Mbunge Tarimba: Nikibahatika kuteta na Rais Samia nina haya kumwelezaMBUNGE wa Kinondoni, Abbas Tarimba, ametaja mambo mawili yanayotawala kifikra zake, hata atakapopata faragha na Rais, atayawasilisha rasmi, akiyataja ni; kuwapo bima ya afya kwa kila Mtanzania, na maboresho kwa baadhi ya kodi.

Tarimba aliiambia Nipashe jijini hapa hivi karibuni kwamba ushuhuda wake wa magumu ya matibabu yanayoukabili umma, pia kasi ya kupanda kwa gharama za maisha kunaweka ulazima wa kuwapo hatua hizo, kuwaletea unafuu wananchi.

Mwanasiasa huyo ambaye awali alikuwa diwani, pia sasa anaongoza taasisi ya SportPesa, alisema mtazamo wake unatokana na alichokishuhudia muda wote kwenye uongozi wa kisiasa, pia watu wanavyoathiriwa na ongezeko la bei ya mahitaji muhimu linalojitokeza kwa sasa.

Ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo ya Nipashe na mbunge huyo ambaye ni mdau mkubwa wa michezo:

SWALI: Ukipata nafasi ya kuteta na Rais Samia japo kwa dakika moja, utamshauri jambo gani kubwa kwa Taifa?


 
TARIMBA: Kwa upande wa kitaifa ninatamani sana tunakuwa na bima ya afya kwa kila Mtanzania. Nilipokuwa diwani na sasa mbunge, nimeona Watanzania wengi wanahangaika katika masuala ya afya kwenda kupata matibabu.

Hivyo, nikipata nafasi ya kuzungumza naye, nitamwambia Mheshimiwa Rais kwamba serikali ijipige kadri inavyoweza iweze kupata bima ya afya kwa kila Mtanzania.

La pili; nitamshauri kufanya mapitio ya kodi zote zinazomgusa mwananchi moja kwa moja ili kuzuia kupanda gharama za maisha.

Zipo kodi zinaweza kuangaliwa ili mwananchi wa kawaida aweze kupata nafuu ya kimaisha, hii inaweza kwenda sambamba na kutanua wigo wa watu kulipa kodi.

SWALI: Kero kubwa ya Kinondoni kwa sasa ni ipi? Hatua zipi zimechukuliwa kuitatua?

TARIMBA: Nilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2020, mchango wangu wa kwanza ulikuwa ni kuiomba serikali kuharakisha kuanza kwa mradi wa Mto Msimbazi ili wananchi wanaopitiwa na mto huo waweze kuepukana na mafuriko ya mara kwa mara.

Kwa hiyo, moja ya ajenda yangu kubwa ni kuhakikisha tunapambana na hili tatizo la mafuriko. Ajenda yangu ya kwanza ikawa kuiomba serikali juu ya mradi wa Mto Msimbazi uweze kuanza. Na huo ndiyo ulikuwa mchango wangu wa kwanza kabisa nilipoingia bungeni. Bahati nzuri huo mradi unakwenda kuanza Julai mwaka huu na matatizo ya wakazi wa maeneo wanaopitiwa na Mto Msimbazi yanakwenda kuisha.


 
SWALI: Ni mafaniko gani yamepatikana kwa muda mfupi ndani ya Jimbo la Kinondoni?

TARIMBA: Mimi ni mkazi wa Kinondoni pia nimefanya uwekezaji hapo, hivyo mimi ni mdau kama walivyo wakazi wengine, mimi ni mkereketwa kama walivyo wakereketwa wengine wa maendeleo Kinondoni.

Nilitaka ubunge ili nisaidie kutoa huduma ambayo mimi mwenyewe ningependa kuipata kutoka kwa mbunge. Kuna vitu ambavyo tulikuwa tunakosa wakazi wa Kinondoni kwa muda mrefu.

Kinondoni ni jimbo lililoko mjini lakini lina changamoto nyingi. Karibia asilimia 75 ya eneo lake lipo kwenye mabonde na mito, hivyo wananchi wake wanapata matatizo makubwa wakati wa mvua.

Mimi nimewahi kuwa diwani kwa miaka 10, nimeona yanayotokea Kijitonyama, Makumbusho, Tandale, Mzimuni, Kigogo. Hivyo, moja ya ajenda yangu kubwa ni kuhakikisha tunapambana na hili tatizo la mafuriko.

Ajenda yangu ya kwanza ilikuwa ni kuiomba serikali juu ya mradi wa Mto Msimbazi uanze. Na huo ndiyo ulikuwa mchango wangu wa kwanza kabisa nilipoingia bungeni kama nilivyodokeza hapo awali.

Ninahangaika kuhakikisha wale watakaopitiwa na mradi huo na nyumba zao kubomolewa wanapata stahiki zao mapema.

Nimekuta mradi wa Mto Ng’ombe ambao unapita katika maeneo mengi serikali ilishaanza kuutekeleza kwa Sh. bilioni 32.

Nilipoingia nilikuta mradi huu unasuasua sana, nikaanza kuufanyia kazi kwa kuhakikisha mkandarasi anakuwa kazini.


 
Wananchi walikuwa wanahangaikia kulipwa fidia, lakini baadaye serikali ilitoka Sh. bilioni 4.3, hivyo kwangu ni mafanikio makubwa kwa wananchi kulipwa fidia zao.

Mimi nimelenga maeneo makuu yanayowagusa watu. Pia nimejikita katika kata ambazo hazijawahi kupata huduma za afya wala shule.

Kwa mfano, Kata ya Kinondoni haijawahi kuwa na huduma hizo. Nilichokifanya siku ya kwanza niliwachukua madiwani wote wa jimbo langu nikaja nao bungeni, tukakutana na Waziri wa TAMISEMI.

Niliwaleta ili waje waone mchakato pamoja na wao waongeze uzito. Hivi ninavyozungumza shule ya sekondari inajengwa katika Kata ya Kinondoni.

Sasa hivi pia kuna ujenzi wa kituo cha afya, hivyo katika kata zangu zote ambazo hazikuwa na huduma hizo zinakwenda kupata.

Kwenye Kituo cha Afya Kigogo tunahangaikia kupata fedha kwa ajili ya kujenga jengo la kuhifadhi maiti, tathmini imeshafanyika. Hivyo, kwenye maeneo ya kijamii tumefika mbali sana.

SWALI: Unawezaje kujigawa kufanya majukumu ya kibunge, Mkurugenzi wa SportPesa na baba wa familia?

TARIMBA: Ubunge kwangu mimi kama ibada, nikimwangalia binadamu ninauona utukufu wa Mungu, ninaona kumtumikia Mungu kupitia kuwatumikia binadamu.

Ukifanya kazi ya kumtumikia binadamu, wewe mwenyewe unanufaika. Mimi ninanufaika kwa imani yangu kupata rehema za Mungu.

Kuhusu SportPesa, nina wafanyakazi, siku hizi tunaendesha shughuli kwa mtandao, mafaili yote ninayaona kwa simu, ninapata muda wa kuyapitia, nikipata nafasi mwishoni mwa wiki ninakwenda ofisini.

Kwenye ubunge sijaharibikiwa, nikiwa hapa bungeni ninafanya shughuli zangu, mimi ni mjumbe wa kamati, ninafanya shughuli zangu vizuri. Ninapata nafasi ya kwenda jimboni kama kuna ziara au shughuli inayonihitaji ninakwenda.

Ubunge wangu ni wito, siuchukulii kama ajira, ninauchukulia kama wito wa kuwatumikia wanadamu pamoja na Tanzania.
Kuhusu familia, sina tatizo sana kwa sababu mke wangu anasimamia mambo yangu, biashara zangu, familia anasimamia yeye.

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad