5/02/2022

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kibwana ni Kapombe wa miaka 10 iliyopita
 
TANZANIA tuliteketea kwa mabao 2-1 dhidi ya Msumbiji pale mjini Maputo mwaka 2014. Aliyekuwa beki wa kulia wa Tanzania jioni ile, kijana mdogo wa miaka 22, Shomari Kapombe aliketi juu ya nyasi za uwanja wa EStadio do Zimpeto kumwaga machozi akisikitika kile kilichotokea.

Msumbiji waliikatisha safari ya Tanzania kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika kwa idadi ndogo sana ya mabao. Nyumbani Tanzania tulitoka sare ya 2-2 kisha tukafungwa 2-1 Maputo, tukaondoshwa kwa jumla ya mabao 4-3.

Akiwa na sura ya kivulana, Kapombe aliyeteseka sana jioni ile hakuwa na kingine cha kufanya kupunguza machungu zaidi ya kulia. Achilia mbali machungu ya matokeo yaliowaumiza watanzania wote, Kapombe alikuwa na machungu binafsi ya mateso aliyokutana nayo kutoka kwa kiungo wa kushoto wa Msumbiji Elias Pelembe.

Aliyemwona Kapombe usiku ule pale Maputo asingeamini siku moja anaweza kuwa beki bora wa pembeni kulia nchini. Hapohapo Maputo miaka nane nyuma, tulibahatisha suluhu dhidi ya Msumbiji baada ya kukimbizwa sana katika mchezo wa kufuzu mashindano ya mataifa Afrika.


 
Katika benchi la Tanzania alikuwepo Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Unajua kwa nini Cannavaro alianza benchi? Kwa sababu mabeki wa kati walioanza siku ile, Victor Costa na Salum Swedi walimzidi Cannavaro uwezo, umri na uzoefu. Nani angekubali Cannavaro acheze mbele Costa na Swedi?

Miaka miwili mbele, Cannavaro alikuwa akiombwa jezi na Samuel Eto’o wa Barcelona kule Yaoundé Cameroon baada ya kumkabili vizuri katika mapambano mawili ya Dar es Salaam na Yaoundé.

Katika benchi la Tanzania siku ile walikuwepo Kelvin Yondani na Erasto Nyoni. Wangecheza wapi mbele ya Salum Swedi na Nadir Canavaro?


Miaka ilisogea na kila mtu anafahamu Yondani na Nyoni walikuja kuwa kina nani nchini. Kipo kipindi tuliwaomba wasistaafu. Kisa? Walikuwa mabeki muhimu zaidi kikosini kwa sababu ya uwezo na uzoefu waliokuwa nao.

Uzoefu ulikuja kwa Yondani na Nyoni baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo katika klabu zao na timu ya taifa. Ni kama ambavyo Cannavaro aliibuka kuwa beki mzuri baada ya kucheza mechi nyingi za ndani na za kimataifa akiwa na Yanga na jezi ya timu ya taifa. Ni kama ambavyo leo tunamtazama Kapombe kama beki bora wa kulia nchini baada ya kucheza mechi nyingi akiwa na jezi za Azam, Simba na timu ya taifa.

Hapo tunajifunza kumbe uwezo pekee haukufanyi kuwa mchezaji bora. Kumbe unahitaji kuongeza na uzoefu kukamilika. Kumbe tuna wachezaji vijana tunaodhani ni kawaida leo wanaoweza kuja kuibuka kuwa wachezaji muhimu siku za mbele kwa klabu zao na timu ya taifa kama ambavyo ilikuwa kwa kina Canavaro. Kumbe Shomari Kibwana anaweza kuwa Shomari Kapombe wa miaka ijayo. Unashangaa?

Mtandao wa Wikipedia unaonyesha Kibwana amezaliwa Novemba 2000. Kwa maana hiyo miezi nane ijayo atatimiza miaka 22. Ni katika umri huo Shomari Kapombe alikuwa akilishwa nyasi na winga wa Msumbiji kule Maputo.


 
Kipindi kile Kapombe alikuwa kama Kibwana wa leo. Hakuelewa baadhi ya mambo ya msingi anayopaswa kufanya kama beki wa pembeni. Kadiri muda ulivozidi kwenda ndivyo alivozidi kuimarika hadi alipofika leo. Hapo tunajifunza athari za kukosa mechi za kutosha katika mashindano ya vijana. Pengine kama Kibwana angepata mechi za kutosha za ndani na za nje katika mashindano ya vijana, labda angekuwa mbali zaidi ya alipo leo.

Pengine wachezaji wetu wangeimarika mapema zaidi kama wangepata mechi nyingi za kimashindano wakiwa vijana. Hili lingewarahisishia kupata nafasi ya kwenda nje wakiwa na umri mdogo. Lakini hata huyu Kibwana ninayetabiri anaweza kuja kuwa Kapombe, itawezekana kama tu atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Bahati mbaya yupo Yanga ambapo nafasi ya kuvumiliwa ni ndogo.

Inabidi apambane na wachezaji wa kimataifa walioimarika kama ilivyo sasa kwa Djuma Shaban. Si kazi rahisi sana! Bahati mbaya nyingine ni kwamba hawezi kwenda katika klabu ndogo kwasababu ya tofauti kubwa ya kiuchumi iliyopo katika Simba, Yanga, Azam na vilabu vingine.

Hawezi kupata maisha anayoyapata Yanga akiwa Namungo.


Tunapaswa kuondokana na ligi maskini kwa ajili ya kulinda vipaji.


HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger