4/30/2022

Vita Russia, Ukraine vyapaisha bei ya dhahabu soko la dunia

Nafasi za Ajira Jiunge Group la Telegram la AJIRA YAKO Kwa Kubonyeza >> HAPAVITA kati ya Ukraine na Russia vimepandisha bei ya dhahabu katika soko la dunia baada ya wakia kupanda kutoka Dola za Marekani 1,412.98 (Sh. milioni 3.2) kwa Julai 2019 hadi Dola 1,947.83 (zaidi ya Sh. milioni 4.5) Machi, mwaka huu.

Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko, aliyasema hayo jana bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23 huku akiliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 83.4.

Biteko alisema kuongezeka kwa bei ya dhahabu kumetokana pia na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwapo wa ugonjwa wa UVIKO-19.

“Uchumi wa madini nchini kwa kiasi kikubwa unatokana na madini ya dhahabu  ambayo huchangia takribani asilimia 80 ya mapato yatokanayo na rasilimali madini. Wachambuzi wa masuala ya uchumi duniani walitarajia bei ya dhahabu kuendelea kuwa tulivu kwa mwaka 2022.

“Hata hivyo, bei ya madini ya dhahabu kwa wakia imepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 1,412.98 Julai 2019 hadi kufikia 1,947.83 Machi, 2022. Kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwapo wa UVIKO-19.” alisema Biteko.


 
Biteko alisema athari ya vita kati ya Russia na Ukraine inaweza kusababisha mahitaji makubwa ya madini ya dhahabu, akitoa sababu kwamba watu na taasisi duniani hupendelea kuhifadhi thamani ya fedha zao katika madini ya dhahabu kwa kuwa ni amana iliyo salama zaidi hasa wakati wa mitikisiko ya kiuchumi.

Waziri Biteko alisema mwaka 2021 bei ya madini ya almasi katika soko la dunia iliongezeka na kufikia wastani wa Dola za Marekani 241 kwa karati, ikilinganishwa na wastani wa Dola za Marekani 150 kwa karati mwaka 2020.

Alisema hadi Februari, mwaka huu, bei ya almasi iliendelea kuongezeka na kufikia wastani wa Dola za Marekani 369 kwa karati na kwamba  ongezeko hilo limetokana na kupungua kwa mlipuko wa UVIKO-19 na uhitaji mkubwa wa bidhaa za usonara zinazotumia almasi uliojitokeza katika kipindi cha sikukuu za krismasi na mwaka mpya.


Waziri Biteko alisema kuna viashiria vya bei ya almasi kwa mwaka 2022 kubadilika kwa kupanda au kushuka kutokana na Russia ambayo ni mzalishaji mkubwa wa almasi duniani kuwa katika vita na Ukraine.

“Ili kunufaika na ongezeko la bei za madini, wizara inakusudia kuchukua hatua mbalimbali, ikiwamo kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuangalia uwezekano wa kupunguzwa kwa baadhi ya kodi na tozo kwa wachimbaji ili kuwaongezea wigo wa faida na kuchochea uzalishaji zaidi.,” alisema Biteko.

Kuhusu utoroshaji madini, Waziri Biteko alisema mojawapo ya hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuimarisha ukusanyaji maduhuli ni pamoja na kudhibiti biashara haramu na utoroshaji wa madini.

Alisema kazi hiyo hufanywa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya pamoja na raia wema.


 
Biteko alisema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, mwaka huu, madini ya aina mbalimbali yakiwamo dhahabu, vito, mchanga na madini ya viwandani yenye thamani ya Sh. milioni 501.2 yalikamatwa katika matukio ya utoroshaji na biashara haramu katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Manyara, Dodoma, Lindi, Geita, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger