Utatu Unaotesa Siasa za Kenya Huu Hapa

  


Agosti 9, mwaka huu mamilioni ya Waafrika na watu wa mabara mengine wataelekeza macho na masikio yao Kenya. Ni siku ambayo Taifa hilo litakuwa likifanya Uchaguzi Mkuu.

Kenya kwa historia ya hivi karibuni, uchaguzi wake umekuwa ukiundwa na upinzani mkubwa. Haukuwa ushindani mwepesi kipindi Rais wa Pili, Daniel Moi alipokuwa akigombea kutetea kiti alichokuwa amekalia.

Mwaka 2002, Moi alipokuwa anakwenda kando kikatiba, ikashuhudiwa chama tawala kikiwekwa benchi. Ushirika wa vyama vya Narc Kenya, ukimweka mbele Mwai Kibaki, ulikiangusha chama tawala, Kanu, kilichomsimamisha Uhuru Kenyatta.

Uchaguzi Kenya kwa historia umekuwa ukibeba siasa za ukabila na kutengeneza chuki za kijamii. Mara nyingi (aghalabu), uchaguzi Kenya hutawaliwa na misukosuko, vurugu na hata umwagaji wa damu. Rejea uchaguzi wa mwaka 1991/92, 1997, 2007/2008 na hekaheka za mwaka 2017.

Wakati Uchaguzi Mkuu Kenya 2022 ukiwa jirani, hatari kubwa ni teknolojia za Wamarekani na China ambazo kila upande unajinasibu kuzitumia, kuhakikisha hauibiwi kura.

Tutajadili hatari ya teknolojia, lakini tuanze na changamoto ya kimazingira; ukweli ni kuwa kwa Wakenya wengi wenye kuijua siasa kinagaubaga na wanaofahamu historia ya nchi yao, uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu pengine kuliko wowote uliowahi kufanyika ndani ya ardhi hiyo.

Uhuru ndiye Rais wa Kenya kwa sasa. Siku zinavyosogea ndivyo tarehe ya ukomo wa madaraka inavyokaribia. Uhuru aliingia madarakani kwa tiketi ya Jubilee mwaka 2013, kisha akaongeza muhula mwaka 2017 katika uchaguzi tata.

Muhula wa pili wa Uhuru umekumbwa na misukosuko mingi, deni la Taifa limepaa, rushwa imezidi kutamalaki serikalini, wakati huohuo, nchi bado inaitafuta miguu yake, ili isimame tangu dhoruba kali la Uviko-19.

Wanaochuana kuwania kiti cha urais ni Naibu Rais, William Ruto ambaye anasafiri kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na uchaguzi ujao atatumia leseni ya Azmio la Umoja.

Uchaguzi wa safari hii Kenya unabeba hisia kubwa kwa sababu nyingi; Mosi, Rais na naibu wake hawaivi chungu kimoja. Uhuru hagombei tena, ameshafika ukomo wake kikatiba. Hata hivyo, hamuungi mkono Ruto.

Uhuru amechagua kusimama na Raila. Na anasimama majukwaani kumwombea kura. Si hivyo tu, Uhuru amekuwa kiungo muhimu wa kuunganisha wanasiasa wengi wazito, ili kupata mchanyato wa Azimio la Umoja.

Pili, historia haizungumzi amani pale Uhuru na Ruto wanapokuwa pande mbili zinazopingana. Uchaguzi Mkuu 2007, Ruto alikuwa upande wa Raila, wakati Ruto alisimama kumpigia debe Kibaki.

Ushiriki wa wawili hao katika pande mbili zilizokuwa zinasigana ndio unaotajwa kuwa chanzo cha machafuko Kenya mwaka 2007 na 2008. Watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Swali ni hili; itakuwaje mwaka huu?

Jambo ambalo halitasahaulika ni kwamba Uhuru na Ruto baada ya machafuko ya mwaka 2007 na 2008, walishitakiwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), The Hague, Uholanzi. Mwaka 2014 Uhuru alishinda kesi, kisha Ruto naye aliachiwa baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha.

Turejee kwenye teknolojia za Wachina na Marekani. Uchaguzi wa mwaka huu Kenya utapewa msisimko mkubwa na majukwaa ya kimtandao kuanzia Twitter na Facebook kwa Wamarekani, kisha TikTok ya Wachina. Instagram ya Marekani itaweza kuwa na mchango wake, lakini si kufikia majukwaa hayo matatu ya awali.

Kingine ni jinsi pande zote mbili zilivyojipanga kiteknolojia kuhakikisha hawaibiwi kura. Wakati huohuo inakumbukwa kuwa Uchaguzi Mkuu 2017, mtaalamu wa teknolojia, Chris Msando aliyeingiza mfumo wa upigaji kura kielektroniki, aliuawa takriban miezi mitano kabla ya uchaguzi.

Vita ya mkate

Kinachozungumzwa mtaani Kenya ni tofauti kuhusu mgogoro wa Uhuru na Ruto. Kinachosemwa ni kwamba Uhuru amechagua kusimama na Raila kwa sababu wao wanatoka kwenye familia mbili ambazo zinaongoza kwa kujimegea vipande vikubwa vya keki ya Taifa.

Uhuru ni mtoto wa Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza wa Kenya. Raila ni mwana wa Jaramog Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa kwanza Kenya. Hivyo, wote wanatokea katika familia za viongozi wakuu waasisi wa Taifa la Kenya.

Katika hoja hii, Ruto pia anaitumia, na amekuwa akijenga hoja kuwa kumfanya Raila kuwa Rais wa Kenya baada ya Uhuru ni kuendeleza siasa za utawala wa kinasaba (dynastic politics), hivyo Wakenya wanapaswa kumchagua yeye, ili aingize vionjo tofauti vya uongozi.

Kenya kimtaani zaidi ni kuwa kuna familia tatu ambazo zimenufaika kwa kiasi kikubwa na keki ya Taifa; ya Kenyatta, Odinga na Daniel Moi, Rais wa pili wa Kenya. Mtaani inaelezwa kuwa endapo Ruto atashika hatamu ya nchi atashughulikia familia hizo, ikiwemo kunyang’anya baadhi ya mali.

Taifa la Kenya likiwa linaelekea kutimiza umri wa miaka 59 tangu lilipopata Uhuru, familia ambazo zilitambulika zaidi kwa kuchota sehemu kubwa ya utajiri wa Kenya ni ya Kenyatta na Moi. Hata hivyo, Raila alifanikisha kuiingiza familia yake kwenye mrija wa Taifa, nyakati za mwisho za uongozi wa Moi.

Kuanzia miaka ya 1990, Raila alipofanya mapatano na Moi, ulikuwa mwanzo wa familia tatu kufyonza sehemu kubwa ya uchumi wa Kenya. Sasa, mtaani inaelezwa kuwa Ruto kupitia agenda yake ya wapambanaji (Hustlers), anataka kuziba minyororo ya ulaji kwa familia hizo tatu, ili wapambanaji wa mtaani nao wanufaike.

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad