Russia yaikamata Miji Mingi zaidi Ukraine, Bidhaa zapanda

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



Moscow, Russia. Wakati Russia ikisitisha mapigano katika Jiji la Mariupol nchini Ukraine ili kuwaruhusu raia kuondoka salama, vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya siku 10 sasa vimeathiri biashara kwa kupandisha bei ya bidhaa huku vikiyumbisha thamani ya sarafu.

Jana, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza: “Kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa muda wetu, tutasitisha mapigano ili kuwaruhusu wananchi katika miji ya Mariupol na Volnovakha kupata huduma za kibinadamu na kuondoka salama.”

Tangazo hilo lilitolewa muda mfupi baada ya Meya wa Mariupol, Vadim Boychenko kusema: “Jiji lipo katika hali ya hatari kutokana na mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na wanajeshi wa Russia”.

Meya huyo alisema mashambulizi hayo yaliyofanywa kwa siku kadhaa, yamesababisha jiji hilo kukosa umeme, huduma za maji, chakula na kusitishwa kwa usafirishaji, hali iliyowahi kushuhudiwa mara ya mwisho kipindi cha Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (WWII).


“Kwa sasa tunaangalia namna ya kutatua changamoto za kibinadamu ili kuondoa vikwazo hivi vinavyowakabili wananchi waliopo Mariupol,” alisema Boychenko, akiomba kusitishwa kwa mashambulizi kuruhusu dawa na vyakula kuwafikia wananchi.

Maelfu ya raia wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa tangu Russia ilipoivamia Ukraine kuanzia Februari 24, hivyo kuishikilia miji huku ikiharibu kinu cha nyuklia kinachoendeshwa na mataifa ya Ulaya yaliyoiongezea vikwazo vya uchumi na kibiashara Serikali ya Russia.

Ukiacha Jiji la Mariupol lenye bandari muhimu kwa uchumi na biashara nchini Ukraine, majeshi ya Russia yanaishikilia miji mingine miwili ya Berdiansk na Kherson iliyopo katika ufukwe wa Bahari Nyeusi (Black Sea), kusini mwa nchi hiyo.

Kuchukua uongozi wa Jiji la Mariupol lenye takriban wakazi 450,000 na bandari muhimu iliyopo katika bandari ya Azov, yanaelezwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa majeshi ya Russia, kwani sasa yatakuwa yanaruhusu nini kiingie au kutoka kupitia usafiri wa majini Ukraine, kwani bandari hiyo inaiunganisha na Crimea pamoja na Donbas.

Juzi, Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov alisema Russia inasubiri awamu ya tatu ya mazungumzo nchini Belarus.

Kutokana na makubaliano yaliyofanyika, mamlaka ya Jiji la Mariupol liliwatangazia wananchi kwamba wangeruhusiwa kuondoka jana kuanzia saa sita usiku, kwani hakutakuwa na mashambulizi yoyote yatakayofanywa.

“Mnaweza kuondoka kwa magari binafsi. Madereva wote mnaombwa, kadri muwezavyo, kuwabeba raia wakati mnaondoka. Magari yenu yajae ilimradi asiachwe mtu. Siku kadhaa zimetolewa kwa raia wote kuondoka Mariupol,” ilisema taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.


Sarafu zaanguka, zapanda

Ukiacha madhara kwa raia, kuharibika kwa miundombinu na kudorora kwa huduma za kijamii, vita kati ya Russia na Ukraine imeyumbisha biashara kutokana na kukosekana kwa usalama hivyo kuyumbisha thamani ya baadhi ya sarafu kubwa duniani.

Katika kipindi chote cha mapigano, kampuni nyingi zimelazimika kusitisha shughuli zao nchini Ukraine, hata Russia huku mataifa hasa ya Ulaya na Amerika yakiiwekea vikwazo vya kiuchumi Russia, hali inayoongeza wasiwasi itachelewesha kufufua uchumi ulioathiriwa na janga la Uviko-19.

Mchambuzi wa masuala ya biashara na uwekezaji nchini Uingereza, Dan Smith-Cox alisema kampuni nyingi zinaondoka Russia na Ukraine kutafuta sehemu salama zaidi watakakozalisha bidhaa zao.

“Kampuni nyingi zinakimbilia Uturuki. Mapigano haya yataleta ugumu mkubwa wa biashara kuliko yalivyokuwa masharti ya Uviko,” alisema Smith-Cox.

Jumanne iliyopita, kampuni kubwa za meli duniani, ikiwamo MSC, Maersk na CMA CGM zilitangaza kusitisha huduma zao katika bandari ya Russia, ikiwamo kubwa zaidi, Saint Petersburg iliyopo katika Bahari ya Pacific hivyo gharama za usafirishaji kupanda.

Vita hivyo, vimepaisha bei ya mafuta ambayo sasa yanauzwa kwa dola 120 kwa pipa moja katika soko la dunia, huku aluminium ikipanda na kuvunja rekodi yake.

Vita hivyo pia vimesababisha uhaba wa malighafi zisizopitisha joto wala umeme (semikonda) zinazotumika kutengeneza bidhaa za kielektroniki, zikiwamo simu za mkononi. Russia na Ukraine kwa pamoja zinatoa asilimia 23 ya ngano iliyouzwa duniani kote mwaka 2021/22 huku zikizalisha asilimia 60 ya alizeti inayotumika duniani.

Kutokana na vita vinavyoendelea, thamani ya yuan, sarafu ya China imepanda na kuvunja rekodi iliyodumu kwa miaka minne sasa huku soko lake la hisa likiimarika.

Jumatano iliyopita, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na yuan 6.30, bei ambayo kwa mara ya mwisho ilionekana Aprili 2018.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad