5/24/2022

CHADEMA yaomba usalama kina Lissu

JIUNGE NA GROUP LA TELEGRAM LA AJIRA YAKO KUPATA AJIRA MPYA ZINAZOTANGAZWA KILA SIKU BONYEZA HAPA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewasilisha kwa serikali hoja kuu mbili za kufanyia kazi ambazo ni kushughulikia madhara yaliyotokana na ukiukwaji wa haki pamoja na kurejeshwa na kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.
Katika hoja yake ya kwanza inayohusu haki, chama hicho kimeiomba serikali kuwahakikishia usalama viongozi na aliowaita wakimbizi wa kisiasa.

Viongozi wa chama hicho wanaoishi nje ya nchi kwa sasa kutokana na kile wanachodai tishio la usalama wao ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, jana  alipozungumza na waandishi wa habari, alibainisha kuanza kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa chama hicho ulioongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe na upande wa serikali ulioongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Katika kikao chetu na viongozi wa CCM na serikali, tulitaka hakikisho la usalama kwa viongozi na wakimbizi wengine wa kisiasa walioko nje ya nchi.


 
"Vilevile, tulitaka kuondolewa bungeni kwa waliokuwa wanachama 19 wa CHADEMA na kushughulikia masuala yaliyowakumba viongozi kutokana na ukandamizwaji wa demokrasia," Mnyika alisema.

Aliendelea: "Kuhusu katiba mpya, tunaamini ni nyenzo kuu ya kulipeleka taifa letu mbele na kufungua ukurasa mpya wa kimfumo na kitaasisi. Katika nchi yetu tumepeleka upande wa serikali mapendekezo yetu juu ya namna ya kung'amua mchakato wa katiba ulipokwamia."

Alisema katika hilo rai na mapendekezo yao wameelekeza katika kuwa na ratiba na taratibu zitakazowezesha Katiba Mpya kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. 


Kuhusu madhara yaliyotokana na ukiukwaji wa haki, Mnyika alisema katika mazungumzo yao na upande wa serikali, waliwasilisha mapendekezo 10 ikiwamo kuundwa kwa tume ya ukweli na upatanishi na kushughulikiwa kwa madhara yatokanayo na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Jambo lingine ni kufutwa kesi zenye mwelekeo wa kisiasa na kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa. Lingine ni kufutwa au kurekebishwa kwa sheria kandamizi katika nchi yetu. Jambo lingine ni kushughulikia masuala yanayohusu viongozi wa chama na watu walioshambuliwa, kupotea au kuuawa kwa sababu za kisiasa," alisema.

Mnyika ailisema huo ni mwanzo tu wa mazungumzo na hatua nyingine zinafuata na kuwataka wanachama wa chama hicho kuwa watulivu katika hatua hizo zilizoanza kwa kuwa mchakato wa maridhiano na wa muda mrefu unafanyika hatua kwa hatua.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza msimamo wa kutoshiriki kutoa maoni katika kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia na kusema kuwa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa  chama hicho kitatoa maoni mbele ya kikosi kazi leo si ya kweli.


 
“Ninaomba umma na wanahabari mfahamu kuwa CHADEMA haitakwenda kesho (leo) 24 Mei kutoa maoni mbele ya kikosi kazi. Msimamo wetu kuhusu mchakato unaoendelea wa kikosi kazi ni ule ule haujabadilika," alisema Mnyika.

KAULI YA CCM

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema jana jijini Dodoma kuwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyoketi juzi jijini Dodoma, mbali na kupokea na kujadili mambo mbalimbali, ilimpongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele kutafuta maridhiano na viongozi wa kisiasa nchini ili kusaidia uwapo wa haki, amani na umoja wa kitaifa.

"Kamati Kuu imempongeza mwenyekiti wake kwa kuendelea kushiriki majadiliano ya kupata maridhiano na makundi mbalimbali ya kisiasa wakiwamo viongozi wakuu wa vyama, akiwamo (Prof. Ibrahim) Lipumba na hivi karibuni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

"Maridhiano ndiyo njia pekee ya kuendeleza amani, haki na umoja wa kitaifa ambao waasisi wetu walituachia, hivyo Kamati Kuu inampongeza sana Rais Samia kwa kuendeleza jitihada za kutafuta maridhiano nchini," alisema.


Shaka alisema vikao hivyo vya maridhiano ni njia ya kutafuta mwafaka wa pamoja na CCM ipo tayari kuendelea na mijadala ya kuimarisha demokrasia nchini.

Aliwataka Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao, kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada hizo za kutafuta maridhiano na umoja wa kitaifa.

Rais Samia hivi karibuni alishiriki ufunguzi wa mkutano wa haki, amani na maridhiano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) ambao pamoja na mambo mengine, aliagiza kutolewa maoni ya namna bora ya vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara.

Pia, aliagiza kukusanywa kwa maoni yatakayosaidia kufanya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa na ile ya uchaguzi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na vyama vya siasa.

*Imeandikwa na Jenifer Gilla (DAR) na Paul Mabeja (DODOMA)

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger