6/08/2022

Bernad Membe Ala Kiapo "Sibanduki tena CCM hadi nife"

JIUNGE NA GROUP LA TELEGRAM LA AJIRA YAKO KUPATA AJIRA MPYA ZINAZOTANGAZWA KILA SIKU BONYEZA HAPA
“DHAMIRA yangu ya kukitumikia chama hadi nitakapokwenda kaburini ipo pale pale. niliondolewa CCM nilisikitika sana… nilisononeka na ninyi mlisikitika na mkasononeka pia.”

Ni ushuhuda wa aliyewahi kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2015 kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe.

Membe mwana CCM mkongwe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika awamu ya nne, alivuliwa uanachama Februari 2020.

Sababu zikitajwa kuwa uamuzi huo ulichukuliwa dhidi ya kada wake ni kutokana na mienendo yake katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2014.

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, iliyokutana Februari 28, 2020, iliazimia Membe kufukuzwa uanachama baada ya taarifa ya ndani ya chama hicho kuonyesha mwenendo wake kuanzia 2014 kutoridhisha, ikibainisha kuwa aliwahi kupata adhabu nyingine lakini hakujirekebisha wala hazikumsaidia.


Baada ya kuvuliwa uanachama Julai 15, 2020 alijiunga na ACT-Wazalendo akawa mshauri mkuu na mwishoni aliteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho.

Machi mwaka huu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ilimsamehe na kumrudishia uanachama baada ya kufuatilia mienendo yake na kuridhika.

Akizungumza wakati akikabidhiwa kadi yake na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, mwishoni mwa mwezi uliopita mkoani Lindi, anasema amefarijika kurejeshewa kadi yake.


“Nimefarijika kati ya Machi 30 na Aprili mosi , mwaka huu niliitwa Dodoma kwenye kamati ya maadili nikapewa nafasi na Rais na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, nizungumze na wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ili nieleze chochote nilichokuwa nacho kuhusiana na kurejea nyumbani,”anasema Membe.

Anamshukuru Mwenyekiti wa Chama kwa kumpatia nafasi ya kuzungumza na kuazimia kwa kauli moja kurejea CCM.

“Nimerejea CCM kwa sababu mbili ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini kwamba nirejee CCM nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya taifa na mikoa nirejee nyumbani , nilishauriwa na marafiki wa bara na visiwani kila aliyeniona ,wanachama wa CCM walinishauri nirudi CCM,”anasema Membe.

Kutokana na ushauri wote huo hakuwa na namna nyingine bali ni kutii mawaidha na ushauri wa viongozi wa chama, viongozi wa dini walimweleza, kumuomba na kumshauri arudi CCM amekubaliana na ushauri wao na amerudi rasmi, anaongeza Waziri wa Mambo ya Nje mstaafu.


Anasema sababu ya pili ya kurudi ni kutokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini.

“Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana nanyi mlisononeka sababu zilizonifanya niondoke CCM hazipo tena Narudia hazipo tena nimerudi namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu kunirudisha nimerudi kwenye chama ambacho nimezaliwa, kukulia na kusomeshwa,” anasema.

Anaongezea :“Ninaahidi sitaondoka tena nitabaki CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu nitaendelea kukitumikia chama changu kushirikiana na mbunge wangu Nape Nnauye. Mwaka 2015 niliahidi kuwaletea Nape nikamleta. Mtama sasa mtakuwa na wabunge wawili mbunge wetu Nape na mimi nitakuwa mbunge wa chini chini.”

NAPE NA MACHUNGU

Mbunge wa jimbo la Mtama ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, anasema baada ya Membe kuondoka kwenye chama wananchi wengi walichukia, ingawa aliwaomba wasichukie akiamini ipo siku atarejea.


“Mwenyezi Mungu ameturudishia faraja watu wa Londo, Chiponda... Mtama ni wastaarabu na hatuna shida tena, tuna imani kubwa na Membe, alinikabidhi kijiti na kuvaa viatu vyake, kulikuwa na mambo yaliyokwama huku nyuma kwa sababu za kisiasa, lakini Mama Samia amekuja ameziondoa,” anasema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mtama kushikamana, fitina ambazo ziliingia kati zimekwisha.

“Membe amenipigania katika mambo mengi, nilipotaka ubunge Ubungo baada ya kuonekana fitna zimeingia katikati Membe aliamua kuchora ramani.”

Anaongezea kuwa:“Ndio maana safari yangu ya ubunge imekuwa nyepesi. Kaka Membe amenipigania sana na bahati nzuri amerudi CCM.”

AKABIDHIWA KADI

Shaka anasema Membe amerudishwa CCM kwa kufuata utaratibu ikiwamo kujadiliwa na tawi lake na vikao vya ngazi ya juu.


Anasema Membe na wanachama wengine zaidi ya 1,670 walivuliwa uanachama wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, hivyo wanaweza kukabidhiwa kadi zao kwenye matawi yao.

“Kurejea Membe ndani ya Chama Cha Mapinduzi ni kuendelea kuwa na chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususani kwa wanachama wa jimbo la Mtama,”anasema Shaka.

AONYA MADIWANI

Shaka anawataka madiwani wa CCM nchini kuhakikisha wanasimamia maslahi mapana ya wananchi wao hilo ni jambo la msingi.

“Kumekuwa na changamoto kwa ndugu zetu madiwani wanajisahau wakifika huko…alilolieleza wananchi wapo sahihi kwa asilimia 70 wapo baadhi ya madiwani wakifika huko kwenye Halmashauri, majiji, manispaa wanasahau kilichowafikisha huko ni wananchi,”anasema.

Anaongeza kuwa: “Simamieni gharama za miradi na iweze kuwafikia wananchi na manufaa yake yaweze kuonekana yapo maeneo kadhaa madiwani hawatimizi wajibu wao niwaombe madiwani wa CCM kutimiza wajibu wao kwa wananchi.”

Shaka anasema mpaka wananchi wanaona udhaifu huo kuna sehemu hawafanyi vizuri na kazi ya kiongozi ni kujitathimini na kuona mambo hayaendi vizuri unajipanga upya.

“Ninyi ndiyo wasaidizi wa Rais Samia, sote tutimize wajibu wetu wa kuwatumikia wananchi hawa wametuweka katika hiyo nafas,” anasema Shaka.

Shaka alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia baadhi ya viongozi kutotoa ushirikiano kwa wananchi licha ya kwamba wao ndiyo wamewaweka madarakani.

“Nikiri kweli kuna tatizo la baadhi ya viongozi lakini tayari hatua zimeshachukuliwa na kuanzia hivi sasa viongozi hawa wanaochaguliwa watapatiwa mafunzo ili wawe na uwezo na ujuzi wa kutosha,” anasema.

Mwanachama Mzee Bakari Omar Bakari, anaeleza kuwa kuna tatizo la baadhi ya viongozi wa chama akiwemo diwani wao kupungukiwa na sifa za kiuongozi.

Anasema tatizo la Lindi wana viongozi ambao wamewachagua wakati wa kampeni lakini elimu zao ni ndogo wanatekwa na wakuu wa idara.

“Kila kitu kitakachokuwa kinaulizwa kinahusu elimu bila kuwa na elimu huwezi kuleta maendeleo tujitahidi kupata viongozi wenye elimu ya kutosha ili waweze kututetea wananchi ambao wapo chini kwenye malalamiko mengi ,”anasema Bakari.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger