Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Watoto Waomba Adhabu Ya Viboko Kufutwa
WATOTO wameliomba bunge kuweka mkazo kwenye mambo kadhaa ikiwamo kuongeza bajeti ya elimu, kufanya mapitio ya sheria ya ndoa na kufuta adhabu ya viboko.


Watoto walitoa maombi hayo wakati wa kuwasilisha ajenda za watoto na vijana balehe kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ikiwa ni mkakati wa kuendeleza ajenda za watoto na vijana chini ya mashirika ya Femina Hip na UNICEF. Pia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 75 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF).Najma Mohamed akiwasilisha ajenda ya nguzo ya elimu, aliliomba bunge kuweka msukumo kwa serikali kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuongeza bajeti ya elimu ili kusaidia ajira za walimu kwa malengo ya kukidhi mahitaji ya kupata elimu bora kwa watoto, kuwa na maabara, maktaba zenye vitabu vya kiada na ziada na maabara ya Tehama.Naye Godlisten Boniphase aliomba wabunge kuhakikisha wanasimamia ufutwaji wa adhabu ya viboko shuleni kutokana na walimu kutotekeleza ipasavyo sheria ya sasa na kupendekeza kuwepo adhabu mbadala kama kutoa kazi nyingi za masomo ambazo ni ziada."Sheria ya sasa inaelekeza viboko visivyozidi sita, kama kuna haja ya adhabu Mwalimu Mkuu anatakiwa kusimamia utolewaji wa adhabu, sheria hii haifuatwi na walimu matokeo yake wanaadhibu wanafunzi na kujenga hofu kwa mtoto badala ya kuwafanya wajutie kosa," alisema.Kwa upande wa Derrick Mwakyeja alishauri bunge kufanya mapitio ya Sheria ya Ndoa kwa kubainisha umri wa mtoto wa kike kuolewa na kuhakikisha serikali inaboresha huduma za afya ya uzazi wa watoto na vijana balehe.Naye Najma Paul aliwaomba wabunge kuishauri serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na programu ya kutambua na kuibua vipaji ili vijana waweze kujiajiri na kuajiri ajira zenye staha.Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuzungumza na kuwasikiliza watoto ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili na kusisitiza kuwa wazazi wana wajibu wa kuwafuatilia watoto wao katika mienendo yao ili kuwajenga kimaadili na kuwawezesha kujieleza pale wanapopata changamoto.Pia amewahakikishia watoto hao kuwa hoja zao zimepokelewa na kuwa bunge litasimamia maboresho ya sheria zinazosimamia watoto pale itakapobidi kwa kushirikisha makundi yote muhimu ikiwemo watoto wakati wa kufanya mapitio ya sheria.Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk John Jingu amewataka wazazi na walezi kuwajibika katika malezi na makuzi ya mtoto ili kuwasaidia watoto kuepukana na vitendo vya ukatili ambao ni tatizo kubwa kwa sasa.Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM) amepongeza mchango wa UNICEF katika kupambana na mimba za utotoni katika Mkoa wa Mtwara ambalo lilikuwa tatizo kubwa.Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema) amewahakikishia watoto hao kuendelea na kazi ya kushawishi serikali ili kuhakikisha sheria ya ndoa inafanyiwa mapitio.

 HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWA APP YA UDAKU SPECIAL, DOWNLOAD HAPA KUZISOMA HATA KAMA HUNA BUNDLE

 Udaku Special Blog

Post a Comment

0 Comments