Ticker

6/recent/ticker-posts

Kimei Atia Neno Kauli ya Ndugai "Tanzania si ya kwanza"MBUNGE wa Vunjo, Dk. Charles Kimei, amesema Tanzania si nchi ya kwanza na wala haitakuwa ya mwisho kutekeleza miradi kwa kukopa.

Katika hafla ya kupokea vyumba vya madarasa 85 vilivyojengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 1.7, mbunge huyo alisema juzi kuwa serikali ina nia ya dhati katika kuwaletea wananchi wake maendeleo hususani kwa wale wa ngazi ya chini, lakini wapo baadhi ya watu wenye maneno ya kukatisha tamaa, hivyo wasipewe nafasi.

Alisema Deni la Taifa bado ni himilivu na kuwa si tishio kama ambavyo inasemekana. Alisema nchi nyingi duniani zimekuwa zikikopa ili kujenga miundombinu ambayo itawawezesha wananchi wake kufanya biashara sambamba na kutoa huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa mbunge huyo ambaye ni mtaalamu wa uchumi, bado Tanzania ina sifa za kukopesheka na ndio maana imeendelea kuaminiwa na wahisani mbalimbali ikiwamo Mfuko wa Fedha Duniani na Benki ya Dunia (WB).

"Sisi bado tupo katika hali nzuri ya kukopesheka na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan alivyoenda kukopa, aliaminiwa mara moja tofauti labda na mataifa mengine, sisi bado tunayo rekodi nzuri katika mkopo na suala la mkopo si aibu, hatujaanza sisi kukopa wala hatutakuwa wa mwisho," alisema.


Alisema yeye kama mtaalamu wa fedha, alishawahi kuzunguka katika taasisi nyingi na kujifunza vigezo vya kupewa mkopo na kuwa ni lazima uwe na rekodi nzuri ya matumizi ya mkopo lakini pia kipaumbele cha mkopo wenyewe kitambulike au kuonekana.

Alisema fedha hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwa muda mfupi, hivyo wananchi waunge jitihada za miradi hiyo pamoja na inayoanzishwa na serikali hususan katika ile miradi ambayo inamgusa moja kwa moja mwananchi wa chini.

"Serikali imekuwa ikianzisha miradi ambayo imekuwa ikigusa wananchi wa hali ya chini ikiwamo maji, barabara na afya hivyo wananchi hawana budi kuunga mkono na kuachana na propaganda zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wasio iwazia mema nchi dhidi ya miradi hiyo" alisema Dk. Kimei.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda, alisema ifikapo mwezi Januari mwakani, yaani kuanzia kesho, mzazi ambaye hatampeleka mtoto shule atakumbana na mkono wa sheria.

Alisema hatua zitajumuisha kufungwa jela kwa kuwa hakuna sababu ya kutompeleka mtoto shuleni kwa sababu serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa madarasa na shule mpya.

"Itakapofika muda wa kufungua shule mtoto ambaye hatapelekwa shule, mzazi wake ajiandae moja kwa moja kukumbana na mkono wa sheria kwani hakuna kizuizi kinachompelekea mtoto kukosa elimu tena na kuwa serikali imekuwa ikipambana katika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu," alionya.

Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments