IGP Sirro "Panya Road wamenivunjia heshima Kufanya Uhalifu Eneo Ninaloishi"SIKU chache baada ya kundi la vijana wanaofanya uhalifu mitaani, maarufu panya road kuvamia nyumba 23 eneo la Chanika jijini Dar es Salaam kisha kujeruhi na kupora mali za raia, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, amesema kitendo hicho ni sawa na kumvunjia heshima kwa kuwa uhalifu wa aina...

hiyo umefanyika anakoishi.

IGP Sirro alitoa kauli hiyo juzi Chanika wakati akiwa kwenye kikao ambacho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, walipotembelea majeruhi wa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumapili ya wiki iliyopita.

Akizungumza katika kikao hicho, IGP Sirro alisema Chanika ni kwake na ana miaka 28 anaishi huko na aliposikia habari ya tukio hilo la wananchi kuvamia na kujeruhiwa, alipata tabu.

"Lakini, ninajua historia ya Chanika, ndiyo maana kama mnakumbuka nilikazana tujenge Kituo cha Chanika, ndiyo maana kama mnakumbuka nilisema tuifanye kuwa Wilaya ya Kipolisi kwa sababu ninajua tabu ya vijana wetu.

“Niwape pole kwa kilichotokea lakini mimi siyo msemaji, niwahakikishie mahali anakotoka IGP kuwa na uhalifu wa namna hii ni kumdhalilisha IGP, narudia mahali anakotoka IGP kufanya matukio ya ovyo namna hii ni kumdhalilisha IGP.”


Alisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na waziri wana mambo mengi ya kufanya, hivyo hawapaswi kuwapa shida ya kufikiria Chanika.

Aliwawaeleza wana Chanika kuwa vijana waliofanya hivyo watawapata na mali zilizochukuliwa zitapatikana.

“Bahati nzuri niliwahoji baadhi yao. Kwa mfano, Yunusi anachoeleza ni utoto ni kijana ana miaka 13 au 14 ni kijana wa kwetu, walichofanya wanakutana kwenye mchezo wa pool table, viwanja vya mpira wanavuta bangi, wanakunywa konyagi halafu wanakwenda kufanya kazi hii.


“Vijana wetu 10 wa Chanika walishiriki katika hili, vijana kutoka Mbagala, mjini Kariakoo takribani 21, jumla walikuwa 31, mali yetu imechukuliwa nyingi imepelekwa sehemu ambazo siwezi kusema, lakini tumepata mahali pa kuanzia, tutapata majibu," alifafanua.

IGP Sirro aliwaeleza wana Chanika kuwa anapoweka mguu mahali mara zote husimamia suala la haki.

“Huwezi kutafuta televisheni yako halafu anakuja mtu kufanya mambo ya ovyo ovyo, hii kwetu ni matatizo na ni fursa, Mheshimiwa Waziri nikueleze shida moja waliyonayo wana Chanika, baadhi yetu suala ni ubinafsi, bahati nzuri umelizungumzia hili nimekuwa nikipiga sana kelele,” alisema.

Alibainisha kuwa askari waliopelekwa huko ni wachache kulinganishwa na idadi ya wananchi na ili kuziba pengo hilo ni suala la kuwa na vikundi vya ulinzi shirikishi.


“Lakini, Mheshimiwa Waziri mtu ana kuambia ‘Mimi nina kitu gani? Nitakuja kuibiwa kitu gani?’ Akiwa na nyumba yake akiwa na chumba chake ukimwambia changia Sh. 1,000 anasema ‘wachangie matajiri’ sasa ndugu zangu kama mtaa hakuna mtu usiku, hakuna ulinzi shirikishi, mtaa utakuwa na vibaka tu.

“Huwa ninawaambia ukienda maeneo mengine kuna vikundi shirikishi, sasa wametoka Mbagala wamekuja kutuumiza kwa sababu hatuna ulinzi shirikishi, lakini sheria zipo ndogondogo, nilikuwa ninamuuliza Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, (Jumanne Muliro) tuchukue sheria zile tuwashtaki wasiotaka kushiriki ulinzi wa umma, ulinzi wa umma ni wa lazima.

“Mwingine anasema ‘nina geti nina ulinzi wangu’ hao watu 31 au 40 habari ya geti siyo kitu, wataingia watakushughulikia utakufa utaacha mali," alionya.

Masauni aliwasilisha pole za Rais Samia kwa wananchi hao na kuwaeleza kuwa lilimgusa, kumsononesha na kumsikitisha, hivyo akapewa maelekezo.


Katika mkutano huo mama mmoja ambaye watoto wake watatu walijeruhiwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kundi hilo aliishia kulia huku akimweleza waziri kuwa watoto wake wamepata matibabu lakini anadaiwa fedha za matibabu na uwezo hana.

Mkazi mwingine Majaliwa Rashid alisema wazazi wanachangia watoto wao kuharibikiwa kwa sababu licha ya kufanya makosa huwalinda.

Mzazi mwingine Khadija Sindi alitoa ushauri kwa IGP Sirro utaratibu wa zamani kila mjumbe wa mashina kujua watu wake urejeshwe kwa sababu kwa sasa chumba kimoja wanakuta 'masela' sita na wapo wanavuta cocaine na bangi.

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad