.

9/10/2021

Samia Ataja Faida Nne Makala Aliyorekodi "Huko Duniani Wengine Wanaamini Mlima Kilimanjaro Upo Nchi ya Jirani"

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anatarajia kwamba makala aliyoshiriki kuiandaa itasaidia kuitangaza vizuri Tanzania na kuondoa upotoshaji wa makusudi kuhusu nchi yetu.

Tangu Agosti 28 mwaka huu Rais Samia alikwenda kwenye maeneo mbalimbali Zanzibar na Tanzania Bara kurekodi makala ya televisheni inayotarajiwa kuzinduliwa nchini Marekani.

Wakati akiendelea na kazi hiyo, Rais Samia alisema aliacha urais pembeni ili kufanya kazi ya kuongoza watalii kuwaonesha vivutio.

“Nimeshiriki kuandaa makala ya Tanzania itakayorushwa katika kipindi maarufu Duniani cha Royal Tour. Ni matarajio yangu kuwa makala hii itasaidia kuitangaza vizuri nchi yetu, kuinua utalii, kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji na kuondoa upotoshaji wa makusudi kuhusu Tanzania,” aliandika jana kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.


Rais Samia alianza kurekodi makala hiyo Unguja, akaenda Pemba, Bagamoyo, Kilimanjaro, mgodi wa tanzanite, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Hifadhi ya taifa ya Serengeti na akamalizia kazi hiyo juzi kwenye tamasha la utamaduni Kisesa wilayani Magu katika Mkoa wa Mwanza.

Wakati akizungumza na wananchi wa Sanya Juu mkoani Kilimanjaro akiwa njiani kwenda Marangu alisema walikuwa wanatengenezwa filamu kuonesha mazuri yaliyopo Tanzania.

“Asubuhi tumeanza Kilimanjaro kwenye mlima wetu, huko duniani wengine wanaamini mlima wetu upo nchi jirani. Tumekwenda


kuupiga picha kuwaonyesha kwamba upo hapa Tanzania,” alisema Rais Samia na kuongeza; “Lakini tumekwenda Mererani pia kuonyesha ulimwengu kwamba tanzanite ni ya Tanzania. Na tumekwenda kwenye machimbo, tumechukua picha inavyochimbwa, inavyopimwa, inavyoongezwa thamani mpaka tunapata vito. Sasa wale wanaouza hovyo hovyo huko wajue kwamba ile kitu kwao ni wapi, Tanzania. Na ulimwengu utaamini hivyo kwa sababu tunawaonyesha.”

Wakati akizungumza na wananchi wa Karatu alipokuwa njiani kwenda Ngorongoro, Rais Samia alisema alikuwa anafanya kazi maalumu ya kurekodi filamu ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii baada kwisha kwa ugonjwa wa Covid-19.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger