5/07/2022

Hatimaye LATRA yaruhusu nauli mpya kuanza kutumikaMAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) imeruhusu wamiliki wa magari ya abiria jijini Mwanza (daladala) kuanza kutoza nauli mpya, ikitengua agizo la awali walilotoa la kupandisha nauli kuanzia Mei 14 mwaka huu.

LATRA jijini Mwanza jana ilitangaza kuanza kutumika nauli mpya ambayo ni ongezeko la Sh. 100 kwa kila safari, kinyume cha tangazo lake la awali, lengo likitajwa kuwa ni kuepuka mgomo wa kutoa huduma ya usafiri uliokuwa umepangwa na wamiliki wa daladala kama kusingekuwa na ongezeko la nauli.

Jana asubuhi, gari la matangazo lilipita maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza na kutoa tangazo la ongezeko la bei kwa usafiri wa daladala.

Akizungumza na Nipashe, mmoja wa maofisa wa LATRA jijini Mwanza ambaye hakutaka kutaja jina lake, alikiri kwamba bila kufanya hivyo, wamiliki wa magari hayo wangegoma kutoa huduma.

Alisema uamuzi wa awali ulikuwa nauli mpya ianze kutumika Mei 14 mwaka huu kwa ongezeko la Sh. 100 kwa kila safari moja ama kituo kimoja hadi kingine.


Hata hivyo, alisema ili kuzuia mgomo huo wa wamiliki wa daladala, walilazimika kutangaza nauli hiyo ianze jana badala ya Mei 14.

Aliongeza kuwa juzi jioni walifanya kikao na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kukubaliana kwamba jana watangaze nauli mpya kwa jiji zima.

Alisisitiza kupanda kwa nauli kumetokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika mikoa mbalimbali ambayo imesababisha wamiliki wa daladala kulalamika kutaka nauli nayo iongezeke.


Kutokana na hali hiyo, jana asubuhi baadhi ya abiria walilamikia na hata kufikia hatua ya kurushiana maneno na makondakta wa daladala waliotaka kuwalipisha nauli mpya.

Baadhi ya abiria walisema nauli hiyo iliyotangazwa na LATRA, muda wake wa kuanza kutumika ulikuwa bado na kwamba walishangaa jana kuambiwa imepanda.

Hivi karibuni LATRA ilitangaza nauli mpya za mabasi ya mijini, maarufu daladala, na mabasi ya masafa marefu yanayokwenda mikoa mbalimbali nchini.

Akitangaza kiwango hicho kipya cha nauli hiyo Aprili 30 mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe, alisema kiwango hicho kipya kingeanza kutumika baada ya siku 14.


Alisema kwa mabasi ya mijini kuanzia kilomita 0 hadi 10 nauli itakuwa Sh. 500 badala ya 400 na nauli ya Sh. 450 itakuwa ni 550.

HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

Share:
Loading...

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger