Umoja Party Kubisha Hodi kwa Rais Samia Kuomba WasajiliweDar es Salaam. Uongozi wa chama cha Umoja Party umemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili kuhakikisha wanapata haki yao usajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, mwanzilishi wa Umoja Party, Seif Maalim Seif alisema waliwasilisha maombi ya usajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu Aprili mwaka jana, lakini hadi sasa bado hawajapata usajili huo, licha ya kufuata taratibu zote, ikiwemo kujibu mapingamizi yaliyowekwa juu ya rangi za bendera, nembo na mwonekano wake.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza aliliambia Mwananchi kuwa maombi yaliyowasilishwa na chama hicho yanashughulikiwa na kuwataka viongozi wawe watulivu kwa kuwa usajili una hatua na taratibu zake ambazo lazima zifuatwe.

“Huwezi kuomba leo, kesho ukapata, tatizo la binadamu akiomba jambo basi anataka alipate papo hapo, lakini kwenye usajili lazima ufuate hatua zinazotakiwa. Maombi yao yanashughulikiwa na tupo vizuri, wasilalamike barabarani waje ofisini.


“Uzuri wenyewe wanakuja hapa ofisini na tunawaeleza hatua tuliyoifikia kuhusu suala lao, sasa nashangaa wanalalamika. Waambiwe wasiwe na shaka maombi yao yanashughulikiwa,” alisema.

Hivi karibuni Umoja Party kilizua gumzo baada ya kuonekana kwa picha zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi ya watu wakiwa wamevaa sare za chama hicho, zikiwa na bendera na picha za Hayati John Magufuli.

Hatua hiyo ilisabababisha Nyahoza kuwaandika barua akionya chama hicho kuanza kufanya kazi kabla ya kupata usajili wa muda na kimekiuka utaratibu kwa sababu maombi yao yanashughulikiwa.


Katika maelezo yake, Nyahoza alisema aliwakumbusha wanaotengeneza, wanaovaa fulana hizo na Watanzania kwa ujumla kuwa ni kosa kisheria kwa taasisi yoyote kufanya kazi ya chama cha siasa wakati hakijasajiliwa.

Msimamo wa Umoja Party

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Seif alisema wanamuomba Rais Samia awasaidie kufanikisha usajili wao kwa kuwa ukimya wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa unawapa hofu ya kusajiliwa.

Alisema kadri siku zinavyokwenda ndivyo wanavyozidi kuwapata wakati mgumu kwa kuwa tayari kuna watu wanataka waanze kazi mara moja.

“Nitumie fursa hii kufanya maombi ya moja kwa moja kwa Rais Samia, yeye ndio mlinzi mkuu wa Katiba na sheria za Tanzania. Kwa taadhima ikimpendeza alitizame suala hili kwa macho mawili.


“Endapo msajili akitoa sababu zake za kutotusajili basi na sisi atufanyie hisani, atuulize na kufanya ‘check and balance’ tujue tatizo ni kitu gani,” alisema Seif.

Seif alisema chama hicho, kilikamilisha hatua zote za mchakato huo, ndio maana Novemba mwaka 2021 Ofisi ya Msajili ilitoa taarifa katika gazeti la Serikali kama kuna mtu au chama kina pingamizi kwa muktadha wa nembo, rangi na jina kuhusu kusajiliwa kwa Umoja Party basi ajitokeze na alitoa siku 21.

Alisema Februari mwaka huu, walipokea barua ya mapingamizi matatu yaliyowasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wameshayafanyia kazi.

“Tumelazimika kubadilisha nembo na rangi ya chama chetu kutokana na mapingamizi tuliyowekewa, haya yote tumeyafanya lakini bado haturidhishwi na kasi ya usajili tuliouomba, tuna hofu mambo hayaendi sawasawa kama tulivyotarajia,” alisema.


Picha ya Magufuli

Seif alisema wameamua kutumia picha ya hayati John Magufuli katika fulana zenye nembo ya chama chao kwa kuwa falsafa zake na sera zinafanana na alichokuwa akisimamia kiongozi huyo.

“Sisi alichokuwa akikifanya hayati Magufuli kilikuwa kinatufurahisha sana, aliifanya nchi yetu itekeleze miradi kwa kutumia fedha zake, aliwatetea wanyonge na kusimamia rasilimali za taifa vizuri,” alisema.

Katiba mpya

Kuhusu madai ya Katiba mpya, Seif alisema chama chake kikiingia madarakani kitajikita zaidi kuimarisha uchumi, lakini hawatasita kusimamia upatikanaji wake kama ndilo hitaji la wananchi wengi.

“Msimamo wetu upo wazi, sera yetu ni siasa na uchumi, lakini tunaheshimu wenzetu waliobeba ajenda ya Katiba Mpya kwa sababu lazima tupeane nafasi. Sisi tunataka watu wachape kazi ili kuijenga nchi yetu,” alisema.

Hata hivyo, alisema ni lazima siasa zinazofanyika zijali masilahi ya Taifa.

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad