Wafanyakazi Fastjet wamuangukia Rais Samia, wadai Bil.5

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA





WAFANYAKAZI 105 wa Shirika la Ndege ya Fastjet Tanzania wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuzuia ndege aina ya Embraer 190 (5H-FJH) ya shirika hilo ili waweze kulipwa stahiki zao. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Wafanyakazi hao wamefikia uamuzi huo baada ya kusotea haki zao takribani Sh.bilioni tano ambazo ni mishahara kuanzia Septemba 2018 hadi Januari 2019 pamoja na michango ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari aliyekuwa Mfanyakazi wa Ndani ya Ndege hiyo, Mummy Katolila amesema baada ya kufukuzwa kazini mwaka 2019 wafanyakazi 105 wakiwakilishwa na mwenzao Alex Mjoge walifungua kesi iliyopewa jina la CMA/DSM/Ilala 914/19 chini ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Amesema wamesotea haki zao kwa takribani miaka mitatu pamoja na kushinda katika kesi zote ambazo walifungua hivyo wanaomba Rais Samia kuingilia kati, ili mamlaka husika zisimamie waweze kulipwa haki zao.


 
“Sisi tumeshinda kesi ambayo tulifungua CMA tunadai Sh.bilioni 5 kwa Fastjet, ila hawataki kutulipa, mbaya zaidi kuna taarifa kuwa ndege hiyo imefutiwa usajili hivyo inaweza kuondoka na wao kukosa haki zao,” amesema.

Katolila amesema wanamuomba Rais Samia kuelekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), kuzuia ndege hiyo ili isiondoke kwenye anga la Tanzania hadi walipwe fedha zao ambazo wamezisotea kwa miaka mingi.

Amesema kesi hiyo iliendeshwa CMA ambapo mwishoni mwa mwaka 2019 hukumu ya zuio hilo ilitoka, ambapo baada ya miezi sita zuio hilo lilifika kikomo, hivyo hawakuendelea na kesi katika mahakama bali waliwasiliana na mfilisi ambaye aliteuliwa na mahakama kuu.


Amesema ndege hiyo hadi sasa imeegeshwa kwenye anga la Precions Air, hivyo kuzitaka mamlaka kuchukua hatua haraka.

“Tunamuomba Rais Samia atusaidie kuzuia ndege hiyo kuondoka hapa nchini kwani ndio dhamana iliyobakia, ndege nyingine imeshaondoka, sisi ni watoto wa Kitanzania hatuna pengine pakukimbilia,” alisema.

Aidha, amesema kutokana na sakata hilo, waliona ni vyema kwenda kuifahamisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA- Mkoa wa Ilala) kuhusiana na madai ya kodi (kwa mishahara ya wafanyakazi iliyokwishalipwa ambapo walichukua hatua na kuitaka TCAA kuzuia ndege husika 5H-FJH kuondoka, hivyo kuwepo kwa taarifa kuwa imefutiwa usajili ni habari ya kuwasikitisha.

“Pamoja na kutolipwa mishahara, pia michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF tangu September 2018 mpaka January 2019 haikupelekwa, jambo ambalo limezidisha ugumu wa maisha,” amesema.


 
Naye Mfanyakazi Ernest Robert amesema kadhia hiyo ya kuondolewa kazi imesababisha aishi katika maisha magumu kwa miaka mitatu sasa, hivyo anamuomba Rais Samia kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.

“Kitendo cha kudaiwa usajili wa ndege hiyo umefutwa kinaacha maswali mengi kwetu naomba Rais aagize vyombo vyake kuchunguza ni nini kilichopo nyuma ya pazia,” amesema.

Akizungumzia sakata hilo Kiongozi wa Kampuni ya Ufilisi, Arnold Shirima, amekiri kupokea maombi ya wafanyakazi hao kuwa wanufaika katika mchakato wa kufilisi shirika hilo, ila hadi sasa bado ufilisi haujafanyika.

Shirima amesema Fastjet inadaiwa na taasisi mbalimbali zaidi Sh.bilioni 46 ambapo TRA inadai zaidi ya Sh. bilioni 16 na kwamba wapo kwenye mchakato wa kuhakisha wadai wote wanalipwa.


“Ni kweli madai hayo ya waliokuwa wafanyakazi wa Fastjet yamefika mezani kwetu tunayafanyia kazi ni imani yangu iwapo mdaiwa akilipa watalipwa, hicho ndicho naweza kusema kwa sasa, niwasihi wawe na subira,” amesema.

Akizungumzia taarifa hiyo kuhusu ndege kubadilishiwa usajili, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga amesema ni kweli ndege hiyo Embraer 190 (5H-FJH), ilibadilishwa namba na wameshachukua hatua kwa mujibu wa sheria wanazosimamia.

Malanga amesema ili kubadilisha namba ya usajili wa ndani mwenye mamlaka ya kubadilisha ni mkurugenzi mkuu wa TCAA, hivyo hadi sasa haijafutiwa usajili kutokana na kuwepo kwa michakato mbalimbali ambayo haijakamilishwa.

“Ndege ile haijafanyiwa usajili mpya, kwa sababu mkurugenzi mkuu hajaikana hii ya 5H, hivyo haiwezi kuondoka nchini. Kilichotokea pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ni wale watu kubandika namba nyingine na hapa tunaanda taarifa na kuwaadhibiti, wamefanya kosa.

Ukienda pale JNIA, utakuta wamebadilisha na kurejesha namba ya usajili wa ndani ambayo ni 5H, tumewaelekeza waendelee kuitumia 5H, unajua wanataka kuitoa kwa sababu wanaona hasara,” amesema.


 
Kaimu mkurugenzi huyo amesema kuwepo kwa ndege hiyo sio kwa sababu ya wafanyakazi bali ni kutokana na tozo mbalimbali ambazo inadaiwa ndege kama ndege na sio kampuni ya Fastjet.

Amesema TCAA, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, KADCO walikuwa wanaidai ndege hiyo na wameshalipwa ila bado TRA ndio inadai hivyo haiwezi kuondoka mpaka walipe.

Malanga amesema pia zipo gharama nyingine ambazo kampuni inadaiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo wafanyakazi na wanaendelea na mchakato wa kuwalipa hatua kwa hatua.

“Unajua ndege ile Fastjet walikodisha, hivyo sio ya kampeni, kuendelea kukaa hapa ni kutokana na madai ya TRA, wakiwalipa TRA wataondoka hayo madai mengine sio ya ndege hiyo ni ya kampuni,” amesema.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad