Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Uhaba wa Maji Walikumba Jiji la Dar, Unaambiwa ni Mwendo wa madumu tuNI mwendo wa madumu! Ndicho kinachoonekana kwenye baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kutokana na uhaba wa maji uliotokana na kuwapo kwa mgawo wa huduma hiyo ya msingi.

Jana Nipashe ilishuhudia katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo wa kibiashara wananchi wakiwa na madumu, wakitafuta maji kwenye maeneo yanakouzwa.

Mathalani, maeneo ya Kimara maji yalikuwa yakiuzwa kwa Sh. 200 kwa dumu la lita 20, Tabata yaliuzwa kati ya Sh. 200 na 500 kwa dumu, Mbezi yaliuzwa kati ya 300 na 400 kwa dumu, Makumbusho Sh. 500 kwa dumu, Gongo la Mboto yaliuzwa kati ya Sh. 300 na 500 kwa dumu, Buguruni Sh. 500 kwa dumu na Kinondoni yaliuzwa kati ya 300 na 500 kwa dumu.

Wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amekiri kuwapo kwa mgawo wa maji mkoani humo, akisema serikali inapanga kutumia chanzo cha maji ya Mto Rufiji kukabili mgawo wa maji ulipo hivi sasa katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Aweso alibainisha hayo jana jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya maji katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.


Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza wizara hiyo kuhakikisha inalifanyia kazi tatizo la upatikanaji wa maji salama katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Tatizo la mgawo wa maji katika Jiji la Dar es Saalam litaondolewa kwa kutekeleza mradi huu wa kutoa maji katika Bonde la Mto Rufiji na kuyapeleka Dar es Saalam ili kuviongezea nguvu vyanzo vingine vinavyotumika hivi sasa," alisema Aweso.

Alisema kukamilika kwa mradi huo wa Rufiji kutasaidia kuondoa kero ya mgawo wa maji katika Mkoa wa Dar es Saalam moja kwa moja, huku akibainisha hatua zingine wanazozitumia kukabiliana na uhaba wa maji mkoani humo ni kusitisha utoaji wa vibali vya umwagiliaji katika kipindi hiki ambacho kuna ukame.


UPOTEVU WA MAJI

Waziri huyo alisema moja ya kero ambayo bado inazikabili mamlaka za maji na usafi wa mazingira ni pamoja na upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa.

Alisema kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika ni asilimia 20 tu na siyo vinginevyo, hivyo kama kuna eneo yanapotea zaidi ya kiwango hicho basi kinatokana na wizi.

“Kama kuna eneo kuna upotevu wa maji zaidi ya asilimia 20, basi hiyo inatokana na baadhi ya watu kutokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakiunganishia watu maji kinyume na utaratibu katika maeneo kama hoteli na viwanda," alisema Aweso.

Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, wastani wa wakazi wa mijini wanaopata huduma ya majisafi na salama imeongezeka kutoka asilimia 25 ya wakazi wote wanaoishi mijini mwaka 1961 hadi kufikia wastani wa asilimia 86 mwaka 2021.


Waziri huyo alisema kikwazo kikubwa katika sekta ya maji ni uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, hivyo kuna haja kulinda na kutunza miundombinu ili iendelee kutoa huduma endelevu kwa wananchi mijini na vijijini.

*Imeandikwa na Paul Mabeja (DODOMA) na Maulid Mmbaga (DAR)

 HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWA APP YA UDAKU SPECIAL, DOWNLOAD HAPA KUZISOMA HATA KAMA HUNA BUNDLE

 Udaku Special Blog

Post a Comment

0 Comments