4/12/2022

Yanga yawalilia Aucho, Fei Toto

Nafasi za Ajira Jiunge Group la Telegram la AJIRA YAKO Kwa Kubonyeza >> HAPABAADA ya kufanikiwa kutinga kwa mbinde nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), maarufu FA Cup juzi, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema pamoja na mafanikio hayo kutokuwapo kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Khalid Aucho ni tatizo kubwa kwao katika utengenezaji wa nafasi.

Yanga juzi ilifuzu nusu fainali ya Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti 7-6 baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold FC kwenye mechi ya robo fainali iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumzia mchezo huo baada ya mechi kumalizika, Kaze alisema mchezo ulikuwa mgumu kwa upande wao kutokana na wachezaji kucheza kwa kupooza na Geita Gold FC kumiliki vizuri mpira hasa katika safu ya kiungo na kushindwa kutengeneza nafasi ya mabao.

Alisema Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza hawakuwa fiti kwa asilimia 100, hivyo kusababisha kucheza chini ya kiwango na hayo yote yakichangiwa na kukosekana kwa mtu wa kupelekea mipira.

“Tatizo si kufunga au kutumia washambuliaji wawili, bali lilikuwa ni kukosekana kwa mtu wa kufikisha mipira mbele, tumeliona hilo na sasa tutalifanyia kazi kwa kipindi hiki ambacho tutawakosa Fei Toto na Aucho,” alisema na kuongeza:


 
“Mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu Geita Gold FC walicheza vizuri dakika zote walifika mbele na kupata nafasi moja na kuitumia vizuri, sisi tulishindwa kutumia nafasi tulizopata na kuingia katika hatua ya penalti na bahati kuwa kwetu,” alisema Kaze.

Kuhusu suala la kipa wao, Djigui Diarra kukosa penalti, ilikuwa bahati mbaya kwa sababu kipa huyo ni mzuri na hufanya vizuri katika mazoezi ya kupiga penalti.

“Tunashukuru kupita na kwenda kucheza nusu fainali na sasa tunaenda kujiandaa na michezo yetu ijayo kwa kufanyia kazi mapungufu yetu,” alisema Kaze.


Kwa uapnde wa Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Fred Felix Minziro, alisema alikuja kutafuta matokeo, lakini mwisho wa siku Yanga walifanikiwa kupita kwa Penalti.

“Tumekubali matokeo bahati haikuwa kwetu, Yanga wamefanikiwa kushinda na sasa tunaangalia mechi zilizopo mbele yetu kwa kufanyia kazi mapungufu yetu,” alisema Minziro.

Naye mchambuzi wa soka, Ally Mayai alisema kutokuwapo kwa Fei Toto na Aucho kunaonyesha mapungufu katika safu ya kiungo ya Yanga ndiyo sababu iliwafanya Geita kutawala kati.

“Yanga walishindwa kupata watu ambao wanapelekea mipira mbele, kwa sababu ukiangalia Geita Gold FC walifanikiwa kutawala nafasi ya kiungo na kuhakikisha Yanga wanashindwa kupeleka mipira mbele,” alisema.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger