Profesa Kitila: Nilifukuzwa shule kwa kukosa ‘buku mbili’ za ada

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA




Dodoma. Kitila Mkumbo alipofukuzwa shule kwa kukosa Sh2,000 mwaka 1989 hakuna aliyefahamu kwamba angekuja kuwa msomi mbobezi nchini lakini kama wahenga walivyosema, maisha ni safari ndefu.

Mbunge huyu wa Ubungo (CCM) anasema aliipata kadhia hiyo akiwa kidato cha pili katika Sekondari ya Mwenge alikokuwa anasoma kipindi hicho.

Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye ofisi za Mwananchi jijini hapa juzi, Profesa Mkumbo alisema anaguswa zaidi na mijadala ya elimu kutokana na kumbukumbu hizo za kufukuzwa shule kwa kukosa ada.

“Wakati sikuwa na wazazi kwa hiyo nilisoma kwa kusaidiwa leo na mjomba, kesho fulani hivyo niliungaunga tu,” alisema Profesa Kitila.


 
Baada ya kufukuzwa shule, anasema ilimlazimu kuingia mtaani kutafuta vibarua ili apate ada kumwezesha kuendelea na masomo ya sekondari.

Licha ya kujitahidi hizo anasema hakufanikiwa kupata kibarua kumwezesha kulipa ada aliyokuwa anaitafuta. Akaungana na rafiki yake mmoja kuendelea kutafuta cha kufanya bila mafanikio.

Siku moja, baada ya mizunguko anasema walienda kunywa maji kwa dada wa rafiki yake na wakamsimulia kilichomsibu. Aliposikia kisa hicho, anasema dad huyo alimpa Sh2,700 akiimweleza Sh2,000 akalipe ada na Sh700 kwa matumizi yake.


“Nakumbuka maneno ya huyo dada alisema ‘kila siku mimi natumia Sh5,000 kunywa bia kumbe kuna mtu anakosa Sh2,000 ya kulipa ada.’ Akavuta droo na kunipa Sh2,700 kwa ajili ya ada na matumizi mengine,” alisema.

Profesa Mkumbo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya awamu ya Tano, alisema mpaka sasa wanaishi kama ndugu.

“Hapa nilipo mimi ni zao la elimu, isingekuwa elimu nisingekuwa kitu. Naamini silaha ya kuikomboa nchi hii na kuitoa katika umasikini ni elimu ndiyo maana nilipigania kufuta ada ya sekondari,” alisema.

Harakati za kutaka ada ifutwe anasema alizianza tangu mwaka 2010 alipokuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndipo Hayati John Magufuli akaifanyia kazi naye anamwona ni shujaa wake.


 
Alisema uamuzi wa kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ni ujasiri mkubwa na anamheshimu kwa sababu ameokoa maelfu ya Watanzania waliokuwa wanashindwa kuwalipia ada watoto wao.

Alisema hiyo ndio sababu pia katika jimbo lake suala la elimu ni kipaumbele cha kwanza na mwaka huu atatumia Sh3.5 milioni kuwalipia ada wanafunzi wa kidato cha sita kwani Sh2,000 alizopewa anasema zilimwongezea ari ya kusoma kwa bidii baada ya kubaini hana kitu kingine cha kutegemea.

“Nilikuwa na maisha ya upweke si unafahamu ukiwa hauna ndugu. Mimi tukifunga shule badala ya kwenda nyumbani nilibaki shuleni. Kilichokuwa kikinipa faraja ni uongozi kwani nikiwa kidato cha pili nilikuwa kiranja,” alisema.

Anasema alikuwa anasoma sana na ilimsaidia kuwa mzungumzaji mzuri katika midahalo na alikuwa kiongozi wa klabu ya Kingereza Mkoa wa Singida hali iliyomsaidia kutoogopa kujenga hoja maishani mwake na ambayo watu wanaikimbia yeye hupambana nayo.


“Ndio maana mtandaoni watu wanalikimbia jambo lakini mimi nalijadili kwa sababu mimi ni zao la klabu za majadiliano. Sasa vijana wa leo hawajajengwa katika mijadala ndio maana wana matusi na dharau,” alisema.

Sikukidhi kuwa mhadhiri Udsm

Profesa Mkumbo anasema hakuwa na sifa ya kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kwa sababu alifaulu kwa GPA ya 3.5 na ili upate nafasi ya kufundisha chuo kikuu lazima uwe na GPA ya 3.8 na alipanga kwenda kufundisha Sekondari ya Nganza iliyopo mkoani Mwanza mara tu baada ya kuhitimu chuo kikuu.

“Profesa Daniel Mkude, akiwa naibu makamu mkuu wa chuo wa utawala aliniita akaniuliza naenda wapi...nikamuonyesha barua kwa furaha kwamba naenda zangu kufundisha Nganza. Akacheka sana, akasema wewe utafukuzwa ndani ya mwezi,” alisema.

Alisema Profesa Mkude alisisitiza kuwa yeye (Profesa Mkumbo) hawezi kwenda kufundisha katika shule hiyo kwa kuwa alimfahamu mikiki yake aliyokuwa akiifanya alipokuwa rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso).

“Alijua kuwa siwezi kutulia ningeenda kugombea urais Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Nikamuuliza sasa ninatakiwa nifanyaje? Akaniambia sehemu pekee ya wewe kufanya kazi ni chuo kikuu huko ndiko kutakakokufaa,” alisema.


 
Anasema naibu huyo alimweleza asubiri amfanyie utaratibu abaki chuoni hapo. Alimpigia simu mtu mmoja akamweleza “Mkumbo abaki katika ofisi ya wanafunzi kwa sababu alikuwa ana uwezo sana wa kuwaongoza wanafunzi.”

Hivyo ndivyo alivyobaki chuo kikuu ambako baadaye alisoma shahada ya pili. Ingawa hakuwa na sifa za kupata ufadhili ambazo zilitaka mwanaume afaulu kwa GPA 4.2 na wanawake GPA 3.8 lakini marehemu Profesa Matthew Luhanga na Profesa Mkude wakajadiliana kuwa Mkumbo anao uwezo mkubwa angeweza kupata GPA 4.2 ila kwa sababu ya Daruso ndio maana alishindwa kulipata daraja hilo.

Anasema wawili hao walipendekeza apewe ufadhili huo na majina yalipotoka, lake lilikuwa la kwanza katika orodha licha ya GPA yake ya 3.5.

“Watu walishangaa lakini nilipata kwa sababu wale wazee waliona nilipata GPA hiyo kwa sababu ya Daruso. Baada ya kumaliza masters nilienda kwa Profesa Akindael Mbise kumuomba nijitolee kusimamia semina za wanafunzi,” anasema.

Ombi hilo anasema lilimgusa Profesa Mbise kwa sababu watu wengi hawataki kujitolea. Anasema alijitolea kwa mwaka mzima hata wanafunzi wakampenda.

“Baada ya kumaliza mwaka mmoja Profesa Mbise akaniambia kwa nini nisihamie kwenye ualimu. Nikasema napenda sana kuwa mwalimu lakini GPA yangu hoi, akaniambia kama unapenda niachie mimi hiyo kazi,” anasema.

Alisema Profesa Mbise alipokwenda kuuza hoja hiyo kwa Profesa Luhanga alimsifia (Mkumbo) kwa kusema ana akili sana hivyo akathibitishwa kuwa mhadhiri.

Alisema jambo hilo linamfanya kulikumbuka maishani kwa sababu wazee hao walikuwa viongozi wanaotambua vipaji vya vijana na kuvilea.

“Mimi bila wale wazee (profesa Luhanga na Profesa Mbise) nisingekuwa profesa leo hii. Kwa sasa hivi viongozi wetu wa vyuo vikuu kwa ninavyowaona wako rigid (hawanyumbuki) sana. Lakini mimi kwa mazingira yaliyopo leo nisingekuwa mwalimu wa chuo kikuu,” alisema.

Alisema wazee hao walitambua uwezo alionao zaidi ya alama ambazo zilikuwa kwenye karatasi na kutoa wito kwa viongozi wote kutambua vipaji na uwezo walioyonao zaidi ya alama wanazopata madarasani.


 


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad