5/04/2022

CHADEMA yaombwa kujitizama tena, lakini kupunguza ukali 
SIKU chache baada ya CHADEMA kusita kutoa maoni kwenye kikao cha Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kupokea mapendekezo katika maeneo kadhaa ikiwamo katiba, chama hicho kimeshauriwa kubadili msamamo huo mkali kwa manufaa ya Watanzania.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, akisema chama hakijaridhia kutoa maoni. PICHA: MTANDAO.
Katibu wa Kikosi Kazi cha Rais Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, wiki iliyopita alisema, chama hicho ni moja ya vyama vya siasa vinavyotarajiwa kutoa maoni na mapendekezo yao Mei 9, mwaka huu, lakini kilitoa msimamo unaoonyesha kutokuwa tayari.

Chama kinadai hakitakuwa tayari kushiriki katika kikao hadi kuwe na makubaliano ya wapi pa kuanzia na ajenda za mazungumzo ziwe wazi.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, Abbas Mwalimu, anasema, kinachofanywa na CHADEMA ni siasa za kuviziana na kushauri viongozi wake kubadilisha msimamo kwa manufaa ya umma.

"Busara iwaongoze viongozi wa chama hicho kushiriki mchakato unaoendelea wa kutaka kupatikana katiba mpya, kwani kususia ni sawa na kupoteza nafasi ya kutoa maoni na maduku duku yao," anasema Mwalimu.


 
Siasa za kuviziana na kutafuta sababu za kukwamisha mchakato huo siyo jambo jema, badala yake wadau washirikiane ili kuhakikisha nchi inapata katiba, kwa kutoa maoni yanayohitajika, anasema Mwalimu.

"Lengo kuu la katiba ni kuleta ustawi kwa wananchi, lakini wanasiasa watazama sehemu yao yenye maslahi kwao, wanasahau kuwa inagusa ustawi wa jamii, usalama, utamaduni na pia uboreshaji wa huduma za umma. Watoe maoni badala ya kuendelea kutoa visingizio kila wakati.”

Anafafanua kuwa suala la kuwapo kwa katiba linategemea utashi wa Rais na kwamba Rais Samia, ameonyesha utayari huo akiwataka wanaosusa kuacha mambo hayo.


"Nikumbushe kuwa kupata katiba kunahitajika utafiti kisayansi, ikiwamo kujifunza kwa wengine walivyofanikiwa kutengeneza katiba yao au ni wapi wamekwama ili kuwe na pa kuanzia. Yote yanahitaji ushirikiano," anasema Mwalimu.

  HAKI KIDEMOKRASIA

Mwana harakati, mtetezi wa haki za binadamu Dk. Helen Kijo-Bisimba, anasema, hivyo ndivyo demokrasia ilivyo, kwamba msimamo  wa chama hicho ni jambo la kawaida katika siasa, na kwamba la muhimu uwe na mashiko.

Anafafanua kuwa hajazizingatia sababu zinazokifanya chama hicho kutoshiriki vikao vinavyoandaliwa na kikosi kazi, bali anachojua ni kwamba, kila mmoja ana haki ya kukataa au kukubali jambo kulingana na jinsi anavyoliona.

"Sioni tatizo kama kuna sababu za msingi za viongozi wa chama hicho kukataa kushiriki vikao vya kikosi kazi kilichoundwa kutafuta katiba bali ninachukulia kama haki yao kidemokrasia," anasisitiza Dk. Kijo-Bisimba.


 
Anaongeza kuwa, kinachotakiwa kufanywa na wadau au Kikosi Kazi hicho ni kuchambua hoja za chama hicho ili kuona zina uzito gani, kwa maelezo kwamba viongozi wa chama hicho wanaweza kuwa na hoja za msingi.

"Kwanza tujiulize, CHADEMA wamekuwa mstari wa mbele kudai katiba mpya, wamepewa nafasi kupitia Kikosi Kazi, lakini wanakataa, kwa nini? Inawezekana wana sababu za msingi," anasema.

Mkurugenzi Mtendaji mstaafu huyo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anasema suala katiba mpya linahitaji maridhiano, na kwamba iwapo baadhi ya watu wakikataa kushiriki mchakato, huwa kuna jambo haliko sawa.

          MSIMAMO WA CHADEMA

Baada ya kutangazwa kwa kikao hicho wiki iliyopita, Nipashe ilizungumza na Mkurugenzi wa Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, ambaye alisema chama hakijabadili msimamo.


"Kama ambavyo Kamati Kuu iliazimia kuhusu kutoshiriki mchakato huo, hadi sasa hakuna uamuzi uliobadilika na tuna imani kuwa tutaweza kufanya mazungumzo kwanza ili tukubaliane tunaanzia wapi na ajenda za mazungumzo zitakuwa zipi.

"Tumemsikia mheshimiwa Rais alipokuwa Marekani aliweka wazi kuwa ataendeleza mazungumzo hayo, nasi tutakuwa tayari kuendelea baada ya kuweka misingi ya mazungumzo husika."

Wakati chama kikiwa na msimamo huo, taarifa ya Kikosi Kazi inaonyeha kuwa maoni na mapendekezo ya wananchi na taasisi katika maeneo hayo tisa yatapokewa jijini Dar es Salaam kuanzia kesho hadi Mei 13, mwaka huu.

Ratiba hiyo pia inaonyesha kuwa kesho watakaoanza kutoa maoni na mapendekezo ni CCM),  ACT-Wazalendo na kufuatiwa na Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD).

Mei 6 itakuwa siku ya CUF, NCCR-Mageuzi kutoa maoni yao na siku itakayofuata (Mei 7) ni Jumuiya ya Wahindu Tanzania na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).


 
Mei 9 itakuwa nafasi kwa CHADEMA, ADC, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) huku kesho yake vikifuatia vyama vya United Peoples Democratic Party (UPDP), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA) na Alliance for African Farmers Party (AAFP) na vingine vyote.

Masuala yanayojadiliwa na Kikosi Kazi ni pamoja na katiba mpya, mengine yanayotolewa maoni na mapendekezo ni mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi na elimu ya uraia.

Mengine ni mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa na ushiriki wa wanawake na makundi maalum katika siasa na demokrasia ya vyama vya siasa.

Rushwa, maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa na uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma pia yanatakiwa kutolewa maoni na wadau hao

HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger