4/25/2022

HATIMA ya Halima Mdee na wenzake 18 kuendelea kuwa wabunge wa viti maalumu itajulikana tarehe 11 Mei 2022
HATIMA ya Halima Mdee na wenzake 18 kuendelea kuwa wabunge wa viti maalumu itajulikana tarehe 11 Mei 2022, wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) watakapojadili rufaa zao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Halima na wenzake walivuliwa uanachama wa Chadema tarehe 27 Novemba 2020 wakituhimiwa kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni Dodoma, kuapishwa na aliyekuwa Spika, Job Ndugai.

Ni siku 20 zijazo, ndizo zitaamua hatima yao katika Baraza Kuu hilo, chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, lililosogezwa mbele kutoka 25 Aprili 2022 hadi 11Mei, kupisha waumini wa dini ya Kiislamu ambao ni wajumbe wa kikao hicho, kumalizika Mfungo Mtukufu wa Ramadhan.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza na gazeti hili jana, alisema: “Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu, waliomba kusogezwa mbele kwa kikao hicho, ili kupisha Mfungo wa Ramadhan, kwani wengine wanatoka mbali.


 

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
“Kutokana na maombi hayo, viongozi wa juu wa chama walikubali na kusogeza mbele hadi 11 Mei 11 na kikao cha Kamati Kuu kitafanyika 10 Mei  na vikao vyote vitafanyikia Dar es Salaam,” alisema Mrema alipoulizwa kuhusu maandalizi ya kikao hicho kilichoahirishwa mara kadhaa.

Kuhusu kina Mdee, Mrema alisema: “Awali alitumiwa barua ya kujulishwa kuwa kikao ni Aprili 25 na baada ya mabadiliko haya, tumewapelekea barua kwa njia mbalimbali ambazo tunajua zitawafikia au zimewafikia.”

Baada ya kufukuzwa, Halima na wenzake, walikata rufaa katika kikao cha Baraza hilo kupinga uamuzi huo wa Kamati Kuu iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Mbowe.


Tangu walipotimuliwa Chadema na kuwasilisha barua kwa uongozi wa Bunge, Ndugai aliwakingia kifua akidai hatambui uamuzi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kuwataka kutokuwa na wasiwasi na waendelee kuchapa kazi.


Hata hivyo, baada ya Ndugai kujiuzulu 6 Januari 2022 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Dk Tulia Ackson kwa kuchaguliwa, alilizungumzia suala hilo siku chache baada ya kuchukua uongozi wa Bunge.

Dk Tulia alilizungumzia suala hilo 14 Februari 2022 katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari Dodoma, akijibu swali kuhusu uhalali wa kina Halima kuwa bungeni.

“Uharamu haupo, kwa sababu hawezi kuwa haramu halafu akawepo ndani. Nchi yetu inaendeshwa kidemokrasia na kisheria. Jambo moja tu linalosubiriwa, ni watu kumaliza michakato yao inayohusika,” alisema Dk Tulia na kuongeza:


 
“Jambo linalosubiriwa ni kumaliza michakato yao ya ndani ya chama. Katiba yetu inasema mbunge lazima awe mwanachama, kwa hiyo wakimaliza wakaleta taarifa, tutachukua hatua.”

Mbali na Halima, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA), wengine ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, na aliyekuwa Katibu Mkuu BAWACHA, Grace Tendega.

Katika orodha, wamo pia Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa Katibu Mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu BAWACHA Zanzibar na Katibu Mkuu wa BAWACHA Bara, Jesca Kishoa.


Dk. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Tanzania
Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (BAVICHA), Nusrat Hanje na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Mtwara, Tunza Malapo.


Halikadhalika wengine waliofukuzwa ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Kuhusu ujio wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA-Bara, Tundu Lissu anayeishi uhamishoni Ubelgiji, Mrema alisema: “Kama alivyosema mwenyewe kwamba atarejea kabla ya Aprili 24 mwaka huu, bado hajabadili uamuzi huo, kwa hiyo tuendelee kuwa na subira.”

HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger