Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa
SERIKALI imewataka viongozi wa dini kujiepusha na migogoro na kutoa matamko, ambayo yatasababisha uvunjifu wa amani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, jijini hapa kwenye ibada ya kumweka Wakfu Askofu Mkuu Msaidizi wa Kanisa la Pentekoste Renew Assembly (PRA).
Alisema viongozi hao wanapaswa kutumia nyumba zao za ibada kuzungumza habari za upendo na amani, kuepuka kutoa matamko yanayoleta mgawanyiko kwenye jamii na waumini wao.
“Sisi wananchi tunawaamini sana ninyi viongozi wa dini, lakini ikitokea migogoro kati yenu inatuchanganya, kwa sababu tunaamini mnayajua vizuri maandiko matakatifu ya Mungu na jinsi ya kuvumiliana na kuishi kwa upendo,” alisema.
Waziri Simbachawene alizitaja baadhi ya sababu za migogoro mingi iliyopo katika taasisi za kidini kuwa inayosababishwa na kugombea madaraka au fedha.
Alibainisha kuwa sababu hizo na zingine zimekuwa zikisababisha kuwagawa waumini wao na kusababisha uvunjifu wa amani .
Aidha aliwakemea baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitumia vibaya nyumba hizo za ibada kutoa matamko, ambayo yanaleta mgawanyiko katika jamii.
Alisisitiza kuheshimu sheria, kwa sababu kila dhehebu la dini limesajiliwa kwa madhumuni ya kutoa huduma zilizokusudiwa na sio kusababisha migogoro.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Wilson Mwaoga, alisema ibada hiyo ilikuwa maalumu, kwa ajili ya kumweka Wakfu Askofu Mkuu Msaidizi wa Kanisa hilo, Emmanuel Mogope.
Askofu Mwaoga alisema katika ibada hiyo waliwaalika watu wachache, kutokana na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO- 19.
Alisema kanisa hilo lina matawi mengi nchini na nje ya nchi ambao walitamani kufika, uwapo wa ugonjwa huo uliwazuia kufika.
Aidha aliiomba serikali kusaidia migogoro inapojitokeza, ili kuepuka kusababisha uvunjifu wa amani
Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA