6/18/2022

Hoja Tano za Moto Bajeti ya Serikali

JIUNGE NA GROUP LA TELEGRAM LA AJIRA YAKO KUPATA AJIRA MPYA ZINAZOTANGAZWA KILA SIKU BONYEZA HAPA


By Sharon Sauwa


Dodoma. Mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 ulianza jana bungeni, huku hoja tano zilizoibuliwa zikionekana kuwa moto zikigusiwa na wabunge tofauti.


Hali ikiwa hivyo bungeni, nje ya Bunge wadau wa bajeti, wakiwemo wafanyabiashara wenye viwanda, wataalamu wa uchumi na vyama vya siasa wameendelea kuichambua bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni Jumanne na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Mwigulu Nchemba


Miongoni mwa hoja hizo ni kuhusu nia ya Serikali ya kutaka wateule wanaoenguliwa kurudi kwenye mishahara yao ya zamani badala ya kuendelea na waliyokuwa wakilipwa wakiwa kwenye wadhifa.


Nyingine ni ya maofisa wa Serikali kukopeshwa magari ya ofisini ikilenga kubana matumizi na suala la kuondolewa kwa asilimia tano kati ya 10 ya fedha za mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu kupitia halmashauri.


Pia, suala la kodi limeibua mambo mbalimbali kama kutoza asilimia mbili ya kodi kwenye madini, usafirishaji wa wanyama hai na uamuzi wa kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 awe na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) ili alipe kodi pale anapokuwa na kipato.


Mbunge wa kwanza kuchangia baada ya Kamati ya Bajeti kuwasilishi taarifa yake alikuwa Janejelly Ntate, mbunge wa Viti Maalumu ambaye alisema suala la kuwaondolea mshahara wateule wa Rais pale wanapoondolewa kwenye nafasi zao halitaleta tija.


“Hili linakwenda kuleta mgogoro kati ya watumishi na Serikali yao na vyama vya wafanyakazi,” alisema.


Alisema ukimhamisha mtumishi kutoka taasisi ya umma ambako kuna mshahara mkubwa na kumpeleka serikalini, hapunguziwi mshahara, lakini kwa wateule, Serikali inataka wapunguziwe mshahara pale wanaposhushwa madaraka.


“Jambo hili haliwezekani, Serikali ilitazame upya,” alisema.


Alisema Serikali kama inataka tatizo hili lisitokee, inapaswa kurudi kwenye mfumo wa zamani, ambapo wakurugenzi walikuwa wanachujwa na menejimenti ya utumishi wa umma tofauti na sasa.


“Hivi sasa hawa wateule mfano wakurugenzi wanateuliwa tu na mamlaka ya uteuzi, ndiyo maana mambo hayaendi sawa.


“Turudi kule tulikotoka, haya mambo ya fulani kaharibu toa, hayatakuwepo,” alisema mbunge huyo.


Mbunge huyo alishauri ili kushusha mshahara wa mtumishi, inatakiwa tume iundwe ambayo itatoa adhabu zitakazoakisi kitu ambacho Serikali inataka kufanya.


“Tume itajadili adhabu zitakazomfanya huyu mtumishi ashushwe cheo na apunguziwe mshahara kwa mujibu wa sheria au afukuzwe kazi, hivyo naiomba Serikali iliangalie hili upya,” alisema.


Lakini mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Judith Kapinga alisema ni vizuri vijana waandaliwe kushika nafasi za uongozi.


Hata hivyo, alisema hiyo haimaanishi kuwa vijana hawawezi kushika nafasi za uteuzi zinazopatikana serikalini.


“Nataka kushauri kama huyu mtu wakati wa uteuzi alikuwa katika nafasi ya juu serikalini, basi arudishwe katika nafasi ile, lakini si lazima nafasi zote za uteuzi zitoke serikalini.


Alisema wapo watu wa sekta binafsi ambao pia wanaweza kuteuliwa lakini waanze na mshahara utakaokuwa umepangwa na Serikali,” alisema Kapinga.


Hoja ya TIN


Katika hatua nyingine, Twaha Mpembenwe, mbunge wa Kibiti, alisema suala la kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 kuanza kulipa kodi limeleta mtafaruku ndani ya jamii na kuomba suala la kuwapa TIN vijana hao liwekwe wazi zaidi kwa Watanzania.


Alitolea mfano wa Uingereza kuwa kila anayefikisha miaka 18 anapewa kadi ya Taifa ya Bima na wanafanya hivyo ili mfumo umtambue mwanafunzi wakati anapomaliza masomo yake na kwenda kufanya kazi.


Akichangia hoja hiyo, Jerry Silaa, mbunge wa Ukonga, alisema kwa tabia ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuwaambia Watanzania kuwa kila mwenye umri wa miaka 18 apatiwe TIN wanajua watafanyiwa wanayofanyiwa wafanyabiashara.Hoja ya magari


Jambo jingine lililoibuka ni la watumishi wa umma kukopeshwa magari ili wayahudumie wao na kupunguza matumizi ya Serikali, ambalo Janejelly alitoa tahadhari kwa Serikali kuwa huenda suala hilo lisiwe na afya.


Alisema hoja hiyo ilishawahi kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tatu, lakini Taifa lilipoteza viongozi wengi kutokana na ajali.


“Unakuta huyu kiongozi anatoka ofisini amechoka, anajiendesha mwenyewe kwenda nyumbani, anagongwa, saa nyingine anawaza mkuu wake wa kazi kampa mikakati ya ajabu ataifanyaje, mwishoni anagonga magari.


“Hili tuliangalie kwa mapana,” alisema.

Usafirishaji wanyama hai


Katika hatua nyingine, Silaa alizungumzia sauala la usafirishaji wa wanyama, akishauri kuimarisha mawasiliano ili kuepuka mambo yaliyojitokeza hivi karibuni, ya kuruhusu usafirishaji huo na baadaye ruhusa ikafutwa.


Alisema walikwenda Muheza mkoani Tanga na kukuta wasafirishaji wa vipepeo wanaathirika na zuio la Serikali la kusafirisha wanyama hai.


“Juzi Serikali ilitoa kauli hapa. Mimi nilielewa ni kusaidia wale wa vipepeo na wanaoshika mijusi na wanyama wengine wadogo, lakini kwa sababu haikushirikisha, ikatengeneza taharuki na Waziri wa Maliasili Dk Pindi Chana naye akajaa upepo akafuta lile agizo,” alisema.


Alisema matokeo yake waliokuwa wakisherehekea kufunguliwa kwa zuio hilo wakarudi tena kwenye masikitiko ya zuio la mwaka 2018.
Kodi ya wachimbaji wadogo


Vilevile, mbunge huyo wa Ukonga alisema kuongezwa kwa kodi ya asilimia mbili na kodi nyingine wanazotozwa wachimbaji wadogo, kunafanya kodi watakazotozwa kuwa asilimia tisa.


Mikopo ya halmashauri


Agnes Marwa, mbunge wa viti Maalumu yeye alilia na Serikali akitaka iangalie mahali itakakotoa asilimia tano ya fedha za halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa maeneo ya wamachinga badala ya kuitoa kwenye asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.


Mwananchi

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger