ngazi ya Taifa unaofanyika mkoani Dodoma hilo, Rais Samia amesema asingependa kuona suala hilo likifanyika kwa mabavu kwa kuwalazimisha watu kuchanja.
Amesema kati ya mambo ambayo angependa ALAT kulishughulikiwa kwa kasi kubwa ni suala la mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19 ikiwemo utoaji elimu.
“Juzi na jana nilivyoingia nchini nimekuta hii agenda ya watu kupita nyumba kwa nyumba na mikoba ya sindano kuchoma watu.
“Tulisema hili jambo ni la hiari, ukipita nyumba kwa nyumba anayetaka mchome, asiyetaka usichome, lakini kubwa nalotaka kusema mtu hana mamlaka ya kukubali au kukataa kama anayo elimu.
“Kwani kama ana elimu yakutosha hawezi kukataa, lakini hana elimu unapita tu na mkoba wako unamwambia nikuchome nisikuchome, atakuambia usinichome,” amesema Rais.
Amewataka wahudumu wa afya kutoa elimu ya afya kwa wingi ili wananchi waone umuhimu wa kuchanja.
“Asipoona hilo hawezi kuona uchungu wa hili suala, nendeni kafanyeni kampeni kubwa watu wakubali kuchanja msiende kufanya kwa mabavu. Tupunguze vifo vinavyotokana na ugonjwa,” amesema.
Aidha amesema ndani ya nchi yetu kuna matatizo makubwa matatu na hili la uviko limejitokeza ni la nne.
Ametaja magonjwa mengine kuwa ni TB, HIV na malaria na kueleza kuwa yameshughulikiwa kwa kiasi kikubwa na kuagiza janga la Uviko-19 lishughulikiwe na watu wapate kinga.