Madai ya Tume Huru ya Uchaguzi yashika kasi

 


Hoja ya mabadiliko katika mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeonekana kujirudia zaidi katika maoni yaliyowasilishwa na makundi mbalimbali mbele ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, wakisema itasaidia kurejesha mamlaka kwa wananchi.


Hoja ya tume huru ni miongoni mwa hoja tisa zilizochambuliwa na kikosi hicho kilichoundwa baada ya mkutano wa wadau wa vyama wa siasa Desemba 15, mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeweka wazi kushughulikia changamoto za kisiasa nchini.


Katika hatua ya upokeaji wa maoni ya wadau, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba na Baraza la Baraza la Habari Tanzania (MCT), walishiriki siku ya kwanza wakigusia umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa tume hiyo, huku wakisisitiza zaidi mchakato wa kupata Katiba mpya uanze sasa.


Siku ya pili Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) walisisitiza umuhimu wa mageuzi ya mfumo wa tume ya uchaguzi itakayokuwa huru kupitia teuzi za wasimamizi wa chaguzi.


Jana ikiwa ni siku ya mwisho, pamoja na hoja nyingine, makundi ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) yaliwasilisha hoja hiyo ya namna ya kuwa na tume huru itakayorejesha mamlaka kwa wananchi.


Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Kondo Bungo alisema maoni yao yameelekeza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi kwa kuondoa mamlaka ya wakurugenzi kusimamia chaguzi wakati ni wateule wa rais, ambaye ni miongoni mwa wagombea.

“Sasa tumeeleza kuwa demokrasia ni maamuzi ya watu, tusikatishe tamaa wapiga kura wakaanza kupuuza chaguzi, kwa hiyo wabadilishwe ili haki iwepo,” alisema Bungo.


Hoja nyingine zilizowasilishwa na taasisi hiyo ni kuondoa mamlaka ya rais kuteua majaji ili kuepuka changamoto za majaji wengi kutoa uamuzi unaoshinikizwa na misukumo ya kisiasa. Alisema Tanzania inaweza kuwa kama Kenya yenye majaji wanaofuta uchaguzi unaohusisha mgombea ambaye ni rais.


Meneja Program wa TLS, Mackphason Buberwa alisema TLS iliwasilisha hoja saba kati ya 17 walizokuwa wameandaa, ikiwamo pendekezo la kubadili Sheria itakayoimarisha uhuru wa tume hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake. “Tume haiko huru, tumeshauri tume iundiwe sheria yake ili kuipatia mamlaka kamiliki bila kuingia na upande wowote, mwaka 2020 tume yenyewe ilipendekeza iundiwe sheria, kwa hiyo tumepitia hapo hapo, hata mawakala wa chaguzi wasitokane na watumishi wa umma ili kuondoa upendeleo,” alisema.


Hoja nyingine zilizowasilishwa na TLS ni pamoja na namna ya kutoa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa nchini, kuimarisha ushiriki wa makundi maalumu katika chaguzi, kuhuisha mchakato wa katiba ili uendelee na kuondoa kikwazo cha Polisi katika mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.

Maeneo tisa

Maoni yote yalitokana na msingi wa maeneo tisa, ikiwamo hoja ya mikutano ya hadhara na ya ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.


Mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na Katiba mpya

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad