Roman Abramovich: Safari ya milima na mabonde kutafuta utajiri na heshimaKatika mwaka ambao Abramovich aliingia katika ulimwengu wa kazi, Russia ilikuwa tofauti sana na nchi tunayoijua leo. Mwaka 1983, ilikuwa bado sehemu ya Umoja wa Kisovieti, wakati huo ikiongozwa na Yuri Andropov, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Urusi (KGB).

Biashara binafsi ilikuwa haramu na katika mazingira kama hayo, shahada ya chuo kikuu ilikuwa mojawapo ya ‘hati’ chache za mafanikio. Lakini, wakati Abramovich akiwa na miaka 17 alikuwa na nia ya kwenda chuo kikuu, ushindani ulikuwa mkubwa na rekodi yake isiyojulikana ya kitaaluma isingemsaidia.

Wayahudi, ambao walikuwa ni asilimia mbili ya idadi ya watu wote nchini humo, hawakuaminiwa. Joseph Stalin ambaye alikuwa kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Kisoshalisti ya Urusi tangu mwaka 1922 hadi alipoaga dunia mwaka 1953 aliwaita Wayahudi kama ‘vimelea visivyo na mizizi’ na kuwataka kukaa nyumbani katika nchi ya Kiyahudi ya Urusi iliyoko Mashariki mwa Siberia inayoitwa Birobidzhan.

Wakati Abramovich akitafuta nafasi ya kujiunga na chuo kikuu, Wayahudi bado walionekana watu wasioaminika kiitikadi na uzalendo wao kwa Urusi ulitiliwa shaka.


 
Hata hivyo, alijiunga na Taasisi ya Viwanda ya Ukhta baada ya kuacha shule mwaka 1983. Baadaye alihamishwa kutoka taasisi ya Ukhta kwenda Taasisi ya Mafuta na Gesi ya Gubkin huko Moscow.

Baada ya kukosa nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Gubkin, Abramovich aliamua kurudi Ukhta kuhudhuria kile kilichojulikana kama Taasisi ya Viwanda ya Ukhta. Simulizi inayoungwa mkono na marejeo kadhaa ni kwamba wakati fulani Abramovich aliacha kozi yake akiwa mwaka wa pili wakati maisha yalipombadilikia.

Akiwa na umri wa miaka 18 aliitwa kujiunga na huduma ya kitaifa katika Jeshi la Urusi (wakati huo- Red Army). Mwanzoni mwa mwaka 1985, alitumwa Kirzach kutumika katika kitengo cha upigaji risasi. Huko ndiko alijifunza ujasiri zaidi.


Katika maisha yake ya ndoa, Abramovich ameoa na kutaliki mara tatu. Desemba 1987, baada ya muda mfupi aliokaa katika Jeshi la Soviet, alimuoa Olga Yurevna Lysova na walitalikiana mwaka 1990.

Oktoba 1991, alimuoa msimamizi wa zamani wa shirika la ndege la Urusi Aeroflot, Irina Malandina na kujaliwa watoto watano; Ilya, Arina, Sofia, Arkadiy na Anna. Binti yake mkubwa Anna ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Columbia na anaishi New York City, na binti yake Sofia ni mtaalamu wa kupanda farasi ambaye anaishi London, Uingereza, baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha London.

Jumapili ya Oktoba 15, 2006, gazeti la ‘News of the World’ liliripoti Irina alikuwa ameajiri mawakili wawili maarufu wa talaka wa Uingereza, kufuatia ripoti za uhusiano wa karibu kati ya Abramovich na Daria Zhukova (Dasha), ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 25, binti wa mmoja wa matajiri wakubwa wa Kirusi, Alexander Zhukova.

Hata hivyo, baadaye Abramovich alimtaliki Irina Machi 2007 na kumlipa dola za Marekani milioni 300. Wakati Abramovich anatalikiana na Irina, pamoja na mali nyingi ambazo wanandoa hao walikuwa nazo nchini Russia, walikuwa na kasri huko Bavaria kusini mashariki mwa Ujerumani, kasri lililoko London, shamba katika jiji la Sussex kusini mashariki mwa Uingereza na nyumba ya shamba yenye bustani kubwa kusini mwa Ufaransa, ambayo hapo awali lilikuwa ni la mwana mfalme mtawala wa jimbo Windsor katika familia ya kifalme ya Uingereza.


 
Wakati wa talaka hii, London ilikuwa inachukuliwa na wengi kuwa mji mkuu wa talaka duniani. Kwa kuwa Irina alikuwa amesomea sheria, wakati akiishi Russia na mumewe alimsaidia katika mambo mengi ya kisheria.

Baada ya kutalikiana na Irina, mwaka 2008 Abramovich alioana na Zhukova na baadaye kujaliwa watoto wawili, wa kiume, Aaron Alexander, na binti, Leah Lou.

Lakini Jumatatu ya Agosti 7, 2017 vyombo vya habari viliripoti kuwa Abramovich na Daria wametengana baada ya miaka 10 pamoja.”

Shirika la Habari la Uingereza (BBC) lilikariri taarifa moja kutoka kwa wenza hao wakisema: “Baada ya miaka 10 ya kuishi pamoja, sisi wawili tumefanya uamuzi mgumu kutengana.”


Abramovich, ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 50, ndiye mtu wa 139 tajiri zaidi duniani.

Taarifa hiyo ilisema wawili hao “wataendelea kuwa marafiki, wazazi, na washirika katika biashara walizoanzisha pamoja.

Waliongeza katika taarifa yao kwamba “wataendelea kufanya kazi pamoja kama waanzilishi wenza wa Jumba la Makumbusho la Garage la Sanaa ya Kisasa huko Moscow na kituo cha kitamaduni cha Kisiwa cha New Holland huko Saint Petersburg”.

Ingawa Agosti 2017 walisema wanatengana tu lakini wabaki kama marafiki huku wakitunza watoto wao, lakini mwaka 2018 walitalikiana.

Ijumaa ya Septemba 14, 2018 Abramovich alihamisha umiliki wa jengo na mali nyingine zilizoko Upper East Side nchini Marekani yenye thamani ya dola milioni 92.3 kwa kummilikisha mtalaka wake, Dasha Zhukova.


 
Gazeti ‘New York Post’ liliripoti kuwa hati za mali ambazo zililifikia gazeti hilo zinaonyesha wanandoa hao wanamiliki mali isiyohamishika zaidi ya New York kuliko ilivyoripotiwa awali.

Septemba 14, Jiji la New York lilirekodi uhamishaji wa majumba matatu kutoka kwa Abramovich kwenda kwa Dasha yenye thamani ya dola 74 milioni. Katika rekodi za mali, Abramovich alijiorodheshea mali za Moscow, wakati Dasha akichukua jumba la UES jijini New York ambako anaishi kwa sasa.

Jumba hilo la New York lenye ghorofa tano kwenye mtaa wa East 64th Street anamoishi Dasha, hapo awali lilikuwa likimilikiwa na mfanyabiashara wa kimataifa wa sanaa, Alec Wildenstein na mke wake wa wakati huo, Jocelyn Wildenstein.

Jumba hilo la Wildenstein na mkewe Jocelyn liliingia kwenye mikono ya Abramovich kwa sababu nao baada ya kutalikiana walilazimika kuliuza kwa Abramovich ambaye naye, kwa sababu ya kutalikiana na Dasha, alilazimika kumwachia.

Pamoja na yote hayo, Ijumaa ya Oktoba 11, 2019, Zhukova alifunga ndoa na Stavros Niarchos II, mtoto wa Philip Niarchos, katika sherehe ya kiraia huko Paris, Ufaransa.

Philip Niarchos ni bilionea wa Ugiriki, mtoto mkubwa wa tajiri wa biashara ya meli wa Ugiriki, Stavros Niarchos.

Je, ni mambo gani ambayo Abramovich ameyapitia katika maisha yake ya kusaka utajiri? Fuatilia mfululizo wa makala haya kesho.
______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad