Ticker

6/recent/ticker-posts

Kilio cha Katiba Chapata Sauti Mpya

 


Moshi. Kilio cha kutaka Katiba mpya kimepata sauti mpya baada ya Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Stephen Munga kujitosa akitaka suala hilo liendelee kujadiliwa kwa kuwa halistahili kuzua mkorogano.


Askofu Munga, aliyestaafu mwaka juzi ametoa kauli hiyo katika ukurasa wake wa Facebook, ikiwa ni sehemu ya salamu zake za kuuaga mwaka 2021.


Kauli ya Askofu Munga imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la watu na taasisi mbalimbali kuhusu kurejewa kwa mchakato wa Katiba mpya ulioanza nchini wakati wa awamu ya nne mwaka 2011 na kusitishwa 2014.


Pia imekuja kukiwa na kampeni iliyotangazwa Desemba 22, ambapo Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) unakusanya saini milioni tano za wananchi wanaotaka kurejewa kwa mchakato huo ili kuziwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan.


Kauli hiyo pia imekuja kukiwa na mvutano kwa baadhi ya wadau, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa wa ama kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya au kuanza na Tume huru ya uchaguzi.


Wakati viongozi wa vyama vya Chadema na NCCR Mageuzi wakitaka kurejewa kwa mchakato wa Katiba, wale wa ACT Wazalendo wanataka ipatikane Tume huru ya uchaguzi kwanza.


Kwa upande mwingine, baadhi ya wanaharakati mitandaoni wanaunda Baraza la Katiba mpya (Katiba Mpya Initiative Council) likiwa na lengo la kutoa mwelekeo wa maoni ya Watanzania wanaotaka mchakato huo urejewe.


Wakati hayo yote yakijadiliwa, msimamo wa Rais Samia umebaki uleule alioutoa Juni alipozungumza na wahariri kuwa aachwe asimamishe nchi kwanza kiuchumi, hayo ya Katiba yatafuata baadaye.
Salamu za Askofu Munga


Katika salamu zake hizo, Askofu Munga alisema Watanzania wanamaliza mwaka 2021 na kuelekea mwaka mpya 2022 kukiwa bado na mambo magumu ya kufanyia maamuzi, likiwemo la kupatikana kwa Katiba mpya.


“Kuhusu suala la Katiba mpya kwa mfano, kwa nini inakuwa vigumu angalau kukubaliana turejee kukamilisha mchakato wa Katiba mpya ulioongozwa na Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba (mwenyekiti Tume ya Mabadiliko ya Katiba?” amehoji Askofu Munga.


Ameongeza kuwa, kama kungekuwa na jamii yenye uwazi na inayotazama sawa mambo ya msingi, jambo la Katiba mpya lisingekuwa na utata na mkorogano.
Ataka Tume ya upatanisho


Mbali na suala la katiba, Munga alizungumzia sakata la kiongozi wa kanisa la Ephata, Nabii Josephat Mwingira aliyetakiwa kuhojiwa na polisi baada ya kudai alinusurika kuuawa mara tatu na watu wa Serikali, Askofu Munga alishauri iundwe uume ya ukweli na upatanisho ili kusikiliza malalamiko kama hayo kwa watu wengine.


“Mtumishi huyu analalamika jinsi alivyoumizwa na vyombo vya Serikali. Huyu naye anamalizia mwaka 2021 kwa kuitwa na Jeshi la Polisi kuhojiwa. Kwa kauli ya Mtume Mwingira twaweza kujiuliza, “Je, ingeundwa Tume ya ukweli na upatanisho na watu kufika huko kuzungumza mambo yao, tungesikia mangapi? Lakini pia si ndio ingekuwa njia ya Taifa kupona?” anahoji Askofu Munga katika salamu zake hizo.


“Bali kwa kuwa tumezoea kutuliza mambo kwa vitisho basi tuendelee hivyo mpaka wakati utakapotubadilisha,” alisisitiza.


Alipoulizwa kuhusu suala la kuanzishwa kwa tume hiyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Mohamed Mchengerwa alisema hawezi kuizungumzia kwa kuwa hajamsikia Askofu Munga.


“Ni mpaka nipate fursa ya kusikiliza hizo kauli, kwa sababu nilikuwa ziara na nilikuwa shamba huko vijijini, kwa hiyo nikipata fursa ya kutulia na kusikiliza nitatoa hoja. Unajua wanasema kama hujafanya utafiti huna haki ya kuongea,” alisema Mchengerwa.


Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene alisema “nadhani hilo jambo bado ni premature (halijakomaa), niache na mimi nisikie kwa waliotoa maoni, kwa sababu sioni kinachozungumzwa. Hapo naona kuna maridhiano, unaridhiana na nani? Lakini kikubwa sijasikia bado,” alisema.
Kifo cha Desmond Tutu


Askofu Munga ametumia kifo cha shujaa na mpigania haki, Askofu Mkuu Desmond Tutu ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani, kuelezea umuhimu wa kupigania haki, akisema suala hilo ni kama mapigo ya moyo wake.


“Wapo watu wanaodhani kwamba wakiwanyamazisha wapigania haki watakuwa wamenyamazisha na haki yenyewe. Napenda kuwakumbusha wanaowatesa na kuwaua watetezi wa haki mambo matatu,” alisema Askofu Munga.


“Kwanza, watambue kuwa haki hainyamazishwi kwa sababu haki hainyamazi. Mtawafunga watetezi wa haki na hata pengine kuwaua lakini ukweli ni kwamba haki haifungwi wala haifi.”


“Pili, kutetea haki ni wito na kipawa kinachowekwa ndani ya watetezi wa haki na kwamba imani ya hao ni kwamba haki ina nguvu kuliko mateso na kifo.


“Tena haki ina nguvu kuliko tonge la ugali la kutia mdomoni na kutumbukiza tumboni. Wapigania haki si wachumia tumbo. Neno linasema, “heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa,” alisema akinukuu Mathayo 5:6.


“Tatu, kuna maumivu ya dhamiri na majuto makubwa katika kukanyaga haki za watu. Kwa upande mwingine kuna furaha na amani kubwa mioyoni mwa watetezi wa haki hata katikati ya adha na mateso yao.


“Nne, haitakuja itokee Mungu auache ulimwengu mikononi mwa waovu na wakanyagaji wa haki. Haki ni uwepo wa Mungu ulimwenguni. Mungu ameweka wachungaji wa haki katika ulimwengu, ambao wametawanyika katika maeneo mbalimbali katika jamii, bila kusahau kuwataja majaji na mahakimu.


“Tano, katika maisha ama unasimama upande wa haki au upande wa kupotosha na kukanyaga haki. Katika mambo ya haki ni lazima kuchagua upande wa kusimama. Hawezi mtu kusema anasimama katikati,” alisema Askofu Munga.


Kesi ya Mbowe


Kuhusu kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu Munga alisema kunahitajika mambo matatu ambayo ni uadilifu wa mahakama, uadilifu wa sheria na uadilifu wa majaji, akisema yakisimamiwa, haki itatendeka bali yakiingiliwa na kuvurugwa haki haiwezi kutendeka.


“Freeman Mbowe na wenzake wako kifungoni. Swali kubwa ni ikiwa jamii yetu ina mtazamo na uelewa sawa juu ya masuala ya haki, kwa nini mambo kama madai ya katiba mpya na kesi ya Mheshimiwa Mbowe vimekuwa tata?


“Hapa tunahitaji yazingatiwe mambo matatu. Uadilifu wa mahakama, uadilifu wa sheria na uadilifu wa majaji. Hayo yakisimamiwa basi haki itatendeka. Bali hayo yakiingiliwa na kuvurugwa, haki haiwezi kutendeka,” alisema Askofu Munga, ambaye kwa siku za karibu aliingia mgogoro kuhusu uchungaji wake.
Adai kukutana na mengi


Katika salamu hizo, Askofu Munga alisema katika maisha yake amefanya mambo mengi na kukutana na mambo mengi, yakiwamo yale ya bonde la uvuli wa mauti, lakini yote aliyasogeza katika maombi na kuhesabu karama zake.


“Natangaza rasmi kuwa bado nipo hai kwa neema ya Mungu. Pia nitangaze kuwa kama ilivyo kawaida ya maisha, baadhi ya waliotafuta nafsi yangu wametangulia.


“Kila mmoja wetu anayo himaya yake ya kuishi aliyopewa na Mungu Muumbaji, kwa hiyo tuheshimiane katika maisha. Kwa sasa Bwana amenipa nguvu mpya na ninaendelea na kazi nikisimamia mambo yaleyale kama yeye aliyenituma,” alisema.

Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments