6/17/2022

Maskini Kumbe Dereva wa Basi Alifariki Akiwa Anaendesha Kabla ya Basi Kupinduka

JIUNGE NA GROUP LA TELEGRAM LA AJIRA YAKO KUPATA AJIRA MPYA ZINAZOTANGAZWA KILA SIKU BONYEZA HAPA


DEREVA wa basi la kampuni ya Zuberi, Hamza Haule, amedaiwa kuugua na kufariki dunia akiwa kwenye usukani kabla basi hilo halijaanguka na kusababisha vifo na majeruhi.

Wananchi wakiangalia basi la Zuberi lenye namba za usajili T435 DJS, baada ya kupata ajali katika eneo la Mwigumbi, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga juzi na kusababisha watu watano kupoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Basi hilo lenye namba za usajili T435 DJS lilianguka juzi alasiri baada ya kugonga kingo za daraja eneo la Mwigumbi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na kusababisha watu watano kupoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando, alisema jana kuwa kwa taarifa za awali chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi hilo kupata tatizo la kiafya na kufariki dunia akiwa kwenye usukani.

Alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa ambazo jeshi hilo lilizipata na linaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli, zinadai kuwa dereva huyo kabla ya kuanza safari kutoka Mwanza kwenda Kahama, hakuwa vizuri kiafya na alipofika eneo hilo la Mwigumbi, alifariki dunia akiwa kwenye usukani.

"Ajali hii imegharimu maisha ya watu watano, watu wawili wamefia hapo hapo kwenye eneo la tukio, na watu watatu walifia hospitalini.


"Ninatoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto wawe wanachunguza afya zao kabla ya kuanza safari na endapo wakiwa hawajisikii vizuri, wasiendelee na safari ili kuepusha ajali zisizo za lazima," alisema.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, akiwamo Daniel Sewe, walisema walipofika kwenye eneo hilo la Mwigumbi, basi lilipiga tuta na kuanza kuyumba kisha kupoteza uelekeo na kugonga kingo za daraja, likapaa juu na kuanguka.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dk. Masunga Maneno, alisema hadi sasa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni watano - watu wazima wanne na mtoto mmoja na walipokea majeruhi 26. Kati yao, 13 walitibiwa na kuruhusiwa.


Katika ajali hiyo, miongoni mwa waliofariki dunia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Ng'hama iliyoko Mwalukwa wilayani Shinyanga, Kassam Kassam, huku Mwalimu Mashaka Kasomeko wa Shule ya Msingi Bulambila wilayani humo, akivunjika mkono wa kushoto. Walimu hao walikuwa wakitoka Mwanza waliokwenda kushiriki semina ya elimu jumuishi.

Watu wengine wanne ambao wamefariki dunia katika ajali hiyo, bado hawajatambuliwa majina yao na miili yao iko kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Kolandoto.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger