Sure Boy Afunguka "Nabi nipe hawa Simba SC Niwanyooshe"


Sure Boy amemwambia kocha wake Nasreddine Nabi ampatie nafasi katika mechi ya nusu fainali kombe la Shirikisho dhidi ya Simba ili wananchi wafurahi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sure Boy alisema baada ya kuukosa mchezo uliopita akipewa dakika chache dhidi ya Simba kwenye ligi, sasa anatamani mchezo wa Mei 28 apate muda wa kutosha ili awafanyie kazi bora zaidi mashabiki wa timu hiyo.

Sure Boy ambaye ameanza kutengeneza mabao, alisema anaamini kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi hatakosea akimpa nafasi hiyo akiamini kuwa ubora wa timu hiyo kwasasa utaifanya Yanga kushinda mchezo huo.

“Siwezi kulalamika juu ya muda niliopewa kwenye mechi iliyopita, makocha wanajua zaidi kuliko mimi, ila safari hii namuomba kocha aniamini kwa muda zaidi, mashabiki wa Yanga wanatakiwa kufurahi,” alisema Sure Boy anayefahamika pia kama Babu Kaju.


“Kwasasa naijua Yanga, sio kwamba mimi ni bora lakini nacheza na watu bora ambao wananipa wepesi, mimi sio mtu wa kuogopa mechi tunaheshimu tunakwenda kukutana na timu kubwa kama sisi lakini Yanga tupo kwenye ubora na mashabiki wetu wana nguvu ya kutushangilia wakati wote,” alisema.

Aidha, Babu Kaju alitoa kauli juu ya mwanzo wake bora katika kikosi hicho akisema uwepo wa wachezaji wengi waliokomaa kiakili unampa wakati mzuri kufanya majukumu yake.

“Siwezi kuisema vibaya Azam ile ni timu ambayo imenilea naiheshimu sana lakini kitu tofauti hapa Yanga ni kwamba kuna wachezaji wengi waliokomaa kiushindani, unapopiga pasi unampa mtu ambaye anakwenda kuendeleza kitu kwa ubora sasa hapo lazima mambo yawe rahisi.


“Ushirikiano ni mkubwa sana kwa wenzangu kuanzia mazoezini hadi uwanjani tunapocheza mechi, maisha yetu yamekuwa ya furaha tunafurahia kazi yetu, eneo la namna hiyo lazima mchezaji ufanye makubwa uwanjani.”

Achekelea kurudi Stars, ajipanga

Sure Boy alisema amefurahia kurudishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, jukumu alilonalo ni kuipambania timu kufanya vizuri kwenye michezo kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2023.

“Soka ni mchezo wa wazi kila mmoja anauona hivyo naamini kurudishwa kwangu kumetokana na kiwango kizuri ninachokionyesha kwenye timu yangu ya Yanga. Ninachokifanya huku ndicho nitakachokifanya Stars nikisaidiana na wachezaji wengine walioitwa wote tukiwa na lengo moja,” alisema na kuongeza;

“Nafurahia kurudi kikosi cha Stars ni heshima kulitumikia taifa kila mchezaji anatamani kuichezea Taifa Stars lakini sio rahisi wote tukaitwa hivyo nafasi niliyoipata nitaitumia vyema ili kuwahakikishia Watanzania kuwa sio bahati mimi kujumuishwa bali ni uwezo.”


Alisema umefika wakati wao kuhakikisha wanaitendea haki Stars kwa kuipambania ili na Tanzania pia iingie kwenye mataifa ambayo timu zao za taifa zinafanya vizuri huku akithibitisha kuwa kila aliyeitwa ni bora hivyo watafanya kilicho bora.

Kocha wake wa viungo, Mayele

Kocha wa mazoezi ya viungo wa Yanga, Helmy Gueldich amefunguka kuwa Sure Boy ni kiungo mwenye akili kubwa na uwezo wake kufikiri ni mkubwa anapokuwa uwanjani huku akimfananisha na viungo wa zamani wa Barcelona, raia wa Hispania Xavi Hernandez na Andre Iniesta.

“Sijaona kiungo mwenye akili kubwa inayofikiria kwa haraka hapa Tanzania kama Sure Boy, ni kiungo sahihi aliyetakiwa kuja Yanga muda mrefu nyuma, amefanya maisha ya timu yetu sasa kuwa ya furaha karibu muda wote.

“Bahati mbaya amezaliwa hapa Tanzania, huwa nikimuangalia mazoezini na hata kwenye mechi najiuliza huyu kwanini hafananishwi na kina Xavi au Iniesta, ana ubora mkubwa sana.”


Naye straika wa Yanga, Fiston Mayele alisema: “Huwa namuita Babu Kaju, Anajua sana mpira. Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana, anafanya mambo magumu yaonekane mepesi.”

Mayele pia alisema lengo la Yanga kwanza ni kutwaa ubingwa, kisha ndio tuzo binafsi ya ufungaji bora.
______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad