Ticker

6/recent/ticker-posts


 

Ni vita ya Kisisa ya ‘Kiroboto’ na ‘Wahuni’

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE
Dar es Salaam. Mitandaoni kuna majibizano kati ya wanasiasa wawili wenye sifa zinazokaribiana kutokana na vyeo walivyopata kushika.

Hawa ni Nape Nnauye, mbunge wa Mtama na Humphrey Polepole, mbunge wa kuteuliwa.

Wote ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ni wabunge na kilicho na mvuto zaidi, walipishana kwenye ofisi ya Ukatibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi.

Desemba 13, 2016, Polepole aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kabla ya uteuzi huo, Polepole alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo. Desemba 15, 2016, Nape alimkabidhi Polepole ofisi hiyo aliyokuwa akiishikilia awali.

Hoja iliyoelezwa kuhusu Nape kuondolewa kwenye sekretarieti ya CCM ni kwamba tayari alishakuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa wakati huo, vilevile mbunge wa kuchaguliwa jimbo la Mtama

Hivyo, alipunguziwa kazi za chama ili awajibike vizuri serikalini na katika uwakilishi wa wananchi.

Kinachowafanya Nape na Polepole wazidi kufanana ni kuwa wote walipanda ngazi na kuingia ofisi ya itikadi na uenezi wakitokea kuwa wakuu wa wilaya. Mwaka 2011, Nape aliteuliwa kuwa Katibu wa Uenezi CCM akitokea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.


Vijembe na mafumbo

Kutoka Desemba 15, 2016, wakati wa makabidhiano ya ofisi hiyo ya CCM, usingetaraji kabla ya kutimia kwa miaka mitano, Polepole na Nape, wangegeuka wataalamu wa kurushiana mafumbo, huku wote wakiwa kando ya kiti cha Katibu Mwenezi CCM, kinachoshikiliwa na Shaka Hamdu Shaka.

Mvutano wa hivi karibuni zaidi na kinachofahamika ni kauli ya Polepole kuhusu kuwapo kwa aliowaita kwa jina la ‘wahuni’ , watu wanaojali masilahi yao binafsi kuliko yale ya Taifa.

Baadaye Nape akaibuka, akimtaka Polepole ataje majina ya wahuni aliowamaanisha.

Hata hivyo, Polepole hakutaja majina ya aliowaita na mjadala wa neno hilo uliposhika kasi, Polepole akafafanua:

“Neno wahuni sijaanza nalo leo, wahuni wanaopenda maslahi binafsi kwanza wapo. Mhuni ni mhuni tu hawabadiliki, nitoe rai kwa viongozi wawe macho na wahuni, awamu jana alitukana Serikali leo anakaa upande wa Serikali.

“Na hili la wahuni nililizungumza sana ni wale wanaokwepa kodi utawapata ukienda TRA, wabadhirifu wa mali za umma wapo nenda Takukuru utawakuta, kazi yetu kama viongozi wa Taifa ni kuwadhibiti.

“Sasa naongea mtu mwingine anaibuka. Hivi mimi niite wahuni halafu mtu na akili zake timamu anasimama na kujijumuisha au kufurahia? Niseme wazi watu wakizingua mahala natoka tena nazungumza. Nitatumia kila fursa kuhakikisha na mimi natumia nafasi yangu kushughulika na wahuni,” alisema Polepole.

Akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni hivi karibuni, Polepole alisema: “Mimi sina ugomvi na Nape. Yeye ndiye alinipokea na kunikabidhi ofisi CCM. Niliposema wahuni sikutaja jina la mtu.”


Tafsiri ya maneno ya Polepole

Kwa tafsiri ya baadhi ya watu, maneno ya Polepole kuhusu kuwepo wa wahuni, ni kipimo cha jinsi ambavyo asivyokubaliana na mwenendo wa Serikali, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hivi karibuni, Nape aliandika fumbo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, akisema:

“Aaaah kiroboto, ulishindwa akiwepo godfather, utaweza leo? Kina wenyewe sheikh. Lakini ni kawaida punda roho ikiwa inaacha mwili hurusha mateke. Nonsense!”

Nape hajawa tayari kutaja maana ya ‘tweet’ yake wala mtu aliyemwita kiroboto, ingawa wengi wameipa tafsiri kuwa ni mwendelezo wa mvutano uliopo sasa.

Tafsiri ya kisasi

Maneno ya Polepole kuhusu uwepo wa wahuni, yaliibuka muda mfupi baada ya Nape kutoa hoja bungeni akitaka madeni yote ya Serikali yaliyokopwa wakati wa uongozi wa awamu ya tano, yachunguzwe.

Akijibu hoja hiyo ya Nape, Polepole alihoji mahali ilipotoka na kwa nini imetolewa, akataka ufafanuzi uwazi wa mikopo inayochukuliwa sasa. Kwa kifupi, kwa tafsiri za wachambuzi, hoja za Polepole zinajikita zaidi kwenye kuhakikisha uongozi wa awamu ya tano hauchafuliwi.

Hata programu anayoiita “Shule ya Uongozi”, ambayo Polepole ameianzisha kupitia intaneti, wachambuzi wengi wamekuwa wakitafsiri kama jukwaa la kutema nyongo dhidi ya yanayoendelea kwenye siasa nchini.

Polepole kwa sasa anawekwa kwenye fungu la watengwa kwenye chama, sawa na Nape alivyokuwa wakati wa uongozi wa awamu ya tano. Kwa vyovyote iwavyo, hii ni vita ya hadhi ya kisiasa ndani ya CCM kati ya wanasiasa hawa.

 Join AJIRA YAKO Group for Daily Job Updates CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments