Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Samia Aikaribisha Marekani, Ulaya Kuwekeza Tanzania
KABLA kuhutubia ulimwengu kwenye mkutano wa 76 wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UNGA), Rais Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wafanyabiashara wa Marekani pamoja na Jumuiya ya Ulaya kuja kuwekeza Tanzania.

 

Rais ametoa wito huo alipozungumza na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Charles Michel kisha kukutana na jumuiya za wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani.

 

Kwenye mazungumzo yao, Rais Michel ameomba maoni ya Rais Samia katika mambo manne ya kipaumbele kwa umoja huo wa Ulaya na uhusiano wake na Afrika huku akibainisha utayari wa kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo hayo.

 

Umoja wa Ulaya umeomba maoni kuhusu mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya corona (Uviko-19), mabadiliko ya tabianchi, usalama nchini Msumbiji na mapinduzi ya kidijitali.

 

Kuhusu mapinduzi ya kidijitali, Rais Samia amelijadili suala hilo na Michel miezi kadhaa baada ya kuielekeza benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza kujiandaa kwa matumizi ya sarafu mtandao (cryptocurrency) inayotokana na teknolojia ya blockchain.

 

Rais aliitaka BoT kujitayarisha kwa matumizi ya sarafu mtandaoni akisema wakati umefika hivyo ni muhimu kuanza maandalizi kuruhusu mabadiliko hayo alipozungumza na vijana jijini Mwanza, Juni 13.

 

Akiwa na Rais Michel, Samia alibainisha hatua zilizochukuliwa na Tanzania kukabiliana na Uviko-19 ulioathiri sekta nyingi ikiwamo ya utalii pamoja na mkakati wa kusambaza miundombinu ya afya.

 

“Bado tuna changamoto katika upatikanaji wa vifaatiba na rasilimali watu. Nauukaribisha Umoja wa Ulaya kuangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo,” alisema Rais Samia.

 

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Rais amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika hivyo inalipa kipaumbele suala la kukabiliana na janga hilo.

 

Vilevile, Rais amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Marekani kuja kuwekeza nchini huku akiwasisitiza kuimarisha biashara kati ya na Tanzania.

 

“Kwa sasa biashara zinazofanyika kati ya Tanzania na Marekani ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo. Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinatoa soko la zaidi ya watu milioni 450 hivyo kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema Rais Samia.

 

Ingawa Marekani ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini lakini takwimu zilizopo hazimridhishi Rais hivyo kuwataka Wamarekani hao kushirikiana na wenzao hapa nyumbani kuongeza tija.

 

Mwaka 2019, taarifa zinaonyesha Tanzania iliagiza bidhaa za dola 241 milioni za Marekani na kuuza za dola 46 milioni huku Taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani likiwekeza miradi ya dola 5.55 bilioni iliyoajiri watu 44,118 na Tanzania ikiwa nayo ya dola milioni moja tu.

 

Uwekezaji huo, Rais Samia amesema ni kiasi kidogo ukilinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani na fursa zilizopo Tanzania yenye uwezo wa kuimarisha kilimo na kulisha eneo kubwa la Afrika na dunia kwa ujumla, miundombinu ya afya kuhudumia majirani zake hata bandari ya kuingiza na kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda popote duniani.

 

Aidha, Rais amewaeleza wafan yabiashara hao kuwa Tanzania imesaini mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) unaolegeza masharti ya kulifikia soko la zaidi ya watu bilioni 1.3.

 

Katika mkutano wa UNGA unaoendelea jijini New York, Rais Samia amehudhuria maadhimisho ya miaka 20 ya Tamko la Durban la kupinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa aina yoyote.

 

Wakati huohuo, Rais Samia amekutana na Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass na kuzungumza masuala kadhaa yanayohusu ushiriki wa taasisi kubwa ya fedha duniani kwenye maendeleo ya Tanzania.

 

Kama ilivyo kwa rais Michel, Malpass amezungumzia vita dhidi ya Uviko-19 na umuhimu wa kutoa chanjo kwa wananchi na akabainisha utayari wao kusaidia hilo kwa kutoa mkopo nafuu.

 

“Naipongeza Serikali kwa juhudi inazochukua kuboresha mazingira ya biashara kupitia sekta binafsi. Upatikanaji na usambazaji wa umeme, nyumba nafuu na miundombinu ya kidijitali muhimu sana kukabilia ushindani uliopo,” alisema rais Malpass.

 

Kiongozi huyo alisisitiza umuhimu wa uwazi kwenye mikopo na madeni huku akishauri haja ya kujagua miradi ya kipaumbele na kuainisha vyanzo vyake vya mapato.

 Downlaod App ya BLOG Hii Kutoka Google Play Kwa Kubonyeza HAPA>>>

Post a Comment

0 Comments